Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wana imani na mustakabali bora duniani kuliko watu wazima- Kura ya maoni

Wanaharakati vijana wakiandamana katika mitaa ya Glasgow, Scotland kunakofanyika mkutano wa COP26
UN News/Laura Quinones
Wanaharakati vijana wakiandamana katika mitaa ya Glasgow, Scotland kunakofanyika mkutano wa COP26

Watoto wana imani na mustakabali bora duniani kuliko watu wazima- Kura ya maoni

Masuala ya UM

Kura ya maoni iliyoendeshwa katika nchi 21 ikihusisha watoto na watu wazima imeonesha kuwa watoto wanaamini dunia inakuwa bora zaidi huku watu wazima wakiwa na shaka na shuku.

Matokeo ya utafiti huo ulioratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, yametolewa leo kuelekea siku  ya mtoto duniani tarehe 20 mwezi huu wa Novemba ambapo watoto na vijana wanaamini kuwa maisha ya utoto yamekuwa bora kuliko ya wazazi wao sambamba na huduma za afya na elimu. 

Watoto na vijana pia wanajiona wao kuwa raia wa dunia na wanakumbatia ushirikiano wa kimataifa zaidi kukabili changamoto hizo ikiwemo janga la Corona au COVID-19 na wana imani kubwa na wanasayansi katika kutatua changamoto za dunia. 

Ingawa hivyo watoto na vijana licha ya matumaini yao, hawajabweteka na kila uchao wanahaha kusaka majawabu ya changamoto zinazokumba dunia hivi sasa ikiwemo madhara ya tabianchi, msongo wa mawazo na kutokuaminika kwa taarifa ambazo wanazisoma kupitia mitandao ya kijamii. 

 

Watoto hutengeneza boti zao wenyewe kwa kutumia turubai na chupa za plastiki wakati wa mafuriko makubwa huko Sudani Kusini.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Watoto hutengeneza boti zao wenyewe kwa kutumia turubai na chupa za plastiki wakati wa mafuriko makubwa huko Sudani Kusini.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema”kuna sababu lukuki za kuwepo kwa shaka na shuku katika dunia ya leo. Mabadiliko ya tabianchi, umaskini, ukosefu wa usawa,  ongezeko la kutoaminiana na uzawa. Lakini kuna sababu pia za matumaini watoto na vijana wanakataa kuitazama dunia kupitia lensi ya macho ya watu wazima.” 

Bi. Fore amesema watoto na vijana wamesalia na matumaini na wana mtazamo wa kidunia na wako tayari kufanya dunia kuwa pahala bora. Vijana wa leo wana hofu ya siku za usoni lakini wanajiona kuwa sehemu ya majawabu. 

Kura ya maoni ilipatiwa jina la Mradi wa kubadilika kwa utoto, na ni ya kwanza kufanyika ikihusisha vizazi tofauti ikiwa ni kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 na kuanzia miaka 40 na kuendelea. 

Wahusika walitoka maeneo ya Afrika, Ulaya, Asia, Amerika Kaskazini na ya Kati na wenye vipato tofauti tofauti. 

Takwimu kwa ufupi

  • Kwa wastani asilimia 59 ya vijana wanasema watoto wa leo wanakabiliwa na mashinikizo mengi ya kufanikiwa kuliko enzi za utoto wa wazazi wao.
  • Vijana wengi wanahofia watoto wanakumbana hatari zaidi kwenye mitandao kama vile taarifa za kingono na ukatili
  • Ni asilimia 7 tu ya vijana ndio wamesema wana imani na taarifa za kwenye mitandao ya kijamii, wengi hawana imani.

Unaweza kupakua ripoti nzima hapa.