Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yafuatilia kwa karibu hali katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia

Maandamano jijini New York, nchini Marekani kupinga uvamizi wa Urusi huko Ukraine
Unsplash/Roman Shavnya
Maandamano jijini New York, nchini Marekani kupinga uvamizi wa Urusi huko Ukraine

UN yafuatilia kwa karibu hali katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejulishwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa ripoti za mapigano makali kwenye maeneo yanayozunguka mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia nchini Ukraine, mtambo ambao ni mkubwa zaidi barani Ulaya.
 

Mkuu wa Idara ya masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary Dicarlo amesema hayo leo akihutubia Baraza hilo lililokutana kufuatia ombi la Ukraine wakati huu ambapo jana usiku majeshi ya Urusi yalirusha makombora kwenye jengo Jirani na mtambo huo wa nyuklia.

Bi. Dicarlo amesema operesheni za kijeshi kwenye maeneo ya nyuklia na maeneo ya raia siyo tu hayakubaliki bali pia ni ukosefu mkubwa wa uwabijikaji.

Amesema kila juhudi zinapaswa kuchukuliwa kuepusha janga la nyuklia kama ilivyokuwa kwenye mtambo wa Chernobly mwaka 1968 huku akipongeza juhudi za shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA la kufuatilia hali ya usalama kwenye mtambo huo.

Hadi sasa hakuna miali iliyovuja kutoka kwenye mtambo- IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafaeli Grossi akihutubia Baraza la Usalama akiwa kwenye ndege akielekea Tehran, Iran kikazi. Baraza lilikutana kujadili Ukraine.
UN WebTV
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafaeli Grossi akihutubia Baraza la Usalama akiwa kwenye ndege akielekea Tehran, Iran kikazi. Baraza lilikutana kujadili Ukraine.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi akihutubia wajumbe wa Baraza akiwa kwenye ndege kuelekea Tehran, Iran kikazi amethibitisha kuwa operesheni katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia zinaendelea kama kawaida licha ya mashambulizi ya jana.

“Wadau wa Ukraine waliijulisha IAEA kuwa kombora lililorushwa usiku wa jana lilipiga jengo kwenye moja ya vinu vya mtambo huo na kusababisha moto ambao hata hivyo baadaye ulizimwa,” amefafanua Bwana Grossi.
Kinachofanyika sasa IAEA inaendelea na mawasiliano na mamlaka za Ukraine, ikiwemo serikali na zile zinazosimamia usalama wa nyuklia pamoja kampuni inayoendesha mtambo huo, mawasiliano ambayo ndio msingi wa taarifa zote tunazoendelea kuhusu hali ya usalama.”

Bwana Grossi ameelezea utayari wake wa kwenda Ukraine ili kushauriana na mamlaka husika pamoja na jeshi linalodhibiti mtambo huo ili kuhakikisha vigezo vya usalama vinazingatiwa akiongeza kuwa wanaamini kuwa wana wajibu wa kuitikia ombi la Ukraina la kusaidiwa katika kusimamia usalama wa mtambo huo.

Tunaunga mkono hatua za IAEA: Wajumbe wa Baraza na UN

Mkurugenzi Mkuu huyo wa IAEA ameomba Baraza la Usalama liunge mkono juhudi za IAEA za kuhakikisha usalama wa mtambo huo unazingatiwa, ombi ambalo kwa kiasi kikubwa limeungwa mkono na wajumbe waliozungumza katika kikao hicho wakiwemo wale wa Uingereza, Albania, Norway, Marekani na Ufaransa.

Bi. Dicarlo amekumbusha kuwa mashambulizi dhidi ya mitambo ya nyuklia ni kinyume na sheria za kibinadamu za kimataifa na zaidi ya yote Ibara ya 56 ya Itifaki ya Nyongeza ya Mkataba wa Geneva, inasema kuwa “kazi au mitambo yenye vitu vyenye nguvu kubwa kama vile mabwawa, vituo vya mitambo ya nyuklia haipswa kushambuliwa hata kama maeneo hayo yanatumika kijeshi au mashambulizi ya aina hiyo yanaweza kusababisha madhara makubwa miongoni mwa raia.”

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amekaribisha taarifa nah atua za IAEA na yuko tayari kusaidia kwa kadri anavyoweza.