Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1.5 zahitajika kunusuru Somalia mwaka 2022

Mzee huyu ni miongoni mwa wakimbizi wa ndani katika kambi ya Baidoa nchini Somalia
UNDP/Said Fadheye
Mzee huyu ni miongoni mwa wakimbizi wa ndani katika kambi ya Baidoa nchini Somalia

Dola bilioni 1.5 zahitajika kunusuru Somalia mwaka 2022

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu nchini Somalia hii leo wametangaza mpango wa usaidizi wa kibinadamu nchini humo kwa mwaka 2022 mpango ambao unahitaji jumla ya dola bilioni 1.5 kwa ajili ya kusaidia watu milioni 5.5 wanaokabiliwa na hali ngumu ya kibinadamu.

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Mogadishu Somalia na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, inasema ombi hilo la kusaidia Somalia inazingatia ukweli kwamba taifa hilo la pembe ya Afrika haijapata misimu ya mvua kwa miaka mitatu mfululizo ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30. Tayari Umoja wa Mataifa Umechangia dola milioni 17 kutoka mfuko wake wa dharura za kibinadamu, CERF.

Mkuu wa OCHA Martin Griffiths akizungumzia hatua hiyo ya usaidizi kwa Somalia, amesema, “maisha ya wananchi wa Somalia yako mashakani na hatuna muda wa kupoteza. Ili kuepusha janga lingine la kibinadamu, fedha kutoka CERF, zitawezesha watoa misaada ya kibinadamu kuimarisha operesheni zao za dharura. Nategemea wahisani wengine waoneshe mfano katika kuchangia ombi hilo la usaidizi kwa Somalia ili hatimaye wananchi waondokane na njaa na umaskini.”

Bila usaidizi wa haraka wa kibinadamu, watoto, wanawake na wanaume wataanza kufa kwa njaa Somalia- Khadija Diriye, Waziri - Somalia

Wananchi wa Somalia wamegubikwa na miongo ya mizozo, madhara ya mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya mgonjwa ikiwemo janga la Corona au coronavirus">COVID-19 na athari zake. Baa la nzige lililodumu muda mrefu nalo limeathiri mavuno na mbinu za kujipatia kipato na takwimu zinaonesha kuwa watu 7 kati ya 10 nchini Somalia ni hohehahe.

Ukame wa sasa, kwa mujibu wa Waziri wa masuala ya kibinadamu na kudhibiti majanga Somalia, Khadija Diriye, umepoteza mbinu za wananchi kujipatia kipato huku familia zikiwa hatarini kutumbukia kwenye janga. “Bila usaidizi wa haraka wa kibinadamu, watoto, wanawake na wanaume wataanza kufa kwa njaa Somalia,” amesema Bi. Diriye.

Ombi la kusaidia Somalia kwa mwaka 2022 linalenga zaidi kukabiliana na njaa, utapiamlo uliokithiri, kudhiibiti na kukabiliana na milipuko ya magonjwa, kukabili vitendo vya ukatili na vilipuzi.

Mizozo na ukosefu wa usalama nchini Somalia vimelazimu zaidi ya watu 540,000 kukimbia makazi yao mwaka huu pekee wa 2021 huku zaidi ya watu milioni 2.9 wakiwa ni wakimbizi wa ndani wengi wao wakihitaji misaada.