Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wanawake wa UN wavalia njuga unyanyasaji wa kijinsia

Akina mama wa Mexico ambao binti zao wamekuwa waathiriwa wa mauaji ya wanawake wanadai haki.
Primavera Diaz
Akina mama wa Mexico ambao binti zao wamekuwa waathiriwa wa mauaji ya wanawake wanadai haki.

Viongozi wanawake wa UN wavalia njuga unyanyasaji wa kijinsia

Wanawake

Tunajua kinachofanya kazi. Lakini kwa nini hatuoni athari zake tusipofanyia kazi? Ndio swali lililoongoza mazungumzo kati ya Viongozi Wakuu Wanawake wa Umoja wa Mataifa wakati wakijadili kuhusu Kukomesha Unyanyasaji dhidi ya Wanawake na Wasichana duniani.

Viongozi sita wanawake waandamizi wa Umoja wa Mataifa katika mkutano huo wameeleza kwa nyakati tofauti kuwa iwe nyumbani, kazini, barabarani au hata mtandaoni, wanawake na wasichana kote ulimwenguni wanasalia kuwa katika hatari ya kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia, jambo ambalo janga la coronavirus">COVID-19 limelikuza zaidi. 

Viongozi hao  ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed na wakuu wa mashirika muhimu ya Umoja wa Mataifa, walichunguza njia za kumaliza "dharura hii isiyoonekana" wakati wa mjadala uliofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Mazungumzo hayo ya wazi yaliandaliwa na program iitwayo Spotlight Initiative, ambayo ni mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya -EU unaofanya kazi kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Viongozi walioshiriki

Mkutano huo uliongozwa na Melissa Fleming, mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa uliwaleta pamoja Amina J. Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF

Wengine ni  Ghada Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa UNODC na Reem Alsalem, Mwandishi  Maalum wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya unyanyasaji dhidi ya wanawake Pamoja na wadau wengi kwa njia ya mtandao na wachache wakiwa ukumbini.

'Hatari iliyowazi na ipo sasa'

Akifungua mjadala huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed alielezea unyanyasaji wa kijinsia kuwa ni "hatari ya wazi na iliyopo" kwa mamilioni ya wanawake na wasichana duniani kote.

Muendesha mjadala huo Fleming, ambaye ni mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa, alimuuliza kuhusu athari za wanawake kulengwa na unyanyasaji akigusia pia athari za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu -SDGs.

"Kimsingi kinachofanywa ni kuweka malengo yote (SDG) hatarini," alisema Bi. Mohammed. "Kwa sababu bila asilimia 50 ya ubinadamu kufunikwa na hili basi masuala ya kumaliza umaskini, upatikanaji wa elimu, au kazi ya heshima yote yako hatarini."

Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
UN Women/Erica Jacobson
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia

Sio kwamba unyanyasaji hauonekani 

Unyanyasaji wa kijinsia unaingia katika nyanja zote za maisha, iwe ya umma au ya faragha, alisema Reem Alsalem, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu. Pia huanza mapema, katika utoto, ikiwakilisha "mwendelezo" wa vurugu.

"Ndiyo maana ninajiuliza ikiwa kweli tunazungumzia juu ya dharura isiyoonekana kwa maana kwamba inaonekana kabisa kwa wale wanaotaka kuiona," alisema Bi. Alsalem, ambaye pia ni Mwandishi  Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake na kuongeza kuwa "Ni kama mabadiliko ya tabianchi. Ushahidi upo. Tunaweza kuona, tunaweza kuona matokeo yake."

Majadiliano hayo yalitumika kama njia ya kutoa kanuni kwa Siku 16 za Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake, kampeni ya kila mwaka ya kimataifa inayoanza tarehe 25 Novemba hadi 10 Desemba, Siku ya Haki za Binadamu.

COVID-19 iliongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha unyanyasaji wa kijinsia duniani kote, ingawa takwimu zozote hazijaripotiwa, kulingana na Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA.

Kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia wakati wa janga hilo pia kuliunda "eneo la hatari" kwa wanawake na wasichana, alisema, ambapo waliwindwa na kunyanyaswa.

