Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Imani ya watu kwa redio yazidi kuongezeka licha ya kuwepo kwa mitandao ya kijamii

Angures Buba (kulia) na mwenzake wakisikiliza matangazo ya shule kwa njia ya redio huko Sudan Kusini.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Angures Buba (kulia) na mwenzake wakisikiliza matangazo ya shule kwa njia ya redio huko Sudan Kusini.

Imani ya watu kwa redio yazidi kuongezeka licha ya kuwepo kwa mitandao ya kijamii

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya kimataifa ya redio duniani maudhui makuu yakiwa ni Imani kwa Radio. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2013 kufuatia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2012.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO linasema maudhui ya mwaka huu yanazingatia kuwa kwa historia yake ya zaidi ya karne moja, redio imeendelea kuwa moja ya vyombo vya habari vinavyotumika na kuaminika zaidi.

“Miaka nenda miaka rudi, redio imekuwa ikitoa taarifa zinazowafikia watu kwa wakati huo huo na utafutaji na usambazaji wa habari zenye maslahi kwa umma unaozingatia ueledi, na wakati huo huo kupatia watu burudani na mafunzo,” imesema UNESCO.

Hata wakati wa sasa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, redio imeweza kuziba pengo hilo la kidijitali la kati ya mbinu za kitamaduni za kusikiliza redio na mbinu za kisasa kwa kuja na mifumo mbalimbali ya kuhakikisha taarifa zake zinasikikika kupitia majukwaa mbalimbali kama vile podikasti na kwenye wavuti na hata simu za viganjani.

Habari za UN-Redio inakufa?

Kilichofanya redio kuaminika zaidi

UNESCO inasema matukio ya hivi karibuni na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 yamemomonyoa imani kwa vyombo vya habari na kuchochea kusambaa kwa haraka kwa taarifa za uongo na potofu katika vyombo vya habari.

“Hata hivyo ingawa tafiti zinaonesha kuporomoka kwa imani ya umma katika mitandao ya kijamii na intaneti, bado kuona ongezeko kubwa la imani ya umma kwenye habari. Na raia wengin bado wana imani kubwa na redio kuliko vyombo vingine vya habari,” imesema UNESCO kupitia wavuti wake.

“Sote tunageukia redio, kuliko chombo chochote kile pindi tunapohitaji kupata taarifa.” Audrey Azoulay Mkurugenzi Mkuu UNESCO

Pengo la kidijitali bado linasalia kubwa baina ya jamii na maeneo lakini redio imesalia kuwa kiungo nafuu zaidi ambacho kinaweza kusikilizwa kokote hata ambako hakuna umeme wa uhakika au kiunganisho cha intaneti.

Redio imeendelea kuwa jumuishi na uwepo wa redio za kijamii umeziba pengo la kupata taarifa kwa baadhi ya jamii zilizo pembezoni ambazo sasa zinahizi kuwa zinawakilishwa vyema na vyombo vya habari vya eneo lao.

Mjadala ukiendelea redioni kuhusu ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini.
UNMISS Video
Mjadala ukiendelea redioni kuhusu ukatili wa kijinsia nchini Sudan Kusini.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesisitiza kuwa “sote tunageukia redio, kuliko chombo chochote kile pindi tunapohitaji kupata taarifa.”

Maeneo matatu ya kujikita mwaka huu

Ni kwa mantiki hiyo katika siku hii ya redio duniani, UNESCO inatoa wito kwa vituo vya redio duniani kusherehekea siku hii kwa kuzingatia maeneo makuu matatu ambayo ni  mosi, Imani kwa uandishi wa habari wa redio kwa kuandaa vipindi huru na vya ubora wa juu. Hapa ikimaanisha kuheshimu maadili ya kimsingi ya uandishi wa habari. Redio imekumbwa na changamoto kubwa katika zama za sasa za kasi ya kidijitali lakini ili kuendelea kujenga imani kwa msikilizaji wake, imeendelea kuhakiki na kuthibitisha taarifa zake kabla ya kuzipeleka hewani kwa maslahi ya umma na kujenga jamii endelevu kwa wote.

Kila nchi inategemea vijana wake. Wakati vijana wanatetemeka, ulimwengu unadondoka. - Fatoumata Tamboura, miaka 15,mtoto  mwandishi wa habari. katika redio ya jamii  Kaoural FM  katika mkoa wa kati wa Mopti.
© UNICEF/Seyba Keïta
Kila nchi inategemea vijana wake. Wakati vijana wanatetemeka, ulimwengu unadondoka. - Fatoumata Tamboura, miaka 15,mtoto mwandishi wa habari. katika redio ya jamii Kaoural FM katika mkoa wa kati wa Mopti.

Pili Imani na uwezo wa redio kufikia wengi kwa kujali hadhira yake. Hii ikimaanisha kuwa redio inaweza  kukidhi matakwa ya wasikilizaji iwe kimakundi au kieneo.Mathalani vipindi kwa watu wenye ulemavu, wakimbizi, wanawake na hata viziwi.

Na tatu ni imani na uhalisia wa redio katika kuhakikisha ushindani kwa kuona ni kwa jinsi gani redio inaweza kuendelea kuwepo pindi kuna janga la kifedha katika matangazo ya biashara. Mada hii inauganisha suala la redio kuendelea kujikimu kiuchumi na uwezo wake wa kuvutia na kuendelea kukidhi mahitaji ya hadhira yake.

Siku ya redio duniani inaadhimishwa tarehe 13 Februari ambayo ni tarehe ambayo Redio ya Umoja wa Mataifa ilianzishwa mwaka 1946.