Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 274 kuhitaji msaada wa dharura 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17%: UN

Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan, licha ya msukosuko wa kisiasa.
© WFP/Arete/Andrew Quilty
Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan, licha ya msukosuko wa kisiasa.

Watu milioni 274 kuhitaji msaada wa dharura 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17%: UN

Msaada wa Kibinadamu

Jumla ya watu milioni 274 duniani kote watahitaji msaada wa dharura na ulinzi mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 17% ikilinganishwa na mwaka huu imesema tathimini ya hali ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo. 

Kwa mujibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa idadi hiyo ya watu ni sawa na "Idadi iliyo katika nchi ya nne kkuwa na watu wengi duniani” wakati wa uzinduzi wa mtazamo huo wa kimataifa wa hali ya kibinadamu kwa mwaka 2022 (GHO) huko Geneva Uswisi.

Mtazamo huo unaotolewa kila mwaka na Umoja wa Mataifa na washirika wake unajumuisha mipango 37 ya kukabiliana na dharura za kibinadamu katika nchi 63. 

Tathimini hiyo inakadiria kwamba dola bilioni 41 zinahitajika kutoa misaada na ulinzi kwa watu milioni 183 wanaohitaji zaidi msaada huo. 

Wasiojiweza ndio waathirika wakubwa 

"Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unakumba kwanza watu walio hatarini zaidi ulimwenguni kwanza na unakuwa mbaya zaidi. Mizozo ya muda mrefu inaendelea, na ukosefu wa utulivu na usalama umekuwa mbaya  zaidi katika sehemu kadhaa za dunia , hususan Ethiopia, Myanmar, na Afghanistan, na pia bila shaka janga la coronavirus">COVID-19, ambalo tumekumbushwa hivi karibuni kwamba halijaisha huku nchi maskini zikikosa chanjo.” Amesema Bw. Griffiths  

Ameongeza kuwa "Lengo langu ni kwamba ombi hili la kimataifa linaweza kufika mbali kwa kiasi fulani kurejesha mwanga wa matumaini kwa mamilioni ya watu wanaohitaji sana msaada.” 

Mwanamke aliyetoka kujifungua akifanyiwa uchunguzi na mkunga katika kliniki inayohama nchini Afghanistan.
© UNFPA Afghanistan
Mwanamke aliyetoka kujifungua akifanyiwa uchunguzi na mkunga katika kliniki inayohama nchini Afghanistan.

Umaskini uliokithiri unaongezeka 

Kulingana na ripoti hiyo ya mtazamo wa hali ya kibinadamu duniani, zaidi ya asilimia moja ya watu duniani wamekimbia makazi yao na umaskini uliokithiri unaongezeka tena. 

Katika majanga mengi, wanawake na wasichana wanateseka zaidi, kwani kuna ongezeko kubwa la kukosekana kwa usawa wa kijinsia na hatari za kutokuwa na ulinzi. 
Bw. Griffiths amebainisha kuwa kuna watu milioni 45 wanaoishi katika nchi 43, ambao wako katika hatari ya njaa. 

Ili kuzuia njaa ulimwenguni na kushughulikia matishio makubwa yanayosababisha uhaba wa chakula,  mizozo, mabadiliko ya tabianchi, COVID-19 na majanga ya kiuchumi, mashirika 120 ya asasi za kiraia , karibu 100 kati ya hayo yakiwa katika nchi zilizokumbwa na njaa yametoa ushirikiano kwa kutoa barua ya pamoja ikiwataka viongozi wa dunia kutimiza wajibu wao wa kufadhili kikamilifu hatua za kupambana na changamoto hizo.

Wakulima wanawake wanahimizwa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa
UNDP/PraiseNutakor
Wakulima wanawake wanahimizwa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa

Mwaka wa changamoto na mafanikio  

Mwaka huu wa 2021 "shukrani kwa wafadhili wakarimu mfumo wa kibinadamu umeweza kukabiliana na changamoto na kuwasilisha chakula, dawa, huduma za afya na misaada mingine muhimu kwa watu milioni 107 ikiwa ni asilimia 70 ya lengo.” Amesema Bw. Griffiths huku akiongeza kuwa nchini Sudan Kusini, zaidi ya watu nusu milioni wameokolewa kutoka kwenye hatihati ya baa la njaa. 

Pia amesema jumuiya ya kimataifa imefanikiwa kutoa huduma ya afya kwa watu milioni 10 nchini Yemen, na pia kuzuia baa la njaa.  

Mbali ya hayo mkuu huyo wa masuala ya kibinadamu ameongeza kuwa mashirika ya misaada "Hayakuwahi kuondoka Afghanistan, kufuatia kundi la Taliban kutwaa mamlaka mwezi Agosti. Tuna mpango wa mwaka 2022, ambao ni mara tatu ya ukubwa wa mpango wa 2021 kwa sababu ya ongezeko la mahitaji ". 

(PHOTO) 

Misaada inaweza kuleta mabadiliko  

Mkuu huyo wa masuala ya kibinadamu amewashukuru wafadhili wa kimataifa na mataifa wanachama ambao, hadi sasa mwaka 2021, wametoa zaidi ya dola bilioni 17 kwa ajili ya miradi iliyojumuishwa katika GHO, licha ya matatizo ya kiuchumi yanayoletwa na janga la COVID-19. 

Lakini amekumbusha kwamba "sio pesa nyingi ukilinganisha na mahitaji". Ufadhili unasalia kuwa chini ya nusu ya kile Umoja wa Mataifa na mashirika wadau walichoomba. 

"Misaada ni muhimu na inaweza kuleta mabadiliko", Amesisitiza Bw Griffiths akiongeza kuwa “Sio suluhu kama tunavyoona nchini Afghanistan. Usaidizi si chahu na si njia ya kuleta utulivu katika jamii. Haichukui nafasi ya usaidizi wa maendeleo, ufadhili wa jamii na uchumi. Ni ziada, tu ya kuokoa maisha. Tunafahamu hatutapata dola bilioni 41, lakini tutajaribu na kupata kile tunachoweza.”