Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urithi asilia na tamaduni tofauti Afrika ni chachu ya utimizaji wa SDGs: UN

Mwanamke akitengeneza barakoa za kuuza wakati huu wa janga la COVID-19 akiwa Johannesburg Afrika Kusini.
IMF Photo/James Oatway
Mwanamke akitengeneza barakoa za kuuza wakati huu wa janga la COVID-19 akiwa Johannesburg Afrika Kusini.

Urithi asilia na tamaduni tofauti Afrika ni chachu ya utimizaji wa SDGs: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Utajiri wa utamaduni tofauti na maliasili barani Afrika ni muhimu sana katika maendeleo endelevu SDGs, kupunguza umasikini na kujenga na kudumisha amani amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Kupitia ujumbe wake uliotolewa leo katika kuadhimisha siku ya Afrika Antonio Guterres amesema “utajiri huo unaweza kuweka msingi imara kwa ajili ya maendeleo ya uchumi jumuishi wakati bara hilo kubwa liking’ang’ana kukabiliana na changamoto zilizoletwa na changa la corona au COVID-19.” 

Maadhimisho ya siku ya Afrika mwaka huu yamejikita katika kutanabaisha Sanaa, utamaduni na urithi asilia kama chachu ya kujenga Afrika tunayoitaka amesema Katibu Mkuu na kuongeza kuwa lakini janga la COVID-19 limeifanya dunia nzima kuyumba hasa kiuchumi na hivyo kuanika hatari na pengo kubwa lililopo la usawa. 

“Janga hilo linahatarisha hatua za maendeleo zilizopigwa barani Afrika na zaidi na kuchochea migogoro kutokana na ongezeko la pengo la usawa, na hivyo kudhihirisha hali tete ya serikali nyingi duniani hususan katika kufikisha kwa watu wake huduma za msingi kama za afya, elimu. nishati ya umeme, maji na usafi.” 

Amesema athari za janga la COVID-19 zimezidishwa pia na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa akiasi kikubwa yanaathiri nchi zinazoendelea nyingi zikiwemo barani Afrika.  

Bwana Guterres ameiambia dunia kwamba ili kumaliza janga la COVID19, kusaidia kujikwamua kiuchumi na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ”Tunahitaji kuhakikisha fursa na usawa kwa kila mtu katika upatikanaji wa chanjo za COVID-19. Hivi sasa hakuna uwiano katika usambazaji wa chanjo miongoni mwa nchi na takwimu mpya zikionyesha kwamba hadi kufikia leo nchi za Afrika zimepokea asilimia mbili tu ya chanjo hizo.” 

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema “Katika siku hii ya Afrika narejea wito watu kwa nchi Tajiri kushikamana na Afrika katika suala hili.” 

Siku ya Afrika huadhimishwa kila mwaka Mei 25.