Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatoa msaada wa dola milioni 15 kusaidia uhaba wa chakula nchini CAR

Marceline akisaidiwa na rafiki yake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR
Rena Effendi
Marceline akisaidiwa na rafiki yake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR

UN yatoa msaada wa dola milioni 15 kusaidia uhaba wa chakula nchini CAR

Msaada wa Kibinadamu

Mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF umetenga dola milioni 15 kwa ajili ya msaada wa chakula kwa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR nchi ambayo imeripotiwa kuwa na uhaba mkubwa wa chakula ikifuatiwa na nchi za Yemen, Sudan Kusini na Afghanistan. 

Taarifa kutoka Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati iliyotolewa leo na OCHA imesema msaada huo uliotangazwa leo na Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA Martin Griffiths ambaye amesema fedha hizo zitasaidia zaidi ya watu laki mbili katika vitongoji 10 ambapo uhaba wa chakula ni mkubwa zaidi.

Mratibu wa misaada ya Kibinadamu nchini CAR Denise Brown amesema “msaada huo ni ahueni inayohitajika sana kwa maelfu ya watu ambao wanatatizika kupata hata mlo mmoja kwa siku. Kipaumbele kwetu ni kuokoa Maisha, msaada huu wa dharura utasaidia watu kupata chakula, kurejea tena kwenye kilimo kwenye maeneo inapowezekana na kutibu utapiamlo.“

Watu milioni 2.2 hawana uhakika wa chakula cha kutosha ikiwa ni sawa na asilimia 36 ya idadi ya wananchi wote wa taifa hilo. 

Mtoto akiwa ameshika sabuni aliyopewa msaada na UNICEF (Maktaba)
Pierre Holtz
Mtoto akiwa ameshika sabuni aliyopewa msaada na UNICEF (Maktaba)

Sababu ya uhaba mkubwa wa chakula 

Taarifa kutoka CAR imeeleza sehemu kubwa ya watu hawa wanaokabiliwa na uhaba wa chakula wanaishi kwenye maeneo yaliyoathirika na mizozo ambapo ukosefu wa usalama pamoja na watu kuyakimbia makazi yao kumesababisha kupungua kwa maeneo ya watu kulima na pia kukwambisha upatikanaji wa mashamba. 

Athari ya vita ya Ukraine imezidisha tatizo nchini humo ambapo bei za bidhaa za chakula zinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 70 ifikapo mwezi Agosti mwaka huu 2022. 

Mratibu wa Misaada wa CAR Brown amesema, kupitia fedha hizo za msaada kutoka CERF watahakikisha watu wanapata si chakula pekee bali huduma ya afya na maji safi pamoja na mahitaji mengine. 

Jumla ya mashirika sita ya Umoja wa Mataifa yanatarajiwa kupanua usambazaji wa chakula na kutoa fedha taslimu kwa ajili yakuboresha maisha ya watu kupitia usambazaji wa zana za kilimo pamoja na mbegu. 

Kukamilika kwa afua hizo, na msaada wa lishe utaongeza kunusuru watoto na kusaidia familia zenye watoto walio na utapiamlo mkali kupata maji safi ya kunywa, usafi wa mazingira na vifaa vya kujisafi pamoja na kuwajengea mazoea bora ya usafi muhimu kwa ajili ya kuishi salama.