Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wimbi la OMICRON lisisababishe shule kufungwa: UNICEF

Mwanafunzi akiwa darasani
UNICEF TANZANIA
Mwanafunzi akiwa darasani

Wimbi la OMICRON lisisababishe shule kufungwa: UNICEF

Afya

Wakati idadi ya wagonjwa wa Corona au COVID-19 wakiwa wanaongezeka tena ulimwenguni kote, wakichochewa na aina mpya ya kirusi cha Omicron, serikali nyingi zimeanza kufikiria iwapo zifunge shule kama njia mojawapo ya kupunguza kusambaa kwa maambukizi. 

Lakini Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa lakuhudumia watoto UNICEF Henrietta Fore amesema  nchi zinapaswa kuhakikisha ufungaji shule ni suala la mwisho na kufungua shule liwe jambo la kwanza. 

Ameeleza kuna mambo mengi yanatokea kwa maamuzi ya kufunga shule, ukiachilia mbali wanafunzi kupoteza muda wa kujisomea na mengine ni kama ufikiaji wa huduma za afya na mlo wao wa pekee wa siku hupotea.

“Kizazi hiki cha watoto wa shule kwa pamoja kinaweza kupoteza jumla ya dola trilioni 17 mdio maana kufungwa kwa shule kote nchini kunapaswa kuepukwa kila inapowezekana. Wakati maambukizi ya jumuiya ya COVID-19 yanapoongezeka na hatua madhubuti za afya ya umma kuwa jambo la lazima, shule lazima ziwe sehemu za mwisho za kufungwa na za kwanza kufunguliwa tena.” Amesema Fore.

 Ameongeza kuwa wanafahamu ni lazima hatua za kupunguza maambukizi shuleni zinafaa kuchukuliwa lakini ni lazima tutumie maarifa haya kufanya kila tuwezekanazo kuhakikisha shule zinakuwa wazi.

Mkuu huyo wa UNICEF ameongeza kuwa “Lazima pia tuongeze uwekezaji katika kuwaunganisha kidijitali ili kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma mwaka 2022 hauwezi kuwa mwaka mwingine wa masomo yaliyotatizika. Mwaka huu huo mpya unahitaji kuwa mwaka ambao elimu, na maslahi bora ya watoto, yanatangulizwa.”