Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asanteni kwa kutambua dharura ya tabianchi ni vita vya maisha kwa ajili ya mutakabalki wetu-Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
UN Photo/Cia Pak
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Asanteni kwa kutambua dharura ya tabianchi ni vita vya maisha kwa ajili ya mutakabalki wetu-Guterres

Tabianchi na mazingira

Baada ya mjadala wa siku nzima wa mkutano maalum kwa ajili ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amewashukuru vijana kote duniani kwa kuongoza mapambano na kukibebesha wajibu kizazi cha sasa.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo wa ngazi ya juu mjini New York Marekani jioni hii Guterres amesema “tumekuwa tukidemadema katika mbio hizi dhidi ya mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi. Lakini sasa dunia inaamka , shinikizo linaongezeka, kasi inaongezeka na hatua kwa hatua mwelekeo unabadilika. Leo hii katika ukumbi huu dunia imeshuhudia hamasa na mipango thabiti.”

Katibu mkuu  ameitaja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na “nchi 77 nyingi zikiwa zilizoendelea kiviwanda duniani zimeahidi kutozalisha kabisa hewa chafuzi ya ukaa ifikapo 2050, pia zikiungwa mkono na kanda 10 na miji Zaidi ya 100 ikiwemo mingi kutoka sehemu kubwa ya dunia. Pia nchi 70 zimetangaza zitapiga jeki mchango wake wa kitaifa ifikapo 2020”

Guterres ameongeza kuwa viongozi zaidi ya 100 kutoka sekta binafsi wameahidi kuchapuza mchakato wa kuhamia kwenye uchumi wa kijani unaojali mazingira.

Na kundi kubwa la wamiliki wa mali duniani ambao wamechangia Zaidi ya dola trilioni 2 wameahidi kuhamia kwenye uwezezaji uusiozalisha hewa ukaa ifikapo 2050 na benki za ushirika na maendeleo zimeongeza ahadi zao.

Nayo klabu ya ufadhili wa maendeleo ya kimataifa imetangaza itakusanya dola trilioni 1 za ufadhili wa nishati salama ifikapo mwaka 2025 katika nchi 20 zenye maendeleo duni.

Pia amesema benki 130 ambazo ni theluthi moja ya selkta ya kimataifa ya Benki zimetia saini kwenye sanjari na malengo ya mkataba wa Paris na malengo ya maendeleo endelevu SDGs katika bishara zao.

Tweet URL

Amesema na wengine leo wamekwenda mbali zaidi na kuongeza mara mbili ahadi za ufadhili wa jumla wa mabadiliko ya tabianchi. “Ni muhimu tuhakikishe utekelezaji wa ahadi za nchi zilizoendelea wa kukusanya dola bilioni 100 kwa mwaka kutoka kwa sekta binafsi na sekta za umma ifikapo mwaka 2020 na hasa katika kuzuia na kukabiliana na mabadiliko hayo katika nchi zinazoendelea.”

Pia mkutano wa leo umeshuhudia mikakati mipya ya kutumia uwezo wa mali asili ikiwa ni pamoja na kuhifadhi asilimia 30 ya ardhi ya dunia na maji ifikapo mwaka 2030, pia kulinda misitu ya Afrika ya Kati na watu milioni 60 wanaoitegemea. Pia suluhu zaidi ya 150 za asili za kupunguza utoaji wa hewa ukaa zimetangazwa.

Zaidi ya miji 2000 imeahidi kuweka hatari za mabadiliko ya tabianchi katika kitovu cha maamuzi yao  kwa kuanzisha miradi 1000 inayojali mazingira mijini.

“Nchi nyingi kote duniani kuanzia Pakistan hadi Guatemala, Colombia mpaka Nigeria, New Zealand mpaka Barbados zimeweka ahadi kubwa leo ya kupanda miti zaidi ya bilioni 11.”

Amesema mmefanya mengi , kuongeza kasi, ushirikiano na hamasa lakini bado safari ni ndefu na hatujafika bado kazi kubwa inahitajika ili kufikia lengo la kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo 2050 na kuhakikisha kiwango cha joto kinasalia katika nyuzi hoto 1.5 ifikapo mwisho wa karne hii.

Na katika kusonga mbele Katibu Mkuu amesema “ninaumba mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa kuzisaidia zaidi nchi , biashara na mashirika kujiunga na mikakati ya aleo na kuongeza hatua na hamasa. Kwani tuko pamoja katika suala hili .