Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naibu Katibu Mkuu wa UN akiwa Kigali, Rwanda aeleza vipaumbele vitano kufanikisha SDGs

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia Mkutano wa 8 wa Kanda ya Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu, uliofanyika Kigali, Rwanda. (03 Machi 2022)
© UNECA/Daniel Getachaw
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia Mkutano wa 8 wa Kanda ya Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu, uliofanyika Kigali, Rwanda. (03 Machi 2022)

Naibu Katibu Mkuu wa UN akiwa Kigali, Rwanda aeleza vipaumbele vitano kufanikisha SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kukomesha awamu kali ya janga la COVID-19 na kujenga mnepo dhidi ya mlipuko ujao wa ugonjwa, bado kunasalia kuwa juu miongoni mwa vipaumbele vya kupatikana kwa maendeleo endelevu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amewaambia washiriki katika Kongamano la Kanda ya Afrika la Maendeleo Endelevu leo mjini Kigali, Rwanda. 

"Janga la coronavirus">COVID-19 limeleta maafa kwa jamii na uchumi wetu," amesema, akibainisha, "kuchanja asilimia 70 ya ulimwengu ifikapo Julai mwaka huu bado ni lengo letu kuu." 

 

 Kuhusiana na hili, Bi. Mohammed amesisitiza haja ya "kujenga mifumo ya afya yenye nguvu na imara zaidi kwa kuwekeza katika mifumo ya huduma za afya ya msingi na ufuatiliaji wa afya, pamoja na uzalishaji mkubwa wa chanjo, uchunguzi na matibabu." 

 

Pili kwenye orodha yake ya vipaumbele ilikuwa hitaji la kuongeza na kuharakisha uwekezaji katika ulinzi wa watu na mifumo ya ikolojia katika mstari wa mbele wa janga la tabianchi. "Ripoti ya IPCC kuhusu kukabiliana na hali hiyo iliyotolewa siku chache zilizopita ni hati ya mashtaka ya kushindwa kwa uongozi tabianchi." Amesema. 

 

Naibu Katibu Mkuu amezitaka nchi zilizoendelea kutekeleza kwa haraka ahadi walizotoa katika COP26 huko Glasgow kuweka maradufu fedha hadi angalau dola bilioni 40 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025, na kwa benki za maendeleo za kikanda na kimataifa kuongeza nguvu zao mbadala na ufadhili binafsi.  

  

Tatu kati ya vipaumbele vyake vilivyoangaziwa, ni hitaji la "kusimamia mabadiliko katika nishati, mifumo ya chakula na upatikanaji wa kidijitali", akibainisha kuwa mabadiliko katika nishati kunaweza kuruhusu Afrika kupata nishati safi na nafuu huku ikilinda ustawi wa watu. 

 

Miongoni mwa athari zinazodhoofisha zaidi za ugonjwa wa COVID-19 ni hasara kubwa ya kujifunza waliyokabiliana nayo watoto kote ulimwenguni. 

  

"Hususani katika nchi zinazoendelea, janga hili linaweka hatari ya  kusababisha janga kwa kizazi kizima." Bi. Mohammed ameonya. 

 

Elimu 

 

Kurekebisha hasara kubwa ya ujifunzaji kutokana na janga hili kwa kuendeleza elimu na mafunzo ya kudumu ni miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika hotuba ya Naibu Katibu Mkuu. Ameangazia Mkutano wa Kilele wa Kuboresha Elimu, utakaoitishwa na Katibu Mkuu mwezi wa Septemba mwaka huu kama fursa ya kutumia juhudi kufikia lengo hilo. 

 

"Mkutano huo utajaribu kuhuisha dhamira yetu ya pamoja ya elimu kama manufaa ya umma na kuhamasisha hatua, matarajio, ufumbuzi na mshikamano unaohitajika ili kuboresha elimu." Amedokeza. 

  

Usawa wa kijinsia  

  

Bi. Mohammed pia amesisitiza haja ya kuharakisha usawa wa kijinsia na mabadiliko ya kiuchumi ambayo, amebainisha, yanahitaji hatua kabambe kutoka kwa wote. Amesisitiza haja ya kutekeleza mapendekezo matano ya Katibu Mkuu ambayo ni pamoja na kufuta sheria zote za ubaguzi wa kijinsia; kukuza usawa wa kijinsia katika nyanja zote na katika ngazi zote za maamuzi; kuwezesha ushirikishwaji wa kiuchumi wa wanawake; kuhakikisha kuingizwa zaidi kwa sauti za wanawake wa umri mdogo; na kufuata mpango wa dharura wa kuzuia na kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. 

 

Jukwaa  hili la Kigali limeitishwa na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi ya Afrika, ECA likiwa na  mada: ‘Afrika yenye kijani kibichi, jumuishi na yenye mnepoi iliyo tayari kufikia Ajenda 2030 na Ajenda 2063'. Mkutano huu unalenga kutathmini maendeleo ya kufikia Malengo ya Maendeleo, na kutoa jukwaa la kubadilishana ujuzi na masuluhisho ya sera ili kusaidia utekelezaji wa Ajenda ya 2030, kulingana na vipaumbele vya kikanda na maalum. 

  

Katika hotuba yake kwenye kongamano hilo, Bi. Mohammed ameangazia umuhimu wa Ajenda 2030 na Ajenda 2063 za Muungano wa Afrika pamoja na ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ‘Ajenda Yetu ya Pamoja’ kama mwongozo kwa ulimwengu kukabiliana kwa mafanikio na changamoto zinawazokabili binadamu leo. 

TAGS: , SDGs, ECA, Covid-19