Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN haina taarifa za uwepo wa silaha za kibailojia Ukraine

Izumi Nakamitsu, Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa kuenea kwa silaha akihutubia Baraza la Usalama kuhusu vitisho vya amani na usalama duniani.
UN /Manuel Elias
Izumi Nakamitsu, Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa kuenea kwa silaha akihutubia Baraza la Usalama kuhusu vitisho vya amani na usalama duniani.

UN haina taarifa za uwepo wa silaha za kibailojia Ukraine

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa hauna taarifa zozote kuhusu mipango ya silaha za kibailojia nchini Ukraine, amesema Izumi Nakamitsu, Mwakilishi wa ngazi ya juu wa umoja huo kuhusu udhibiti wa kuenea kwa silaha duniani.

Akihutubia Baraza la  Usalama hii leo, lililokutana kujadili vitisho vya amani na usalama duniani, mkutano ulioitishwa na Urusi, Bi. Nakamitsu amesema “tunatambua ripoti kutoka vyombo vya habari kuhusu madai ya uwepo wa mipango hilo lakini Umoja wa Mataifa hauna taarifa.”

Amesema kutokuwepo kwa mipango hiyo kunatokana na uwepo wa Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1972 kuhusu silaha za kibaiolojia, BWC, ambao unakataza kuendeleza, kuzalisha, kununua, kusafirisha, kuhifadhi na kutumia silaha za kibailojia au za sumu.

Bi. Nakamitsu amesema Urusi na Ukraine zote ni wanachama wa mkataba huo na kwamba silaha za kibailojia zimepigwa marufuku tangu mwaka 1975 mkataba huo ulipoanza kufanya kazi.

Mwanamke akiondoa kifusi kwenye nyumba  yake huko Kyiv baada ya jengo lao kushambuliwa na makombora ya Urusi katika uvamizi wake wa Ukraine
© UNICEF/Anton Skyba for The Globe and Mail
Mwanamke akiondoa kifusi kwenye nyumba yake huko Kyiv baada ya jengo lao kushambuliwa na makombora ya Urusi katika uvamizi wake wa Ukraine

Mkataba wa silaha za kibaiolojia una kasoro

Hata hivyo amesema mkataba huo una kasoro ambazo zinapaswa kushughulikiwa ili uweze kuwa thabiti zaidi. 

“Mkataba hauna mfumo wa kimataifa wa kuthibitisha ambao unasimamiwa na taasisi huru kama ilivyo shirika la kimataifa la kuzuia silaha za kemikali, OPCW. Kwa hiyo kutathmini uzingatiaji wa mkataba ni wajibu wa nchi mwanachama pekee.”

Amesema ni kwa hali hiyo anasihi nchi wanacham awa BWC kushiriki mkutano wa 9 wa tathmnini ya mkataba huo uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu huko Geneva, USwisi ili kuangalia upya mkataba na hatimaye uweze kukabili changamoto za sasa na zijazo.

Vuta nikuvute Barazani kuhusu madai ya Urusi

Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Nebenzia Vassily Alekseevich akihubitia Baraza amedai kwamba Marekani inasaidia mipango  ya silaha za kibailojia nchini Ukraine sambamba na mipango ya kutumia ndege wanaohamahama kusambaza virusi na vimelea vya magonjwa kama vile homa ya mafua ya ndege.

“Tumegundua kuna maabara za kibailojia zenye vijidudu ambapo hatua zinafanyika kuviimarisha vijidudu hivyo vitumike kama silaha,” amedai bwana Alekseevich.

Hoja yake ilipingwa vikali na Albania ambayo mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Ferix Hoxha amesema “taarifa za Urusi kwenye Baraza hili ni uzushi mtupu na hatuna muda wa kupoteza kujadili. Malengo ya Urusi yanachukiza kama ilivyo mbinu zake kwenye operesheni zake dhidi ya Ukraine.”

Marekani ikapata fursa ya kuzungumza ambapo Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Linda Thomas-Greenfield amesema “Urusi imeomba mkutano huu kwa lengo la kusambaza uongo. Mmesikia kutoka kwa Bi. Nakamitsu kuwa UN haina taarifa za mipango ya silaha za maangamizi huko Ukraine.”

Balozi Thomas-Greenfield amesema utabiri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken umetimia, “ya kwamba Urusi itabuni kitu cha kudai matumizi ya silaha za maangamizi.”

Amesema kile ambacho Marekani inashirikiana na Ukraine ni maabara za utafiti wa magonjwa kama vile COVID-19, tafiti ambazo zinasaidia kila mtu.

Akiunga mkono kauli hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa Balozi  Sergiy Kyslytsya amesema mifumo yote ya kiafya nchini Ukraine inazingatia kanuni na wajibu wa kimataifa na inaendeshwa kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa husika.

“Mengine yote hayo mnayosikia ni kiwewe cha Vladmir Putin na washirika wake ambao ni pamoja na ujumbe wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa. Urusi haijali chochote kuhusu usalama wa raia wake, wakiwemo maelfu ya miili ya askari wa kirusi inayoharibika, askari ambao wamesimama kidete na Putin wakati huu wa janga linaloendelea Ukraine,” amesema Balozi Kyslytsya

Ufaransa, Uingereza nao walipinga madai ya Urusi huku India ikisisitiza mazungumzo ili kumaliza mapigano yanayoendelea.

Mtoto mchanga akipimwa uzito katika hospitali moja nchini Ukraine tarehe 7 mwezi Machi mwaka huu wa 2022
UNICEF/Andriy Boyko
Mtoto mchanga akipimwa uzito katika hospitali moja nchini Ukraine tarehe 7 mwezi Machi mwaka huu wa 2022

Dicarlo na diplomasia

Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya siasa, Rosemary Dicarlo pamoja na kuzungumzia kiwango cha athari za mashambulizi hayo yaliyoingia siku ya 15 hii leo, ikiwemo mauaji, majeruhi na uharibifu wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi, amesisitiza suala la diplomasia.

“Katibu Mkuu anashukuru mno kwa nchi nyingi wanachama ambazo zinatumia diplomasia kumaliza mzozo huu. Anaendelea kuwasiliana na mara kwa mara na viongozi wa kikanda na viongozi wengine katika kufanikisha hilo,” amesema Dicarlo.

Amesisitiza tena azma ya Umoja wa Mataifa ya kutambua mamlaka, uhuru na mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa na kusema, “kadri vita inavyoendelea, tayari kuna taswira ya madhara yake kwa zaidi ya kile kinachoendelea Ukraine.Tunaendelea kusikia matumizi ya maneno kama vile, wakati ndio huu sasa, kutoweka kwa ushirikiano wa kimataifa. Naamini hii si kutia chumvi. Baadhi ya madhara yako dhahiri kiuchumi na kisiasa. Nadhani kinachotia hofu zaidi ni hatari yake katika amani na usalama duniani.”

Bi. Dicarlo amesema hatua zote zichukuliwe ili kusaka suluhu na kumaliza vita hiyo iliyoanza tarehe 24 mwezi uliopita wa Februari, “na tuanze hivyo sasa.”