Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi si chaguo ni lazima:WHO

Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi
PAHO/WHO
Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi

Kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi si chaguo ni lazima:WHO

Afya

Leo ni siku ya kuchukua hatua kwa ajili ya kutokomeza saratani ya shingo ya uzazi. Kukiwa na wanawake zaidi ya 300,000 wanaokufa kila mwaka kutokana na saratani ya shingo ya uzazi shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linaungana na wadau kutoka kila pembe ya dunia kuadhimisha siku hii muhimu. 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema mwaka jana pekee, ni asilimia 13 tu ya watoto wa kike wenye umri wa miaka 9 hadi 14 duniani walipewa chanjo dhidi ya virusi vinayovabisha saratani hiyo, au HPV .  

Katika kampeni ya kimataifa ya kutokomeza saratani hii mkuu huyo wa WHO ameungana na watu mbalimbali mashuhuri, wake za marais, manusura wa saratani hiyo na jumuiya za mashirika na wadau wa afya. 

Nyenzo tunazo kutokomeza gonjwa hili 

Washiriki wa hafla hiyo inayofanyika mjini Geneva Uswis moja kwa moja na kwa njia ya mtandao wamezungumzia kuhusu ukosefu wa usawa katika kupata nyenzo na matibabu ya kuokoa maisha, sawa na kile kinachoendelea ktokea wakati huu wa janga la COVID-19, lakini pia wameangazia mafanikio mapya katika kuzuia na matibabu ya saratani hiyo. 

Dkt. Tedros amesema "Saratani ya shingo ya kizazi husababisha mateso makubwa, lakini inaweza kuzuilika kabisa na, ikiwa itagunduliwa mapema, ni moja ya saratani zinazoweza kutibika. Tuna nyenzo za kuweka historia ya saratani ya shingo ya kizazi, lakini ikiwa tu tutawezesha znyenzo hizo kupatikana kwa kila mtu anayehitaji. Pamoja na washirika wetu katika mpango wa WHO wa kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi hilo ndilo tunalenga kulifanya.” 

Ameongeza kuwa saratani ya shingo ya kizazi ni saratani aina ya nne inayowaathiri sana wanawake, na takriban visa vyote vinahusishwa na kuambukizwa nvirusi vya (HPV), virusi vya kawaida sana vinavyoambukizwa kwa njia ya ngono. 

Wahudumu wa afya ni kiungo muhimu katika kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi
Pan American Health Organization
Wahudumu wa afya ni kiungo muhimu katika kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi

Mapengo katika fursa za king ana tiba 

WHO imeonya kwamba wanawake na wasichana katika nchi masikini wanakosa fursa za kupata vituo vya kwenda kupimwa virusi hivyo, chanjo ya HPV na matibabu. 

Akisistiza hilo Dkt. Tedros ameeleza kuwa katika miaka 10 iliyopita, watengenezaji wameelekeza nguvu ya usambazaji wa chanjo ya kupambana na ugonjwa huo katika maeneo tajiri zaidi ndio maana takriban nchi 80 ambazo ndio zina jumla ya theluthi mbili ya mzigo wa saratani ya shingo ya kizazi duniani bado hazijaanzisha chanjo hii ya kuokoa maisha.

Amesema “Kama ilivyo katika janga la COVID-19 pengo katika kiwango cha vifo ni dhahiri vifo 9 kati ya 10 vinatokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati. 

WHO imezipongeza nchi ambazo tayari zimechukua hatua kukabiliana na saratani ya shingo ya kizazi wakati wa janga la COVID-19.” 

Kwani shirika hilo limesema wakati wa COVID-19 kumekuwa na changamoto kubwa hasa watu kuweza kupimwa na idadi ya waliopata huduma imepungua. 
Utafiti wa karibuni uliofanywa katika nchi 155 umebaini kuwa asilimia 43 ya nchi hizo zimeripoti usumbufu wa matibabu kwa kipindi hiki. 
Kiwango cha kimataifa cha chanjo ya HPV pia kimeshuka kutoka asilimia 19 mwaka 2019 hadi asilimia 13 mwaka jana. 

Mustakbali wa saratani hiyo 

WHO imeelezea mafanikio mapya katika kuzuia na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi, kama vile idhinisho la awali la chanjo ya nne ya HPV, ambayo inatarajiwa kuongeza na kubadilisha usambazaji wa chanjo hiyo. 

Mapendekezo mapya ya muongozo wa utafiti katika teknolojia ya uchunguzi wa kutumia akili bandia pia yametolewa, ambayo yatasaidia kuhakikisha kwamba wanapata saratani wanagunduliwa mapema iwezekanavyo. 

Shirika hilo pia limetangaza kituo cha kwanza cha WHO cha ushirikiano kwa ajili ya kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi, kilichopo katika chuo kikuu cha Miami nchini Marekani, ambacho kitakuwa muhimu kwa utafiti na usaidizi wa kiufundi.