UNHCR tunafanya kila liwezekanalo DRC kuhakikisha hakuna mkimbizi anayekosa maji

28 Machi 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC limesema ingawa kuna changamoto, lakini linafanya kila jitihada kuhakikisha hakuna mkimbizi ambaye anaikosa huduma muhimu ya maji katika kambi za wakimbizi nchini humo. 

Kauli hiyo ni kufuatia wakimbizi warundi wawanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Lusenda tarafa ya Fizi katika jimbo la kivu kusini mashariki mwa DRC kuiomba UNHCR na wadau wake kuboresha huduma ya maji kambini humo kutokana na uhaba.  

Uhaba wa maji ni changamoto katika maeneo ya Lusenda na viunga vyake hali inayowafanya wakimbizi hao kuishi kwa mgao wa maji na kiwango cha maji huku wakidai wanachohudumiwa hakitoshi ukilinganisha na mahitaji.  

 

Mmoja wa wakimbizi katika kambi hiyo ni Bi. Manirakiza Bora akifahamiaka zaidi kama Mama Mlezi, amekuwa mkimbizi kambini Lusenda kwa miaka kadhaa na kero yake ni ukosefu wa maji akiomba shirika husika kuboresha huduma ya maji ndani ya kambi. “Kwa kweli kuna shida ya maji. Kuna wakati tunapata huduma ya maji mara tatu katika wiki. Na wakiyafunga inaweza kupita wiki nzima.” Anaeleza akiongeza kuwa kuna wakati maji hayo yanakuja yakiwa yamechafuka huku akiomba ikiwezekana maji yawepo kila siku.   

 

Licha ya UNHCR kuweka tenki za maji katika kambi hii ya Lusenda, bado kunaonekana kuwa na changamoto ya maji. Bwana Iranzi Olivier kiongozi wa kitengo cha kupokea malalamiko ya wakimbizi kambini hapa anasema kuwa uhaba wa maji “unasababisha wanawake kutembea mwendo mrefu kutafuta maji huku baadhi yao wakijikuta mikononi mwa wahalifu wanaowabaka.” 

 

Mwingine ni Bi. Munezero Shandra yeye anahofia magonjwa kutokana na maji kutokuwa na dawa ya kuua wadudu akisema, “maji kuna siku ambapo wakiyaachia unakuta hayana dawa na huwa wanatuambi maji bila dawa usinywe. Lakini sasa wakiyaachilia utafanyaje? Hatuna hela za kwenda kununua vidonge na sisi tunakunywa hivyo.” Kwa hivyo anaomba viongozi kushughulikia suala hilo. 

Mtoto mkimbizi akinawa mikono katika kituo cha Kavimvira huko Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kabla ya kurejeshwa nchini Burundi.
© UNHCR/Sanne Biesmans
Mtoto mkimbizi akinawa mikono katika kituo cha Kavimvira huko Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kabla ya kurejeshwa nchini Burundi.

 

Upande wa shirika la UNHCR Bi Rachel Criswell Afisa wa mawasiliano katika shirika hilo nchini DRC mjini kinshasa anasema shirika hilo linafahamu kuhusu matatizo ya maji katika kambi za wakimbizi ana anaeleza kuwa, UNHCR inadumisha dhamira yake ya kukaa na kuendelea na usaidizi katika kambi za wakimbizi. 

 

Bi Criswell anasema, sababu kubwa kwa nini hakuna maji ni kwa sababu jumuiya ya wenyeji imekatwa kutoka kwenye vyanzo vyake vya maji kutoka katika maeneo yasiyo salama. “Kwa kuongezea chemichemi hizi ni za jamii zote mbili na hakuna nafasi kubwa ya kusaidia kila mtu. Tunakumbuka kwamba maji ni muhimu sana kwa maisha ya raia katika sheria za kimataifa za kibinadamu na kwamba ni muhimu jumuiya inayowakaribisha watafute vyanzo vya maji.” Hata hivyo anasema UNHCR inadumisha dhamira yake ya kupeleka maji na usaidizi katika kambi za Lusenda na Mulongwe lakini hatuwezi kukidhi mahitaji yote ingawa kutokana na Malengo ya maendeleo endelevu “tunataka kweli kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma pamoja na kuungwa mkono kutoka serikali ya DRC na watendaji wa maendeleo katika hatua za mahitaji muhimu tarafani Fizi.” 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter