Hata nikikata pumzi sasa kile nimefanya kimetosha- Mshindi wa Nansen Afrika 2019

19 Septemba 2019

Mshindi wa tuzo ya wakimbizi ya Nansen kwa kanda ya Afrika kwa mwaka huu wa 2019 Evariste Mfaume, amesema hata siku akikata pumzi, kile ambacho ameweza kufanya kuleta utangamano kati ya wakimbizi na wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kitakuwa kimetosha. Tuzo hiyo ya Nansen hutolewa na shirika la kuhudumia wakimbizi duniani,  UNHCR.

Kutana na Evariste Mfaume mkazi wa Baraka eneo la Fizi jimbo la Kivu Kusini nchini DRC ambaye mwaka 2003 alianzisha shirika la kiraia la mshikamano wa wafanyakazi wa kujitolea kwa ajili ya utu, SVH.

Evariste ambaye naye alikuwa akihamahama kutokana na mapigano nchini DRC, alianzisha vijiji vya amani.

"Nimeshuhudia watu wakiuawa, watu wakibakwa. Mali za watu zikiporwa na kuharibiwa. Lakini pia mimi ni binadamu. Nilihisi kuna kitu lazima nifanye, ingawa sikuwa na uwezo, sikuweza kukaa kimya ilibidi nichukue hatua.”

Awali alijikita katika haki za binadamu na uanaharakati lakini baadaye akajumuisha utengamano wa amani kati ya wakimbizi na wakazi wa Fizi.

" Kulikuwepo na wakimbizi wa DRC nchini Tanzania na waliporejea hawakuwa na makazi.”

Sasa eneo lililokuwa msitu limegeuka makazi ya familia zaidi ya 19,000 katika eneo la Mwandiga DRC, wenyeji na wakimbizi wakiishi na kulima pamoja kwa amani. Mmoja wa wenyeji hao ni mkulima Ungwa Sangani.

"Tulikuwa na ubaguzi. Hatukuwa na upendo, lakini wakati tulichangia shamba, tulnakuwa pamoja, tulishajuana tulianza hakuna mawazo kwa magonjwa na furaha. Tulishakuwa pamoja.”

Na Evariste anasema kuwa, “najisikia ninatenda ubinadamu, na ninachangia kitu ndani ya ubinadamu. Siku ambayo pumzi hii itakuwa haipo kile ambacho nimefanya kitakuwa kimetosha.”

Wakimbizi na wenyeji sasa wakiwa wanatoka kwenye shamba la mihogo wakiwa na majembe yao, huku Evariste akiwa miongoni mwao wanasimama na kuanza kucheza ngoma, ishara ya furaha, maelewano na utengamano miongoni mwao.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter