Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Burundi nchini DRC washukuru kupatiwa ardhi ya kilimo

Akarurimana James ni mkimbizi kutoka Burundi ambaye amenufaika na ardhi iliyotolewa na serikali ya DRC kwa ajili ya wakimbizi na wenyeji wao kwa lengo la kuimarisha kujitegemea.
UN/Byobe Malenga
Akarurimana James ni mkimbizi kutoka Burundi ambaye amenufaika na ardhi iliyotolewa na serikali ya DRC kwa ajili ya wakimbizi na wenyeji wao kwa lengo la kuimarisha kujitegemea.

Wakimbizi wa Burundi nchini DRC washukuru kupatiwa ardhi ya kilimo

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, serikali imetangaza kutenga ekari  500 za ardhi kwa ajili ya kilimo itakayotumiwa na wakimbizi kutoka Burundi pamoja na wenyeji, kwa lengo la kuimarisha hali ya kujitegemea na kuishi pamoja kwa amani. Kwa kiasi kikubwa wakimbizi hao wamekuwa wakitegemea msaada kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na jamii za wenyeji zinazowahifadhi wakimbizi hao.  

Taarifa hiyo iliyotangazwa Jumatatu ya tarehe 18 mwezi huu wa Aprili mjini Kinshasa imepokelewa kwa mikono miwili na wakimbizi.

Mwandishi wetu wa DRC Byobe Malenga, punde baada ya kutangazwa kwa ripoti hiyo alifika kambi ya wakimbizi ya Mulongwe na kuzungumza na mkimbizi Akarurimana James kutoka Burundi ambaye anasema kilimo ndio kazi kubwa anayotegemea katika maisha yake.

Bwana Akarurimana anasema, “mimi naweza kutoa shukrani kwa UNHCR kwa vile walitupatia nafasi ya kuishi, lakini sasa kile naweza omba kwa UNHCR ni kuangalia jinsi ya kuongeza usalama.”

Anasema “usalama ukiwa bora zaidi wanaweza kuishi kwa amani zaidi na kwamba hakutakuwa na shida. Maisha ya kambini ni mazuri tunaishi na kulima na kuvuna. Misaada ya UNHCR inakuja lakini kuna wakati inakawia kwa hiyo bila kilimo watu wanaweza kupata madhara sana.”

Hatua ya DRC kugawa mashamba kwa wakimbizi wa Burundi inakuja wakati tayari nayo Uganda imeshakuwa inapatia wakimbizi wanaoishi nchini humo.

Kilimo ni moja ya kazi inayokidhi mahitaji siyo tu ya wakimbizi walio katika kambi za Lusenda na Mulongwe lakini pia kwa raia wa DRC wanaoishi tarafa ya Fizi jimboni Kivu Kusini.