Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fursa ya kukwamua elimu baada ya athari za COVID-19 inapungua - Kikwete

Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa mkutano na wanahabari mjini New  York, Marekani kwenye uzinduzi wa ripoti mpya ya Baraza la wakimbizi duniani, WRC kuhusu masuala ya wakimbizi. (Maktaba)
UN /Mark Garten
Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa mkutano na wanahabari mjini New York, Marekani kwenye uzinduzi wa ripoti mpya ya Baraza la wakimbizi duniani, WRC kuhusu masuala ya wakimbizi. (Maktaba)

Fursa ya kukwamua elimu baada ya athari za COVID-19 inapungua - Kikwete

Utamaduni na Elimu

“Janga hili likiwa linaingia mwaka wake wa tatu hivi karibuni, ujasiri mkubwa wa watoto ulimwenguni kote ambao wanajitahidi kuendelea kujifunza unastahili kutambuliwa.” Hivyo ndivyo alivyoanza tamko lake Mwenyekiti wa Bodi ya GEP ambayo ni 'Ubia wa Kimataifa kwa ajili ya Elimu'. 

Tamko hilo ambalo amelitoa leo Jumatatu jijini New York ambako amekutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed huku akitarajiwa pia kesho Jumanne kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Bwana Kikwete ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Tanzania akiwazungumzia wanafunzi amesema, “tunapaswa kuwapongeza wale wanaowaunga mkono; wazazi wao, walimu na wasimamizi ambao wanafanya kazi kwa bidii ili kuzifanya shule kuendelea kuwa wazi, kukabiliana na masomo nje ya shule au kuanzisha upya madarasa baada ya kufungwa kwa miezi mingi.” 

Ujumbe huu wa Kikwete umekuja wakati dunia ikiwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Elimu ambayo huadhimishwa kila tarehe 24 Januari ya mwaka. 

"Katika siku hii ya kimataifa ya elimu, jumuiya ya kimataifa lazima ifanye zaidi, kabla ya COVID-19 kutengeneza pengo la kudumu katika pengo ambalo tayari halina kisingizio la kiasi wanachojifunza watoto matajiri na maskini." Amesema Bwana Kikwete. 

Bwana Kikwete anaendelea akisema hata kabla ya COVID-19 kuupindua ulimwengu juu chini, karibu robo ya watoto bilioni walikuwa wameacha shule, kwa sababu familia zao hazikuwa na uwezo wa kumudu, au shule zilikuwa mbali sana au hazifai, hasa kwa watoto wenye ulemavu. COVID-19 imeweka kizuizi kipya na cha kutisha kuwaingiza watoto hawa shuleni. Zaidi ya wanafunzi bilioni 1.6 walifungiwa shule mwaka wa 2020 pekee na inakadiriwa kuwa watoto milioni 24 huenda wasiweze kuona tena ndani ya darasa. Wasichana wapatao milioni 13 wanaweza kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo, elimu yao ilikatizwa huku familia zao zikihangaika kumudu gharama za kiuchumi za janga hili. 

Kuhusu Omicron 

Kuhusu mnyumbuliko wa virusi Covid-19 ambao umefanya kutokea Omicron, Bwana Kikwete anasema kutokana na mnyumbuliko huu mpya, fursa ya kusaidia familia kuwabakiza shuleni au kuwaelimisha watoto wao inapungua kwa kasi ya kutisha. Mbali na ndoa za utotoni, watoto katika baadhi ya nchi za kipato cha chini wanalazimishwa kuingia kwenye kazi au kuajiriwa kama wapiganaji huku wengine wakinaswa katika kaya zenye dhuluma au unyanyasaji bila matumaini ya kupata nafuu. “Ni lazima tuzuie matokeo haya mabaya ni vigumu zaidi kuyarejesha nyuma pindi yanapoanza.” Amesema 

Bajeti za elimu zinapungua 

Wahusika wa elimu wanapaswa kutumia wakati huu kuongeza juhudi zote na kubadilisha mifumo yetu ya elimu ili hata watoto waliotengwa au waliotengwa zaidi katika jamii zetu waweze kujifunza, anasema Bwana Kikwete akiongeza, “lakini badala yake, bajeti za elimu zinapungua, na hivyo kuweka hatarini mafanikio yaliyopatikana kwa bidii, hasa katika uandikishwaji wa wasichana. Theluthi mbili ya nchi za kipato cha chini na cha kati zilipunguza bajeti zao za elimu tangu kuanza kwa janga hilo. Ili kuzipa nchi washirika njia mbadala za kupunguza matumizi ya elimu, GPE ilitoa ufadhili wa dola nusu bilioni haraka.” 

GPE inahitaji usaidizi 

Ikiwa tunataka kutoa aina ya ufadhili wa elimu ambao nchi zinahitaji, na kupata watoto milioni 175 katika shule kufikia mwaka 2025, GPE itahitaji usaidizi pia. Julai ya mwaka ulipoita, wafadhili waliahidi dola bilioni 4 kwa GPE katika Mkutano wa Kimataifa wa Elimu, lakini hii inaacha upungufu wa dola bilioni 1 kusaidia kubadilisha elimu katika takriban nchi 90 ambazo zina watoto bilioni 1. “Kushughulikia pengo hili itakuwa ishara wazi ya nia ya kimataifa ya kuchukua hatua.” Ameeleza Jakaya Kikwete akiongeza kuwa, "GPE iliyofadhiliwa kikamilifu ingesaidia kubadilisha elimu kwa kudumu na kuongeza kwa asilimia 30 kiasi ambacho nchi za kipato cha chini zinaweza kutumia katika mageuzi muhimu ya elimu ambayo yanaenda zaidi ya kukidhi gharama zinazoendelea." 

Jakaya Kikwete anahitimisha akitoa wito kwamba, “Tunapaswa kuahidi kwamba kila siku lazima iwe Siku ya Kimataifa ya Elimu; wakati wa kufahamu tishio kwa maisha yetu ya usoni na kuelekeza mawazo na rasilimali zetu kuelekea kubadilisha mifumo ya elimu kwa watoto walio katika mazingira magumu zaidi.” 

GPE ni dhamira ya pamoja ya kumaliza janga la elimu duniani. Ni ushirikiano na mfuko pekee wa kimataifa unaojitolea kikamilifu kusaidia watoto katika nchi za kipato cha chini kupata elimu bora, ili waweze kufungua uwezo wao na kuchangia kujenga ulimwengu bora.