Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulimwengu lazima 'ubadilishe mkondo' ili kulinda bahari dhidi ya janga la tabianchi - Guterres  

Bahari huendesha mifumo ya kimataifa ambayo hufanya dunia iweze kuwa mahali pa kuishi wanadamu.
WMO/Awangku Nazrulddin
Bahari huendesha mifumo ya kimataifa ambayo hufanya dunia iweze kuwa mahali pa kuishi wanadamu.

Ulimwengu lazima 'ubadilishe mkondo' ili kulinda bahari dhidi ya janga la tabianchi - Guterres  

Tabianchi na mazingira

Sayari dunia inakabiliwa na matatizo mara tatu ya uharibifu wa tabianchi, upotevu wa baionuai na uchafuzi wa mazingira, Katibu Mkuu António Guterres ameuambia Mkutano wa Bahari Moja #OneOceanSummit hii leo akionya kwamba, "bahari inabeba mzigo mkubwa". 

Bahari inapotumika kama shimo kubwa la ukaa au kaboni na joto, inakua na joto na asidi zaidi, na kusababisha mifumo yake ya ikolojia kuteseka. 

"Barafu ya kusini na kaskazini mwa dunia inayeyuka, na hali ya hewa duniani inabadilika." Katibu Mkuu Guterres amesema kupitia katika ujumbe wake wa njia ya video kwa mkutano unaofanyika wiki katika mji wa pwani ya kaskazini mwa Ufaransa, Brest.  

Athari  

Jamii zinazotegemea bahari zinaumia pia, ameongeza Guterres, “zaidi ya watu bilioni tatu wanategemea viumbe hai vya baharini na pwani kwa ajili ya maisha yao". 

Katibu Mkuu Guterres ameeleza hali mbaya ya viumbe vya baharini vinavyopungua; miamba ya matumbawe inayokufa; Mifumo ya ikolojia ya pwani ambayo imegeuka kuwa "maeneo makubwa yaliyokufa" huku yanatumika kama sehemu ya kutupa maji taka; na virutubishi na bahari iliyosongwa na taka za plastiki. 

Aidha, hifadhi ya samaki inatishiwa na vitendo vya uvuvi vilivyokithiri na haribifu, pamoja na uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa. 

"Lazima tubadilishe mwelekeo." Amesisitiza Katibu Mkuu Guterres. 

Hali ya joto humaanisha kuyeyuka kwa barafu ya bahari, kuongezeka kwa halijoto ya bahari, na maji yenye joto - kuathiri mifumo ikolojia na mifumo ya hali ya hewa duniani.
WMO/Hwang Seonyoung
Hali ya joto humaanisha kuyeyuka kwa barafu ya bahari, kuongezeka kwa halijoto ya bahari, na maji yenye joto - kuathiri mifumo ikolojia na mifumo ya hali ya hewa duniani.

Kuzingatia sheria 

Ni miaka 40 tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari. "Umuhimu wa uhakika wa kisheria katika bahari ni muhimu." Amekumbushia Bw. Guterres. 

Amesisitiza kwamba Mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa wa Bahari, ambao utafanyika Lisbon kuanzia Juni 27 hadi Julai 1 mwaka huu, ni "fursa ya kuimarisha jukumu la bahari" katika juhudi za kimataifa za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kutekeleza Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

Uchumi unaotokana na bahari 

Kiongozi huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa juhudi kubwa lazima zifanywe kulinda bahari, akisema kuwa "uchumi endelevu unaotokana na bahari unaweza kuleta maendeleo ya kiuchumi na kutengeneza nafasi za kazi", huku ukilinda tabianchi. 

Bwana Guterres amekaribisha "hatua za kutia moyo" zilizochukuliwa na baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kukomesha matumizi ya plastiki moja na akawataka wengine kuiga mfano huo.