Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiswahili ni zaidi ya lugha ya mawasiliano- Azoulay

Siku ya lugha ya Kiswahili duniani
UN
Siku ya lugha ya Kiswahili duniani

Kiswahili ni zaidi ya lugha ya mawasiliano- Azoulay

Utamaduni na Elimu

Habari gani!! Ndivyo salamu zake Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO hii leo katika ujumbe wake wa siku ya kiswahili duniani, ambayo maadhimisho ya kwanza kabisa yamefanyika hii leo.

Akitoa ujumbe wake huo kwa njia ya video, Bi. Azoulay amesema anajisikia furaha sana kusherehekea siku hii ya lugha ya kiswahili huku UNESCO ikiwa inajivunia pia kuwa kitovu cha maadhimisho hayo kufuatia kupitishwa kwa azimio mwezi Novemba mwaka jana wa 2022.

Kiswahili kinasongesha amani

“Tuna shauku kubwa kwa sababu ni kuheshimu suala la kutambua matumizi ya lugha mbalimbali au Multilingualism, ambalo ni muhimu sana kwetu hapa UNESCO, na zaidi ya yote ni kwa sababu Kiswahili ni zaidi ya lugha ya mawasiliano.”

Bi. Azoulay amesema “Kiswahli ni dirisha la kupitia kuelekea tamaduni tofauti tofauti, mawazo, aina za ufahamu wa elimu na pia ina kitu pekee katika mtazamo wake kwa Dunia. Mapinduzi ya lugha hii yamesheheni karne za mabadilishano.”

UNESCO director general's message for the Kiswahili Language day

Mkuu huyo wa UNESCO amesema Kiswahili ambayo ni lugha ya kibantu imeazima maneno ya kiarabu na kuwa pia msingi wa mawasiliano na maeneo ya Mashariki ya Kati.

Amesema ikiwa na zaidi ya wazungumzaji milioni 200, lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani, na hivyo kuweka msingi wa masiliano baina ya watu na nchi.

Kiswahili ni lugha ya diplomasia

Ni lugha ya matangazo hususan hewani kupitia redio za kijamii hasa wakati wa janga la coronavirus">COVID-19 na “UNESCO inajivunia sana kusaidia redio hizo.”

“Kiswahili ni lugha ya diplomasia, na kama lugha rasmi ya Muungano wa Afrika, inasaidia kusongesha ajenda ya Afrika ambayo pia ni kipaumbele kwa UNESCO,” amesema Bi. Azoulay.

Amesema “kupitia utajiri wa utamaduni wake unaowasilisha, ujumbe unaotolewa, madaraja inayojenga, elimu inayotoa na umoja inayoimarisha, kiswahili kinachangia kwenye amani na katika jukumu la UNESCO la kujenga amani. Na neno amani linabeba maadili hayo siyo tu kama kutokuweko kwa mizozo lakini pia kila mara kuchangia kwenye hali ya utulivu.”

“Hii leo hebu na tujizatiti kujenga amani kwa pamoja, heko kwa siku ya kiswahili duniani! Asanteni sana, Thank you,” ametamatisha  Bi. Azoulay.

Kiswahili kwa wageni

Mmoja wa raia wa mataifa ya kigeni ambao ni wanufaika wa moja kwa moja wa lugha ya Kiswahili ni Priscilla Lecomte, mtaalamu wa mawasiliano wa UN- CBi, mpango unaoratibiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNPD kushirikisha sekta binafsi katika kujiandaa kukabiliana na majanga na hata kurejea katika hali nzuri baada ya majanga.

"𝐊𝐈𝐒𝐖𝐀𝐇𝐈𝐋𝐈 𝐊𝐈𝐌𝐄𝐍𝐈𝐏𝐀 𝐀𝐉𝐈𝐑𝐀 𝐔𝐍." - Priscilla Lecomte

Bi. Lacomte ni mzaliwa na raia wa Ufaransa ambaye anaamini lugha zina mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu akitolea mfano lugha aanayoipenda, Kiswahili ambayo alianza kujifunza akiwa kwao Ufaransa kabla ya kubobea liposafri na kuishi Afrika Mashariki kabla ya kupata kazi katika Umoja wa Mataifa ambako alitumia na anaendelea kutumia Kiswahili katika kazi zake.