Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaonesha tofauti ya nchi tajiri na maskini: Dkt. Jakaya Kikwete

Mwenyekiti wa Bodi ya Ubia wa Elimu Duniani, GEP, pia ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete katika mahojiano maalum na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Assumpta Massoi
Mwenyekiti wa Bodi ya Ubia wa Elimu Duniani, GEP, pia ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete katika mahojiano maalum na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

COVID-19 yaonesha tofauti ya nchi tajiri na maskini: Dkt. Jakaya Kikwete

Utamaduni na Elimu

Janga la COVID-19 limethibitisha bayana ukosefu wa usawa uliopo ulimwenguni leo ambapo nchi zilizoendelea shule zilifungwa lakini watoto waliendelea na masomo kwa njia ya mtandao wakati wanafunzi katika nchi zinazoendelea, shule zilifungwa, na watoto hawakujifunza kabisa.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ubia wa Elimu Duniani, GEP Dkt. Jakaya Kikwete katika mahojiano maalum na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani muda mchache baada ya kumaliza mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterees.

Dkt. Kikwete amesema mazungumzo yake na Katibu Mkuu Guterres yamelenga kujadiliana namna taasisi hizo mbili kubwa duniani zinayoweza kuleta mageuzi katika elimu hususan katika nchi za kipato cha chini kwa kuimarisha mifumo ya elimu na matumizi ya teknolojia katika kufundishia.

Tweet URL

“Nchi zilizoendelea kama hapa Marekani wanafunzi wanasoma mtandaoni, lakini suala hili ni gumu kwa nchi masikini kwakuwa ili kujifunza mtandaoni lazima uwe na mtandao, na hakuna intaneti shuleni, hakuna mtandao nyumbani, au lazima uwe na kompyuta, simu simu mahiri vitu hivi watoto hawana kwahiyo walijikuta wakikaa tuu nyumbani”. Anasema Bwana Kikwete.

Fedha za ufadhili

Hata hivyo ameeleza kuwa wamesaidia nchi kukabiliana na athari za COVID-19 katika sekta ya elimu , elimu imeleta athari kubwa na wametoa msaada wa fedha kupunguza machungu ya COVID-19. “Sisi kutoka GPE tumechangia dola nusu bilioni, dola milioni 500 kwa nchi 66 ili watoto wajifunze, kwa sababu baada ya mlipuko wa COVID watoto bilioni 1.6 walikuwa nje ya shule. Lakini kabla ya COVID tayari tulikuwa tunahangaika, kwa hivyo wasiwasi wetu ni jinsi tunavyowaweka watoto kujifunza katika nchi hizi 66.”

Dkt Kikwete ameeleza kuwa kwa zaidi ya miaka 20 GEP imesaidia kuboresha mifumo ya elimu kwa shule za msingi na sekondari na mafanikio yanazidi kuonekana. “ Katika miongo miwili watoto zaidi milioni 160 wameweza kupata elimu na nia yetu ni kufanya zaidi. Tunachangisha fedha kupitia wafadhili na tunatumia pesa hizo sasa kusaidia nchi kubadilisha mifumo yao ya elimu. Nchi zenyewe zinabainisha maeneo mahususi ambayo wana maslahi nayo na wangependa kufanyike mageuzi ambayo na sisi GEP tunachofanya ni kuwasaidia katika eneo hilo.”

Soundcloud

 

Katika mazungumzo hayo ameeleza kuwa Bodi ya Ubia wa Elimu Duniani, GEP kupitia mkutano wa wakuu wa nchini uliofanyika jiji London uingereza walitoa ombi la dola bilioni 5 na wameweza kukusanya bilioni 4, kwa hiyo wanapungukiwa na bilioni 1 kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2025.”Ikiwa mwaka wa kwanza tumeweza kukusanya bilioni 4, tunadhani tutaweza kabisa kupata iliyobaki miaka minne kuongeza kiasi hicho. Nia yetu tukipata fedha hizi, sasa tunadhani watoto milioni 175 watapata elimu.”

Akitolea mifano ya namna fedha wanazokusanya zinavyofanya kazi katika nchi mbalimbali duniani Dkt Kikwete amesema, “kuna maeneo ambayo tumekuwa tukifanya kazi na wasichana na sasa matokeo ni kuwa idadi umeongezeka mara mbili zaidi ya wasichana wako shuleni kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita. Tuna watoto milioni 160 zaidi shuleni kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita na ikiwa tutapata ufadhili wa dola bilioni 5, tutakuwa na watoto milioni 175 zaidi.”

Mabadiliko ya uongozi katika nchi

Kuhusu nchi kuwa na mabadiliko ya uongozi na viongozi na iwapo mabadiliko hayo yanaweza kuleta athari katika kuboresha mifumo ya elimu Mwenyekiti huyo wa GEP amesema kuwa “Uongozi unapobadilka kila watu wana mitazamo yao kuna wengine wana mtazao chanya kwenye elimu na wengine mtazamo hasi, lakini tulichojifunza kwa ujumla wake ni kwamba hakuna nchi ambayo imepuuza elimu duniani. Lakini tumepata matatizo hivi karibuni nchini Afghanistan, walipoingia watawala wapya hawa ( Taliban) wamesema wasichana elimu wanayoweza kupata ni elimu ya msingi tu, kwahiyo tupo tunaangalia namna ya kuweza kubadili hili na pengine kuona tunawezaje kutumia teknolojia kuwasaidia wasichana wa Afghanistan.”

GPE imejidhatiti kuhakikisha kuwa watoto walio katika mazingira magumu wanapata elimu bora katika nchi zenye kipato cha chini duniani.