Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatujala siku nne tunaomba chakula: wakimbizi wa ndani nchini Somalia

Mkazi wa Somalia akiuza nyama sokoni Hudur, ambako uhaba wa chakuna unaendelea kuwatesa
UN Photo/Tobin Jones)
Mkazi wa Somalia akiuza nyama sokoni Hudur, ambako uhaba wa chakuna unaendelea kuwatesa

Hatujala siku nne tunaomba chakula: wakimbizi wa ndani nchini Somalia

Msaada wa Kibinadamu

Wakimbizi wa ndani katika kambi ya Xudur nchini Somalia wameomba wahisani kuwasaidia kupata chakula kwa haraka ili kunusuru maisha yao kwakuwa sasa wameishi siku nne bila ya kupata chakula.

Akiwa ameketi nje ya nyumba yake iliyotengenezwa kwa mifuko ya sandarusi na mabox katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Xudur nchini Somalia, bibi Fatuma Nishow mwenye umri wa wa miaka 80, mama wa watoto watano anasema hajui atapata wapi chakula. “Hatujapika chakula kwa siku nne zilizopita sababu hatuna chakula. Tunakufa na njaa. Tunahitaji hitaji sana kusaidiwa”

Miezi mitatu iliyopita, wapiganaji wa Al- Shabaab waliwalazimisha bi Fatuma na famiia yake kuyakimbia makazi yao huko Moorigaabey Kijiji kilichoko kikometa 30 kutoka Xudur. 

Watoto wake wanakaa na ndugu zake naye huwatumia fedha baada ya kupokea msaaada wa dola 70 hapa kambini. "Tumewakimbia Al-Shabaab. Wametufukuza, wametulazimisha kutafuta makazi na msaada hapa kambini, tuna wasiwasi, tunanjaa, na tunahitaji kitu cha kula”

Ziara ya mawaziri wa Somalia na maafisa kutoka Umoja wa Mataifa kwa kutumia ndege ya Umoja huo inawafikisha kambini hapa ambapo mawasiliano ya barabara yameharibiwa na Al-shabaab hivyo kuwa vigumu kufikisha misaada. 

Mohamedkheyr Nur mwenye umri wa miaka 75, baba wa watoto kumi ,mkimbizi wa ndani kutoka Daleeley anasema “Maombi yangu kwa wafadhili ni kwamba, mimi ni mkimbizi wa ndani ninayeishi hapa. Utegemezi wetu wote ni mashirika ya misaada na Mungu ili tuweze kuishi. Tunateseka sana. Tunaomba chakula, mavazi ya staha na shule kwa ajili ya watoto. Tunahitaji usaidizi wa vitu vingi.”

Afisa Mkakati wa mawasiliano na uratibu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu  Masuala ya Kibinadamu, Olga Cherevko, anasema hali inaweza kuwa mbaya zaidi ikiwa hawatapata msaada hivi karibuni "Mapungufu yaliyopo sasa yanaweza kuongezeka kwa sababu watu wengi wanakimbia mizozo na ukame ," 

Somalia ina idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani duniani. Takriban watu milioni 2.9 sawa na asilimia 25 au idadi ya watu wanchi wote ni watu walioyakimbia makazi yao.