Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujenga mnepo katika sekta ya utalii ni muhimu ili kuhimili majanga kama COVID-19: UN

Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha  Wanyamapori Trust nchini Kenya.
UNEP/Natalia Mroz
Tembo yatima aliyeokolewa huko David Sheldrick kituo cha Wanyamapori Trust nchini Kenya.

Kujenga mnepo katika sekta ya utalii ni muhimu ili kuhimili majanga kama COVID-19: UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Leo ni siku ya mnepo katika sekta ya utalii duniani, Umoja wa Mataifa unahimiza umuhimu wa sekta hiyo ambayo ni chanzo cha kipato na ajira kwa mamilioni ya watu inayoajiri mamilioni ya watu na kuwa na mnepo ili kuhimili mishtuko na majanga makubwa kama COVID-19.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa nchi nyingi zikiwemo zenye maendeleo duni, mataifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea, nchi za Afrika na nchi za kipato cha kati “utalii ni chanzo kikuu cha uchumi, pato la nje, kodi na ajira.” 

Na kwa sababu utalii unaunganisha watu na asili, Umoja wa Mataifa unasema utalii endelevu una uwezo wa kipekee wa kujagiza jukumu la kulind na kuhifadhi mazingira.  

Umoja huo umeongeza kuwa “zahma yoyote inapoikumba sekta ya utalii basi inasambaratisha na kupindua maisha ya nchi na ya mamilioni ya watu mathalani lilipozuka janga la COVID-19, sekta ya utalii imekuwa moja ya sekyta ambazo zimeathirika vibaya.” 

Na pigo kubwa zidi limeshuhudiwa katika nchi za visiwa vidogo zinazoendelea ambako utalii unachangia zaidi ya asilimia 20 ya pato la taifa GDP na asilimia zaidi ya 30 ya palo la jumla la nje. 

Duniani kote Umoja wa Mataifa unasema “sekta ya utalii inasaidia ajira kwa mamilioni ya wat umoja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja hususani kwa wanawake na vijana na ndio maana mwaka 2020 takriban ajira milioni 120 za moja kwa moja kwenye sekta ya utalii zilikuwa hatarini kutokana na janga la COVID-19.” 

Hata hivyo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la utalii duniani UNWTO kuna habari njema kwani “mwaka huu wa 2023 utalii wa kimataifa unatarajiwa kuongezeka na kufikia asilimia 80 hadi 95 ya ilivyokuwa kabla ya janga la COVID-19 kutegemeana na kiwango cha kudorora kwa uchumi, kujikwamua kwa safari za kimataifa Asia na Pasifiki na mwenendo wa vita ya Urusi dhidi ya Ukraine miongoni mwa sababu zingine.” 

Takwimu za UNWTO zinaonyesha kuwa “mwaka jana 2022 zaidi ya watalii milioni 900 walisafiri kimataifa idadi ambayo ni mara mbili ya ilivyokuwa mwaka 2021.” 

Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa sekta ya utalii endelevu na wenye mnepo unachangia katika ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu kwa ukuzaji wa uchumi, kupunguza umasikini , kuzalisha ajira na kazi zenye staha kwa wote. 

Pamoja na kujenga mnepo lengo lingine kubwa la siku hii “ni kutoa wito kwa nchi wanachama kuunda mikakati ya kitaifa kwa kujikwamua baada ya majanga ikiwemo kupitia ushirikiano na sekta binafsi na kupanua wigo wa shughuli za sekta hiyo na bidhaa zake.”