Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je wafahamu misingi iliyowezesha Kiswahili kuadhimishwa 7/7?

Azimio la UNESCO la kutangaza tarehe 7 Julai kuwa siku ya Kiswahili duniani.
UNESCO
Azimio la UNESCO la kutangaza tarehe 7 Julai kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Je wafahamu misingi iliyowezesha Kiswahili kuadhimishwa 7/7?

Utamaduni na Elimu

Mkutano Mkuu wa 41 wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO tarehe 23 mwezi huu wa Novemba mwaka 2021 ulipitisha azimio namba 41C/61 la kutangaza tarehe 7 mwezi Julai kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Katika azimio hilo lenye kurasa tatu, inaelezwa kuwa uamuzi huo unatokana na uamuzi wa kikao cha 212 cha Bodi Tendaji ya UNESCO kwa kutambua misingi mikuu 10.

Misingi 10 ni ipi?

Kiswahili na mawasiliano

Lugha siyo tu njia ya mawasiliano bali  ni kielelezo cha utamaduni na huonesha utambulisho, maadili na dira ya dunia. Ni chombo ambacho kinawasilisha tofauti mbalimbali za tamaduni na mazungumzo ya ustaarabu. Ni daraja linalowezesha uhusiano wa karibu baina ya jamii n ani utajiri thabiti wa kujieleza na kubadilishana mitazamo mbalimbali pamoja na kumwezesha mtu.

Wazungumzaji wa Kiswahili duniani

Kiswahili ni moja ya lugha zinazozungumzwa zaidi barani Afrka na huzungumzwa zaidi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani, ikiwa na wazungumza zaidi ya milioni 200.

Tweet URL

Kiswahili Afrika Mashariki, Kati na Kusini

Ni lugha inayotumika zaidi katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Kati na kusini pamoja na Mashariki ya Kati. Kiswahili kinafundishwa katika Vyuo Vikuu vikubwa duniani.

Kiswahili na kufanikisha SDGs na AcFTA

Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC. Ni kwa mantiki hiyo ni mbinu muhimu sana katika kufanikisha ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kufanikisha pia ushirikiano wa kikanda hususan katika kutekeleza mkataba wa eneo la soko barani Afrika, ACFTA.

Kiswahili katika Idhaa za Umoja wa Mataifa

Katika miaka ya 1950, Umoja wa Mataifa ulianzisha Radio ya Umoja wa Mataifa na leo hii Kiswahili ni Idhaa pekee ya lugha ya kiafrika kwenye Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, DGC.

Umoja wa Mataifa na Matumizi ya lugha zaidi ya moja 

Matumizi ya lugha zaidi ya moja ambayo ni msingi wa maadili ya Umoja wa Mataifa ni kigezo muhimu cha kujenga mawasiliano bora baina ya watu, kwa kuwa inasongesha umoja katika utofauti na maelewano ya kimataifa , stahmala na mashauriano. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 71/328 la tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2017 kuhusu matumizi ya lugha zaidi ya moja, lilikaribisha utekelezaji wa kutengwa kwa siku mahsusi kuadhimisha kila lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa ili kuhabarisha na kupaza Sauti kuhusu historia ya lugha hiyo utamaduni wake, matumizi na kuhamasisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na taasisi kama vile UNESCO kufikiria kupanua wigo wa mpango huo kwa hata lugha nyingine zisizo rasmi lakini zinazungumzwa duniani.

Kiswahili na utajiri katika utofauti wa kiisimu

Tofauti ya kiisimu na uzungumzaji wa lugha mbalimbali ni maeneo yenye umuhimu wa kimkakati ambayo UNESCO inaendeleza katika nyanja zote kupitia majukumu yake ya kisekta. Kuna mafanikio makubwa sasa ya uelewa kuhusu nafasi ya lugha katika maendeleo siyo tu katika kuhakikisha vinafanikisha utofauti wa kitamaduni na mashauriano baina ya watu wa lugha na tamaduni mbalimbali bali pia katika kufanikisha elimu bora kwa wote na kuimarisha ushirikiano katika kujenga ufahamu kwenye jamii na kuhifadhi urithi wa utamaduni na kusongesha utashi wa kisiasa wa kunufaika na sayansi na teknolojia kwa maendeleo endelevu.

Kiswahili ni lugha rasmi ya SADC

Mkutano wa 39 wa viongozi wa SADC waliokutana jijini Dar es salaam nchini Tanzaina mwezi Agosti mwaka 2019, waliridhia Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kazi katika chombo hicho, kwa kutambua mchango wake katika kujenga amani na ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla.

Kwa nini 7/7 na si tarehe nyingine?

Tarehe iliyopendekezwa ya siku ya Kiswahili duniani ni tarehe 7 mwezi Julai kwa kuwa katika tarehe hiyo mwaka 1954 ni siku ambayo chama cha Tanganyika African National Union, TANU chini ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilipitisha Kiswahili kama lugha ya kuunganisha harakati za ukombozi. Bila shaka, Rais wa zamani na pia Baba wa Taifa la Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta, pia alitumia lugha ya Kiswahili kupitia kauli yake maarufu, “Harambee” ya kuhamisha watu wakati wa harakati dhidi ya ukoloni. Zaid iya hapo tarehe 7 mwezi Julai mwaka 2000, jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, ilianzishwa tena kurejesha ushirikiano na utangamano baina ya wananchi wa Kenya, Tanzania na Uganda ambako Kiswahili kinazungumzwa zaidi. Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zimejiunga baadaye na ni wanachama wa EAC.

Maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani

Siku ya kimataifa itaadhimishwa na wadau kwa kutambua umuhimu wa Kiswahili duniani kama lugha ya mawasliano duniani iliyojengwa kwenya maisha ya kila siku ya waafrika kupitia tamaduni zao mbalimbali.

Unaweza kupakua azimio hilo hapa.