Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutaendelea kuwasaidia wananchi wa Afghanistan: FAO

Nchini Afghanistan, licha ya kuwa eneo zuri kwa kilimo watu wengi awapati mazao ya kutosha
UNAMA/Eric Kanalstein
Nchini Afghanistan, licha ya kuwa eneo zuri kwa kilimo watu wengi awapati mazao ya kutosha

Tutaendelea kuwasaidia wananchi wa Afghanistan: FAO

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya umoja wa Mataifa yanayotoa misaada ya kibinadamu yameendelea kuwasaidia wananchi wa Afghanistan ambao wengi wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula  kutokana na machafuko nchini humo. Miongoni mwa mashirika hayo ni lile la chakula la Kilimo FAO.

“Lengo kubwa la FAO kwa mwaka 2021 ni kuendelea na kazi,tunaendelea na tumedhamiria kuendelea kubaki hapa na kusaidia.“ 

Ni Rajendra Kumar Aryal, mwakilishi wa FAO nchini Afghanistan akieleza dhamira yao ya kuendelea kutoa msaada nchini humo wakati huu ambapo inakadiriwa mtu mmoja kati ya watatu hana uhakika wa chakula kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo, janga la corona na kupanda kwa gharama za chakula.

Msaada wa mafunzo na pembejeo unaotolewa na FAO kwa kushirikiana na wadau wake umewanufaisha wakulima kama anavyosema mkulima huyu wa ngano Khialy Gul,“Tumepokea msaada huu wakati tunauhitaji.Tumesaidiwa kilo 50 za ngano, na mbolea ya kupandia na kustawisha”

Malek Nemat ni kiongozi wa jamii ya Kuchi anasema msaada uliotolewa kwa wafugaji umewasaidia kuacha kuuza mifugo kiholela ili kupata hela ya chakula.Hawa watu wamepokea viroba vya chakula cha mifugo yao ili kuweza kuilinda. Watu wanafuraha sana kuhusu hili kwasababu sasa chakula hicho kinaweza kulisha mifugo mpaka miezi miwili au mitatu. Hata kama mtu anasaidiwa kwa miezi 3, hayo ni mafanikio makubwa. “

Msaada wa fedha dola 50 hutolewa kwa wale wasiomiliki ardhi, wanawake na watu wenye ulemavu  wakiwa ni kipaumbele. Video ya FAO inamuonesha Nastaran akipokea mgao wake nakusema.“Tupo watu 6 kwenye familia, lakini ni mtu mmoja tuu mjukuu wangu ndio anafanya kazi nchini Iran. Tatizo letu ni kuwa hatuwezi kununua chakula na mahitaji muhimu. Fedha nilizopewa na FAO zitasaidia kununua kiroba cha mchele, mafuta ya kupikia Pamoja na mahitaji ya shule kwa mjukuu wangu.”

Licha ya mzozo unaoendelea, FAO imejitolea kuendelea kutoa msaada wa chakula na fedha kwa watu wenye uhutaji sana ili kuepusha kuzorota kwa hali ya uhakika wa chakula.