Ufadhili wahitajika haraka kukidhi mhitaji ya kibinadamu Burkina Faso: Griffiths
Ufadhili wahitajika haraka kukidhi mhitaji ya kibinadamu Burkina Faso: Griffiths
Mkuu wa masuala ya kibinadamu na mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amehitimisha ziara fupi nchini Burkina Faso na kusema alichokishuhudia ni madhila kwa mamilioni ya watu ambao wanahitaji msaada wa dhariura kikidhi mahitaji ya msingi.
Katika taarifa yake iliyotolewa mwisho wa ziara hiyo bwana Griffiths ambaye pia ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA amesema huu ni wakati muhimu sana kwa Burkina Faso akitaja sababu kuu tatu.
Mosi, mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka haraka. Robo ya watu wa taifa hilo ambao ni saw ana watu milioni 4.9 wanahitaji msaada wa dharura, ikiwa ni asilimia 40 zaidi ya watu kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa mwaka.
Mmoja kati ya kwatu 10 wa Burkina Faso wamefurushwa kutoka kwenye makazi yao kutokana na migogoro na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.
Pili, kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na vizuizi katika maeneo mengi kumesababisha jamii kutengwa na maeneo mengine ya nchi na kukabiliwa na njaa inayoongezeka.
Pia wafanyakazi wa misaada wa misaada ya kibinadamu wanapata changamoto kuwafikia watu wanaohitaji msaada.
Na tatu, kiasi cha msaada wa kibinadamu kinachopatikana hakitoshi. Ili kutoa usaidizi muhimu wa kuokoa maisha kwa wale wanaohitaji kwa kiwango cha hadhi na heshima ambayo kila mwanadamu anastahili, “Tunahitaji rasilimali zaidi kwa haraka. Mpango wetu wa kuchukua hatua wa dola $805 milioni nchini Burkina Faso umefadhiliwa chini ya theluthi moja.”
Watu wanakula majani na chumvi tu
Mkuu huyo wa OCHA ameongeza kuwa amepata fursa ya kukutana na watu, jumuiya zilizofurushwa na mwenyeji wanaohifadhi wakimbizi, katika mji wa Djibo kaskazini mwa Burkina Faso.
Na pia amezungumza na wanawake na watoto ambao amesema wamemuelekeza kuwa “Wamekula majani na chumvi tu kwa wiki nzima. Hali ni mbaya sana kiasi kwamba wanawake wanahatarisha maisha yao, wakivuka mipaka ya udhibiti wakati wa usiku Kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya watoto wao”.
Pia amezungumza na viongozi wa jamii ambao wametoa wito kwa wale wanaohusika kufungua barabara kwa ajili ya kuingiza chakula, maji, na dawa muhimu, ili kuokoa maisha.
Licha ya changamoto hizo Griffiths amesema “Kuna mipango ya amani ya kutafuta suluhu na bado kuna matumaini. Watu wa Djibo wanastahili heshima yetu, pongezi na msaada wetu zaidi katika wakati huu wa uhitaji mkubwa.”
Ulinzi wa rai ani muhimu sana
Walipokutana na Rais wa uongozi mpya wa serikali ya mpito Ibrahim Traoré, amesema wamejadili kwa kina hali nchini humo na amesisitiza haja ya ulinzi wa raia ikiwemo wale ambao hawawezi au hawako tayari kuondoka katika maeneo yenye operesheni za kijeshi
“Pia nimerejea kusisitiza wajibu wa mamlaka ya kitaifa kuweka mazingira bora kwa ajili ya operesheni za kibinadamu na kuwapa fursa wahudumu wa kibinadamu ili kuweza kuwafuikia Waburkina Faso wenye mahitaji ya dharura kila mahali nchini humo.” Ameongeza bwana Griffiths.
Licha ya changamoto zilizopo afisa huyo wa Umoja wa Mastaifa amesema hatua za kibinadamu zinaleta mabadiliko makubwa nchini Burkina Faso.
Watu milioni 1.8 wamepata msaada
Kwa mujibu wa OCHA katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wamefikisha msaada wa chakula kwa watu milioni 1.8 na kusaidia watu wengine 740,000 kupata huduma za afya katika maeneo ambayo vituo vya afya vimefungwa na ambapo vifaa vya matibabu vinakosekana.
Piawametoa huduma ya maji, kujisafi na usafi wa mazingira kwa watu 550,000 na msaada wa lishe kwa watoto 421,000 na mama ambao ni wazazi wapya na wajawazito.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu,shitrika hilo limesema wafadhili wa misaada ya kibinadamu wametoa kwa ukarimu takriban dola milioni 100 kupitia mfuko mkuu wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa CERF ili kukabiliana na dharura, kwa nchi za Burkina Faso, Cameroon, Chad, Mali, Mauritania, Niger na Nigeria. Ufadhili huu umetuwezesha kukabiliana na changamoto ya watu kuhama makazi yao, ukame, hatari ya njaa na utapiamlo.
Dola zingine milioni 33 zimetolewa kupitia mfuko wa kibinadamu wa Kikanda, ambao utawezesha kusaidia vyema programu zinazoongozwa na jamii.
Hata hivyo, shirika hilo limeongeza kuwa rasilimali nyingi zaidi zinahitajika ili kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ambayo yanasumbua ukanda huo.