Wanawake na wasichana ndio walio hatarini zaidi kuuawa majumbani: UN Women/UNODC

Mwanamke akishiriki katika maandamano ya kupinga ukatili wa kijinsia huko Quito, Ecuador.
© UN Women/Johis Alarcón
Mwanamke akishiriki katika maandamano ya kupinga ukatili wa kijinsia huko Quito, Ecuador.

Wanawake na wasichana ndio walio hatarini zaidi kuuawa majumbani: UN Women/UNODC

Wanawake

Ripoti ya utafiti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu UNODC inaonyesha kuwa wanawake na wasichana ndio walio katika hatari kubwa ya kuuawa majumbani, ikionyesha kuwa kwa wastani zaidi ya wanawake au wasichana watano waliuawa kila saa na wenzi wao au jamaa wa familia kwa mwaka 2021. 

Ripoti hiyo kuhusu mauaji ya wanawake imetolewa siku chache kabla ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Novemba n ani kumbusho kwamba ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni moja ya ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani. 

Kwa mujibu wa utafiti huo wa UNODC na UN Women miongoni mwa wanawake na wasicna wote waliouawa mwaka jana asilimia 56 waliuawa na wenzi wao ay jamaa wa familia saw ana watu 45,000 kati ya 81,000 huku ripoti ikionyesha kuwa nyumbani sio mahali salama kwa wanawake na wasichana wengi. 

Wakati huohuo asilimia 11 ya mauaji yote ya wanaume yanafanywa kwa faragha. 

Tunawaangusha wanawake na wasichana 

Mkurugenzi mtendaji wa UN Women Sima Bahous amesema “Katika kila takwimu ya mauaji ni hadithi ya mwanamke au msina ambaye tumemuangusha. Vifo hivi vinazuilika nyenzo na ujuzi wa kufanya hivyo tayari vipo. Mashirika ya kupigania haki za wanawake tayari yanafuatilia takwimu na kuchagiza mabadiliko ya sera na uwajibikaji. Sasa tunachohitaji ni hatua katika jamii ambazo zitatimiza haki za wanawake na wasichana ili wahisi na kuwa salama majumbani, mitaani na kila mahali.” 

Naye mkurugenzi mtendanji wa UNODC Ghada Waly amesema “Hakuna mwanamke au msichana anayepaswa kuhofia maisha yake kwa sababu tu ya jinsi alivyo. Kukomesha aina zote za mauji ya kijinsia kwa wanawake na wasichana, tunahitaji kumhesbu kila muathirika kila mahali na kuboresha uelewa wa hatari na vyanzo vya mauaji ili tuweze kuandaa vyema mbinu za kuzuia nah atua za kisheria. UNODC inajivunia kuzindua utafiti huu wa mwaka 2022 kuhusu mauaji na UN Women kwa lengo la kuchagiza hatua za kimataifa na kupongeza juhudi za mashirika ya kupigania haki za wanawake kote duniani kukomesha uhalifu huu.” 

Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia
UN Women Tanzania/Deepika Nath
Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia

Asia inaongoza kwa mauaji mengi 

Kuhusu tofauti za kikanda, ripoti hiyo inasema wakati mauaji ya wanawake ni tatizo ambalo linahusu kila nchi duniani, ripoti inaonyesha kuwa Asia ilirekodi idadi kubwa zaidi ya mauaji yanayohusiana na jinsia katika maeneo ya faragha mwaka 2021. 

Kwa bara la Afrika ripoti imeeleza kuwa wanawake na wasichana wako katika hatari ya kuuawa na wapenzi wao wa karibu au wanafamilia wengine . 

Mwaka 2021, kwa mujibu wa ripoti kiwango cha mauaji yanayohusiana na jinsia katika mazingira ya faragha kilikadiriwa kuwa watu 2.5 kwa kila idadi ya wanawake 100,000 barani Afrika, ikilinganishwa na mtu 1.4 Amerika, mtu 1.2 Oceania, mtu 0.8 Asia na mtu 0.6 barani Ulaya.  

Wakati huo huo, matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba mwanzo wa janga la COVID-19 mwaka 2020 uliambatana na ongezeko kubwa la mauaji yanayohusiana na jinsia katika mazingira ya faragha huko Amerika Kaskazini na kwa kiwango fulani Magharibi na Kusini mwa Ulaya. 

Ukatili wa kijinsia waweza kuzuilika 

Hata hivyo ripoti inasema mauaji yanayohusiana na jinsia, pamoja na aina nyinginezo za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, sio kitu kisichoepukika. “Yanaweza na ni lazima yazuiliwe, kwa mchanganyiko wa hatua ikiwemo utambuzi wa mapema wa wanawake walioathiriwa na unyanyasaji, upatikanaji wa usaidizi na ulinzi unaolengwa kwa waathirika, kuhakikisha kwamba polisi na mifumo ya haki inazingatia zaidi mahitaji ya waathirika, na uzuiaji wa msingi kwa kushughulikia sababu kuu za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana ikiwa ni pamoja na kubadilisha tabia mbaya za mfumo dume, kanuni za kijamii, kuondoa tofauti za kimuundo za kijinsia na itikadi kali za kijinsia.”  

Pia ripoti imesema kwa kuimarisha ukusanyaji wa takwimu kuhusu mauaji ya wanawake ni hatua muhimu ya kufahamisha sera na programu zinazolenga kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. 

Siku 16 za uhamasishaji kupinga ukatili wa kijinsia 

UN Women na UNODC wamesema ripoti ya leo itasaidia kufahamisha kuhusu siku 16 za uhamasishaji kupinga ukatili wa kijinsia mwaka huu, ambayo ni kampeni ya kimataifa inayoanza tarehe 25 Novemba, siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, na itaendelea hadi Desemba 10, siku ya haki za binadamu. 

Kampeni hii ya kila mwaka huibua mamia ya matukio kote ulimwenguni ili kuharakisha juhudi za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. 

Maudhui ya kampeni yam waka huu ni “Ungana katika harakati za kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana” ikitoa wito kwa serikali na wadau wengine kuonyesha mshikamano kwa wanaharakati wa kupigania haki za wanawake na kumualika kila mtu kujiunga na vuguvugu la kimataifa kutokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanaake.