Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Radio na nafasi yake ya ujenzi wa amani

Mwandishi wa habari akitangaza katika Radio Miraya nchini Sudan Kusini.
UNMISS/Isaac Billy
Mwandishi wa habari akitangaza katika Radio Miraya nchini Sudan Kusini.

Radio na nafasi yake ya ujenzi wa amani

Utamaduni na Elimu

Hii leo ni siku ya redio duniani ambapo Umoja wa Mataifa unamulika nafasi ya chombo hicho kilichobuniwa takribani karne moja iliyopita katika kukuza na kujenga amani  wakati huu ambapo pia ni miaka 75 tangu kuanzishwa kwa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa.

Ujumbe wa mwaka huu ni radio na amani ambapo Mkuu wa mawasiliano ya kimkakati kwenye Idara ya Umoja wa Mataifa ya ulinzi wa amani Francesca Mold  amesema maadhimisho ya sasa yamekuja wakati muafaka zaidi kwani Umoja wa Mataifa umeanza kampeni yam waka mmoja kuelekea kilele miaka 75 tangu kuanza kwa operesheni za ulinzi wa amani. 

Amesema operesheni za ulinzi wa amani zinategemea mitandao ya redio ambayo ni muhimu sana katika kufikia jamii mbalimbali hasa kwenye maeneo ambako hakuna mtandao wa intaneti na watu wako kwenye mbio mbio kila wakati kutokana na mapigano. 

Ametoa shukrani kwa wafanyakazi wa redio zilizo chini ya operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa kama vile Radio Okapi iliyoko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Redio Guira huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Halikadhalika redio huru ambazo amesema zinatumia vipindi kama vile mijadala jumuishi kujibu hoja za wenyeji kwa kusambaza taarifa sahihi na kuhakikisha taarifa potofu na zisizo sahihi hazipati nafasi. 

Ametoa shukrani pia kwa msikilizaji akisema kuwa kupitia ushiriki wa msikilizaji, “tunakuwa thabiti zaidi na tunaungana ili kuleta amani.” 

Siku ya Redio duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 mwezi Februari kukumbuka kuanzishwa kwa Redio ya Umoja wa Mataifa mwaka 1946.