Utumaji fedha kutoka ughaibuni waongezeka licha ya COVID-19

Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa  jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote
Picha-IFAD
Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote

Utumaji fedha kutoka ughaibuni waongezeka licha ya COVID-19

Ukuaji wa Kiuchumi

Kiwango cha utumaji fedha kwenda nchi za kipato cha chini na kati kinatarajiwa kuwa kimeongezeka kwa asilimia 7.3 na kufikia dola bilioni 589 mwaka huu wa 2021 tofauti na ilivyokadiriwa awali kutokana na hofu ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Taarifa ya Benki ya Dunia iliyotolewa leo jijini Washington DC nchini Marekani imesema ongezeko hilo ni mwendelezo wa mnepo uliojitokeza mwaka 2020 COVID-19 ilipoanza ambapo kiwango kilipungua kidogo tu kwa asilimia 1.7.

Makadirio hayo kutoka kitengo cha Benki ya Dunia cha Uhamiaji na Maendeleo yanaonesha kuwa kwa mwaka wa pili mfululizo utumaji wa fedha kwa nchi za kipato cha chini na kati isipokuwa China, unatarajiwa kuzidi kiwango cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, FDI na misaada ya kimataifa ya maendeleo, ODA.

Afisa wa Benki ya Dunia Michal Rutkowski anasema taswira hiyo inadhihirisha umuhimu wa fedha zinazotumwa katika kusongesha maisha na kusaidia huduma muhimu kama chakula, afya na elimu wakati wa hali ngumu ya kiuchumi katika nchi watokako wahamiaji.

"Fedha watumazo wahamiaji zimekuwa nyongeza ya fedha ambazo serikali hupatia kaya ili kujikwamua wakati wa hali ngumu ya uchumi wakati wa janga la COVID-19. Kwa hiyo serikali zinapaswa kupatia kipaumbele marekebisho ya sera za kurahisisha utumaji fedha kama njia mojawapo ya kusaidia kujikwamua kutoka janga la Corona," amesema Bwana Rutkowski.

Ongezeko la utumaji fedha limetokana na azma ya wahamiaji wenyewe kutaka kusaidia familia zao wakati wa shida sambamba na kukwamuka kwa uchumi Ulaya na Marekani kulikochochewa na hatua za kupatia fedha kaya zinazohitaji na usaidizi kwenye ajira.

Gharama za kutuma fedha ni kubwa ambapo kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara mtumaji analipa asilimia 8 ya fedha atumayo na gharama inakuwa kubwa zaidi fedha inapotumwa kupitia benki kuliko majukwaa ya kidijitali.

Soma kwa kina taarifa hiyo hapa.