Kuogopa kuongea

Suala hili pia liliibuliwa na Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji -UNICEF, ambaye alizungumzia hatari zinazowakabili wasichana wadogo na barubaru mtandaoni, kama vile kujiremba na kutumiwa ujumbe wa ngono, jambo ambalo linaweza kuharibu afya yao ya akili.

Umoja wa Mataifa umeelezea kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia unaoambatana na kuenea kwa COVID-19 kama "janga lililofunikwa na kivuli". Lakini pamoja na kuongezeka kwa matukio, wanawake wamekuwa wakisita kusema juu ya unyanyasaji waliopata.

UN ilifanya utafiti kwa wanawake 16,000 katika nchi 13 uligundua kwamba wakati mwanamke kati ya wawili walisema wanawajua wanawake wengine au wao wenyewe walishafanyiwa unyanyasaji tangu kuanza kwa janga hili, na ripoti hiyo ilieleza ni mwanamke mmoja tu kati ya 10 aliyeripoti suala hilo kwa polisi.

Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia
UN Women Tanzania/Deepika Nath
Jijini Dar es Salaam, Tanzania , wanafunzi wasichana wakiwa kwenye maandamano yaliyoandaliwa kupinga ukatili kijinsia

Kudhulumiwa mara mbili

Zaidi ya hayo, takwimu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa na Uhalifu UNODC ilifichua kuwa mwaka jana, wanawake na wasichana 47,000 waliuawa na wapenzi wao au wanafamilia.

Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, kiwango cha chini cha imani kwa wanawake katika taasisi ambazo zinapaswa kuwalinda, kilikuwa kinatia wasiwasi. Alihofia kuwa wanawake walikuwa wakidhulumiwa mara mbili.

"Kwanza, walifanyiwa vurugu. Kisha wakakosa usiadizi wa kupata haki zao. Na, mara nyingi wanaona kwamba hata wanapotoa taarifa juu ya matukio hayo, wahalifu ni nadra sana kufikishwa mahakamani,” alisema.

Janga la COVID-19 limeongeza matumizi ya mtandao kwa kiasi kikubwa, kwani shughuli nyingi zimehamia mtandaoni.
© UNICEF/Schermbrucke
Janga la COVID-19 limeongeza matumizi ya mtandao kwa kiasi kikubwa, kwani shughuli nyingi zimehamia mtandaoni.

Kuvunja ukimya

Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaendelea kufanya kazi kusambaratisha kile ambacho baadhi ya washiriki walikiita "njama ya ukimya" inayohusu unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, na kuhakikisha kwamba wanaweza kupaza sauti zao.

Kupitia Mpango wa Spotlight, baadhi ya wanawake na wasichana 650,000 waliweza kupata huduma licha ya janga linaloendelea.

Bi. Fore wa pia aliangazia mifano ya shughuli za UNICEF katika nchi mbalimbali  kama vile Mexico, ambapo shirika hilo lilianzisha ushirikiano na Serikali na sekta ya masuaka ya ukarimu ili kutoa makazi salama katika hoteli kwa wanawake walionusurika na watoto wao, ambayo ni muhimu sana wakati wa janga hilo.

Wakati huo huo, nchini Iraqi, Equador na Lebanon, UNICEF ilitenga maeneo salama ili kuongeza ufikiaji wa huduma na habari kwa wanawake na wasichana, haswa wale wenye ulemavu au wanaokabiliwa na aina zingine za kutengwa.

Je! mipango hii na mingine mingi inaweza kukuzwa ulimwenguni? 
Ndiyo, lilikuwa jibu kutoka kwa Bi. Fore, akiongeza kuwa Mpango wa Spotlight umetumika kama nafasi nzuri ya ushirikiano kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Ghada Waly, mkuu wa UNODC, alitaja maendeleo mengine mazuri ambayo yaliibuka kutokana na janga hilo. Serikali sasa zinatambua kwamba lazima ziwekeze katika ukuaji wa kidigitali na mifumo ya mtandaoni, au "e-platforms", ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika masuala ya  haki na kutaja maeneo zaidi ya kuboresha.

"Tunajua wanawake wanakuwa salama zaidi unapokuwa na polisi wanawake wengi, unapokuwa na majaji wanawake wengi, unapokuwa na usawa na uwakilishi wa kijinsia kwa wale wanaofanya maamuzi na kupokea wito wa usaidizi."