Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maneno ni bei nafuu sana lakini vitendo ni bei ghali, tushirikishe vijana kwa vitendo:Msoka  

Emmanuel Cosmas Msoka, Mchechemuzi wa Vijana wa UNICEF Tanzania kuhusu usafi wa maji, usafi wa mazingira (WASH) na ubunifu.
UN/Anold Kayanda
Emmanuel Cosmas Msoka, Mchechemuzi wa Vijana wa UNICEF Tanzania kuhusu usafi wa maji, usafi wa mazingira (WASH) na ubunifu.

Maneno ni bei nafuu sana lakini vitendo ni bei ghali, tushirikishe vijana kwa vitendo:Msoka  

Utamaduni na Elimu

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu leo unakunja jamvi kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York Marekani. Mkutano huo wa siku tatu umeitishwa ili kukabiliana na changamoto ya kimataifa ya elimu hasa kwa kuzingatia suala la usawa na ujumuishwaji, ubora wa elimu na umuhimu.  

Wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa nchi na serikali, mashirika ya kimataifa na makundi mbalimbali katika jamii wamepata fursa ya kupaza sauti zao, miongoni mwao ni vijana walioshiriki kuwawakilisha mamilioni ya wanafunzi kote duniani.  

Emmanuel Cosmas Msoka mchechemuzi kijana wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kutoka nchini Tanzania ni moja wa vijana waliozungumza akiwachagiza viongozi wa dunia kuwashirikisha vijana kwa hali na mali .

“Moja ya mchango ambao niliweza kuutoa ni ushirikishwaji wa vijana katika mambo yote ambayo yanaathiri mabadiliko ya kiuchumi kwa sasa na kwa baadaye , katika hilo lengo langu kubwa ni kuhakikisha kwamba vijana wanashirikishwa kuanzia katika ngazi ya chini kabisa katika kuanzishwa sheria, katika kuanzishwa kwa mitaala ya elimu, washirikishwe vijana hata katika utekelezaji pia , kwani katika nchi nyingi au katika mazingira ambayo tumetokea ni kwamba vijana wanashirikishwa katika sherehe zile ambazo ni za kuhitimisha baada ya sera au sheria kutengenezwa. Ushirikishwaji ambao mi naungalia ni kuanzia kwenye mipango, kuanzia watu wanaposema kwamba kuna kitu Fulani tunataka tukibadilishe , vilevile unapoanza kukusanya maoni tu vijana washirikishwe , katika utekelezaji wa ile mipangopia tuwashirikishe vijana na mwishoni kabisa katika kusherehekea kwamba lengo tulilojiwekea tumeweza kufanikiwa vijana pia washirikishwe. Ushirikishwaji wao ni kuanzia ngazio yaw azo mpaka kwenye kutengeneza sheria na sera na katika kusherehekea mafanikio ya sera ambazo zimetengenezwa katika nchi.” 

Anold Kayanda
Mchechemuzi wa vijana UNICEF Tanzania, Emmanuel Msoka: Maneno ni bei nafuu sana

 

Na kwa Tanzania anakotoka Emmanuel anasema ni wakati wa kujifunza kutoka kwa wengine 

“Nimejifunza kutoka kwa vijana ambao wametokea katika nchi nyingine hapa wameweza kunielezea kwamba katika nchi zao kuna mabaraza ya vijana, mashirika ya kimataifa katika nchi zao yana mabaraza ya vijana , nchi kama nchi ina baraza la vijana . Tanzania sasa ni muda wa kurejesha lile baraza la vijana ambalo lilikuwepo na kikapotea. Ni muda ambao tunahitaji kuwashirikisha vijana  wakati dunia inawahitaji vijana. Kama nchi tunatakiwa tuonyeshe kabisa kuwa tunaelekea katika mwelekeo huo. Na katika hilo tunaamini na watu wengi sio wanasiasa viongozi tunaweza tukasema wamekuwa pia wakisema viojana ni taifa la kesho lakini ushirikishwaji huo uko wapi? Tufanye hivi vitu kwa vitendo , leo nimeweza kusema kwamba maneno yanaonekana ni bei nafuu sana lakini vitendo ni bei ghali sana kwa hiyo ni muda sasa tuweze kuvifanyia kazi tunavyovizungumzia.”