Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakimiliki ya mwili wa mwanamke ipewe uzito mtandaoni kama haki miliki zingine:UNFPA 

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA limezindua kampeni ya hakimiliki ya mwili kwa lengo la kuelimisha juu ya ukatili wa kijinsia mtandaoni hususan dhidi ya wanawake na wasichana na kutaka hatua zichukuliwe kuukomesha
UNFPA
Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA limezindua kampeni ya hakimiliki ya mwili kwa lengo la kuelimisha juu ya ukatili wa kijinsia mtandaoni hususan dhidi ya wanawake na wasichana na kutaka hatua zichukuliwe kuukomesha

Hakimiliki ya mwili wa mwanamke ipewe uzito mtandaoni kama haki miliki zingine:UNFPA 

Wanawake

Kampeni mpya iliyozinduliwa mwezi huu wa Desemba na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani linalohusika pia na afya ya uzazi UNFPA ya “Hakimiliki ya miwli wa binadamu” ina lengo la kuwasukuma watunga sera, sekta za teknolojia na mitandao yote ya kijamii kuuchukulia unyanyasaji na ukatili wa miili ya binadamu hususani ya wanawake mtandaoni kuwa ni suala linalohitaji kupewa uzito kama ilivyo ukiukwaji wa hakimiliki zingine. Flora Nducha na taarifa kamili 

Kupitia video ya UNFPA ya uzinduzi wa kampeni hiyo, mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Natalia Kanem anahoji endapo dunia inafahamu kwamba asilimia 85 ya wanawake walio na fursa ya intaneti wameripoti kushuhudia ukatili mtandaoni na wengine asilimia 38 wakipitia binafsi ukatili huo. 

Amesema wanawake na wasichana, makundi ya walio wachache na watu waliotengwa wana uwezekano mkubwa wa picha zao kutumiwa vibaya mtandaoni, kudhalilishwa na kutumika katika vitendo vya ngono bila ridhaa yao. Hivyo amesisitiza kuwa 

“Ukatili wa mtandaoni unasababisha madhara makubwa, lakini makampuni ya kidijitali na watunga sera wanaonekana kuufumbia macho wakiweka thamani kubwa na ulinzi kwa hatimiliki kuliko wanavyofanya kwa binadamu.” 

Hata hivyo amesema “Ukweli ni kwamba haumiliki mwili wako mtandaoni. Na hii ndio sababu sisi hapa UNFPA, tumezindua haki ya mwili, hakimiliki ya kwanza kwa ajili ya mwili wa binadamu. Kwa kudai haki yetu ya mwili na kuchukua udhibiti wa miili yetu mtandaoni ndio pekee tutakapoweza kukomesha ukatili wa kijinsia unaoshuhudiwa kila siku kote duniani.” 

Bi Kanem ametoa wito kwa kila mtu kuuchukulia ukiukwaji huu wa haki za binadamu kwa uzito mkubwa, na kampeni inawatumia watu mbalimbali wenye ushawishi, mashuhuri, wanaharakati na watumiaji wa mitandao ya kijamii ikiwataka kuongeza herufi (B) kwenye picha zao kuunga mkono ukomeshaji wa ukatili wa kijinsia mtandaoni.