Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Redio Ngoma ya Amani ina mchango mkubwa katika kutunza amani DRC - Wasikilizaji

Doris Milongo (kulia) akiwa na Hussein Jaffar wakati wa matangazo katika studio za Redio Ngoma ya Amani ya mjini Fizi jimboni Kivu Kusini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UN News/Byobe Malenga
Doris Milongo (kulia) akiwa na Hussein Jaffar wakati wa matangazo katika studio za Redio Ngoma ya Amani ya mjini Fizi jimboni Kivu Kusini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Redio Ngoma ya Amani ina mchango mkubwa katika kutunza amani DRC - Wasikilizaji

Utamaduni na Elimu

Katika Siku ya Redio Duniani mwaka huu wa 2023, shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linaangazia redio huru kama nguzo ya kujenga amani na kuzuia migogoro.  

Redio inatazamwa kama chombo muhimu na sehemu muhimu ya kutunza amani. Redio hushughulikia visababishi na vichochezi vya migogoro, kabla hazijaweza kulipuka na kuwa vurugu. Inatoa mbinu mbadala ya kuzuia migogoro, au migongano ya maslahi, kuondoa kutoelewana, na kutambua masuala ya kutoaminiana. Hii inaweza kusaidia kukabiliana na chuki, hamu ya kulipiza kisasi, au nia ya kutumia silaha.  

Wakati hii leo dunia ikiadhimisha siku ya radio duniani chini ya kaulimbiu ya Radio na Amani  

Mwandishi wetu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Byobe Malenga anaangazia Redio Ngoma ya Amani, kituo cha redio cha mjini Fizi jimboni Kivu Kusini kinachohamasisha amani hususani katika maeneo ya mashariki mwa DRC na hii ni taarifa yake.   

 “Ni muda wa taarifa ya habari kwenye radio ngoma ya amani. Ni kawaida kuona watu wakisikiliza redio unapopita katika mitaa ya maeneo mbalimbali mashariki mwa DRC.” Ndivyo anavyoanza kueleza Byobe Malenga.  

Uongozi wa redio hii unasema kwamba unafarijika kuona kwamba elimu yao kwa vijana kutojiunga na makundi ya waasi na migogoro ya kikabila inatiliwa maanani kama anavyoeleza Naibu Mkurugenzi wa redio hiyo Hussein Fils Jafari, "kwanza nataka niseme kwamba  redio Ngoma Ya Amani  ni redio ya kijamii  ambayo iliundwa kwa misingi ya kuunganisha watu baada ya kuona kwamba eneo letu la Fizi na mashariki mwa Congo lilikumbwa sana na ukabila,vita na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya mwanamke na wakati huu wa redio tumefarijika sana  kuona kwamba tumekuwa tukiunganisha watu, tumekuwa tukipata ujumbe wa kusema kwamba watu wanafurahia vipindi vyetu na hiyo ni faraja kubwa sana kuona kwamba watu wameanza kuwa pamoja na kusema neno moja." 

Watangazaji wa vipindi vya Redio Ngoma ya Amani ya mjini Fizi, jimboni Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UN News/Byobe Malenga
Watangazaji wa vipindi vya Redio Ngoma ya Amani ya mjini Fizi, jimboni Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Anayoyasema Naibu Mkurugenzi wa redio ngoma ya amani yanathibitishwa na wasikilizaji. Hamis Mayuto Francois anasema, "tunashukuru sana maana tangu redio Ngoma Ya Amani ilipoletwa hapa kwenye eneo letu tunaifata 5/5, ni redio nzuri sababu wakati tunapopata tatizo la amani sisi kama viongozi  wa shirika la kiraia , tunapita kwenye redio Ngoma ya Amani na kila tukitangaza kuomba amani wananchi wetu wanabaki ndani ya amani mizozo inaisha, kwakweli ni redio nzuri sana maana inatusaidia sana kwa kuleta amani, kiukweli walichaguwa jina zuri sana maana tumepata amani kupitia redio Ngoma Ya Amani." 

Naye Boaz Msembwa anaeleza ule akisema, "naitwa boaz msembwa ni mkaazi wa baraka kata la makampagne ndipo nilipo mimi kwa niaba yangu kulingana na manufaa ya redio Ngoma ya amani ni radio ambayo inatufanya sisi wakaazi wa jiji la Baraka kufahamu mengi kupitia mafunzo kutoka kwa watangazaji wake." 

Claudine Jerome mkazi wa eneo la Fizi ambaye ni mwanaharakati za haki za wanawake anasema redio hii ya ngoma ya amani inaenda mbali zaidi ya kuhamasisha amani dhidi ya vita za kikabila na uasi. Claudine anasema, "naweza kusema kwa upande wangu mimi kama radio ngoma ya amani ilitusaidia sana kwa kutuletea na kututangazia hivyo vipindi vyake maana ubakaji na unyanyasaji wa wanawake ulikuwa mwingi sana hapo awali katika jamii maana kabla, watu  hawakuwa wanamchukulia au kumpa thamani mwanamke. Mwanamke alikuwa  hawezi kufanya baadhi ya vitu kati ya wanaume lakini siku hizi tunashukuru mungu kupitia Radio Ngoma ya amani vitendo vya unyanyasaji kwa mwanamke vimepungua." 

Redio Ngoma Ya Amani Fizi ianzishwa tarehe 30 mwezi Oktoba mwaka 2009 kutokana na vurugu za vita ya mwaka 1996-2000 mashariki mwa DRC na kwa sasa kituo hicho cha Redio kina matawi matatu katika eneo la mashariki mwa DRC kwa lengo la kuhamasisha watu kuishi kwa amani na umoja. 

 

TAARIFA HII IMEANDALIWA NA BYOBE MALENGA WA IDHAA YA KISWAHILI YA UMOJA WA MATAIFA DRC