Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame wa kihistoria Somalia umewaacha taabani watu zaidi ya milioni 7: OCHA 

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia Adam Abdelmoula akiandamana na mjumbe mpya wa masuala ya ukame Somalia Abdirahman Abdishakur ziarani Baidoa, Somalia
UN Photo/Fardosa Hussein
Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia Adam Abdelmoula akiandamana na mjumbe mpya wa masuala ya ukame Somalia Abdirahman Abdishakur ziarani Baidoa, Somalia

Ukame wa kihistoria Somalia umewaacha taabani watu zaidi ya milioni 7: OCHA 

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia Adam Abdelmoula akiandamana na mjumbe mpya wa masuala ya ukame Somalia katika ziara yake ya kwanza, Jumanne wiki hii ameonya kuhusu hali mbaya  kwa mamilioni ya Wasomali walioathirika na ukame, huku kukiwa na hatari kubwa ya baa la njaa. 

Amesema "Hali ni mbaya sana na ya kutisha, watu milioni 7.1 wataathirika na hali hii ya ukame kabla ya mwisho wa mwaka huu". 

Watoto milioni 1.4 wanakabiliwa na utapiamlo mkali.  

Amesema kuwa karibu watoto milioni 1.4 wanakabiliwa na utapiamlo mkali mwaka huu, na wengine 330,000 wana uwezekano wa kuwa na unyafuzi 

Hadi kufikia mwezi Mei, kulingana na ripoti ya hivi karibuni kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Wasomali wapatao milioni 6.1 wameathiriwa na wako katika hali ya dharura kutokana na ukame. 

Kati ya idadi hiyo, 771,400 wamelazimika kuyahama makazi yao kwa ajili ya kwenda kutafuta maji, chakula na malisho, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.  

Mtazamo umezidi kuwa mbaya kutokana na matarajio ya kutokuwa na msimu wa mvua unaopaswa kwa mwaka wa tano mfululizo. 

Bwana Abdelmoula ameyasema hayo wakati akizungumza katika kambi ya ADC ya wakimbizi wa ndani (IDPs) katika wilaya ya Baidoa kwenye jimbo la Kusini Magharibi mwa Somalia.  

Katika ziara hiyo aliandamana na mjumbe maalum wa Somalia wa kukabiliana na ukame, Abdirahman Abdishakur, ambaye aliteuliwa na rais wa Somalia mwishoni mwa mwezi Mei. 

Wanawake na watoto katika kambi ya ADC ambako wakimbizi wapya wamefika Baidoa, Somalia.
UN Photo/Fardosa Hussein
Wanawake na watoto katika kambi ya ADC ambako wakimbizi wapya wamefika Baidoa, Somalia.

 

Hakuna mvua ya kutosha 

OCHA imesema wakati wa mwezi Aprili hadi katikati ya Mei mwaka huu, mvua nyepesi hadi za wastani zilirekodiwa katika maeneo ya kusini, kati na kaskazini Magharibi mwa Somalia, na kulikuwa na dhoruba na mafuriko katika baadhi ya maeneo. 

Lakini kiasi cha mvua kilikuwa chini ya wastani, kilikuwa hafifu katika maeneo mengi na hakitoshi kupunguza hali ya sasa ya ukame. 

Shirika hilo la misaada ya kibinadamu limeongeza kuwa kutokana na mvua hizo duni, Somalia inakabiliwa na msimu duni wa mvua wa nne mfululizo na kuzidi kuwa na hatari ya kukumbwa na njaa katika maeneo sita ikiwa ni pamoja na Jimbo la Kusini Magharibi hasa kama bei ya chakula itaendelea kupanda na usaidizi wa kibinadamu hautaendelezwa ili kufikia watu walio katika mazingira magumu zaidi. 

Zaidi ya hayo, msimu ujao wa mvua unatarajiwa kuwa chini ya wastani pia , nah ii inamaanisha hali ya dharura ya ukame itazidi kuwa mbaya.  

Wakati nchi inakabiliwa na hatari ya njaa katika maeneo hayo sita, mashirika ya misaada ya kibinadamu yanaongeza msukumo wa shughuli zao kuanzia katika kukabiliana na ukame hadi kuzuia njaa, kuelekeza upya  mwelekeo wa jitihada zao ili kulenga wakazi walio hatarini zaidi na kuendeleza mkakati wa kuzuia baa la njaa. 

Baidoa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi 

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia Adam Abdelmoula akiandamana na mjumbe mpya wa masuala ya ukame Somalia Abdirahman Abdishakur ziarani Baidoa, Somalia
UN Photo/Fardosa Hussein
Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia Adam Abdelmoula akiandamana na mjumbe mpya wa masuala ya ukame Somalia Abdirahman Abdishakur ziarani Baidoa, Somalia

Wilaya ya Baidoa katika Jimbo la Kusini Magharibi ni mojawapo ya maeneo ya Somalia ambayo yameathiriwa zaidi na ukame wa sasa. 

Tangu mwanzoni mwa mwaka, watu 230,000 wamelazimika kulihama Jimbo la Kusini Magharibi. 

Eneo lake la Bay lina idadi kubwa zaidi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula,  hii ni pamoja na viwango vya juu vya utapiamlo, hasa katika kambi za wakimbizi wa ndani za Baidoa. Tangu Machi, visa vya kuhara kutokana na maji vimekuwa vikiongezeka, na jumla ya visa 2,279, pamoja na vifo 11, vimeripotiwa tangu Januari mwaka huu. 

"Niko hapa kuhamasisha, kadri niwezavyo, rasilimali, na kuratibu juhudi za misaada ya kibinadamu. Baidoa ni mahali ambapo watu ambao wameathirika zaidi wamefika hivi karibuni na karibu nusu yao ambao wamehamishwa na ukame wako hapa Baidoa," amesema Bwana. Abdishakur katika kambi ya ADC. Ameongeza kuwa "Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zao maradufu na kuunga mkono watu wa Somalia katika wakati huu mgumu." 

Bwana Abdelmoula, ambaye pia anahudumu kama naibu mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa, amebainisha kuwa shirika hilo la kimataifa na washirika wake wanaweza kufanya mengi bila rasilimali zaidi. 

Fedha kidogo, mahitaji yanayoongezeka 

Ufadhili wa hatua za misaada ya kibinadamu wa mwaka huu kwa Somalia, ambao unasaka takriban dola bilioni 1.5 kusaidia watu milioni 5.5 Wasomali walio hatarini zaidi, unasalia kufadhiliwa kwa kiwango cha chini cha asilimia 15.7 pekee hadi kufikia tarehe 20 Mei. 

"Kwa rasilimali chache tulizonazo, tumeweza tu, kati ya miezi ya Januari na Aprili, kufikia watu milioni 2.4 kati ya wale wote wanaohitaji msaada wa kibinadamu," Mratibu wa misaada ya kibinadamu amesema. 

Mjumbe huyo maalum na mratibu wa misaada ya kibinadamu wanakusudia kufanya ziara zaidi za pamoja katika siku za usoni.