Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Huduma ya kubadilisha fedha ni muhimu hususan kwa familia zinazo tegemea kutumiwa fedha na ndugu na jamaa waishio nje ya nchi walizopo

Punguzeni Gharama ya utumaji fedha:Guterres

UN Photo/Stuart Price
Huduma ya kubadilisha fedha ni muhimu hususan kwa familia zinazo tegemea kutumiwa fedha na ndugu na jamaa waishio nje ya nchi walizopo

Punguzeni Gharama ya utumaji fedha:Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

“Nawasihi wadau wote kuendelea na juhudi za kupunguza gharama za kuhamisha fedha duniani, gharama hizo zipungue na hata zikaribia sifuri, maana hii ni huduma muhimu sana, hasa kwa nchi zinazoendelea.”

Kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyoitoa leo jijini New York Marekani katika ujumbe wake ikiwa dunia inaadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa ya utumianaji fedha kifamilia.


Amesema janga la ugonjwa Corona au COVID-19 lilipoikumba dunia mwaka 2019, watu wengi walikuwa na wasiwasi juu ya utumaji wa miamala ya fedha kwa kuwa huduma nyingi za kifedha nyingi zilifungwa.
“Kwa bahati nzuri, utumianaji fedha duniani umeonesha uimara wake na wa kutegemewa kuliko tulivyofikiria. Takwimu za hivi karibuni kutoka Benki ya Dunia, zimebainisha utumaji fedha kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati imefikia dola Bilioni 540 kwa mwaka 2020, ikiwa ni upungufu wa asilimia 1.6 pekee ikilinganishwa na mwaka 2019.”


Guterres amesema kuna sababu nyingi zilizosababisha eneo hilo la kutuma fedha lisiathirike sana lakini sababu kubwa ni wahamiaji wameweka maslahi ya familia zao mbele kuliko matumizi yao wenyewe, pamoja na tabia ya utunzaji wa fedha.  Pia ameeleza hatua za kifedha zilizo chukuliwa na nchi hizo walizopo wahamiaji zimesaidia kuwawezesha kutuma fedha nyumbani.


Akimalizia ujumbe wake wa siku hii amezikumbusha nchi zote duniani wakati wa kupanga mipango yake ya siku za usoni, kuhakikisha wanawasaidia na kuwalinda wahamiaji kwani wameonesha umuhimu wao mkubwa wakati wa kukabiliana na janga la Corona kwa kuhakikisha wanaendeleza utoaji wa huduma muhimu.
 Pia amesema utoaji wa chanjo ya Corona ufanyike bila ya kuangalia iwapo wahamiaji hao wana nyaraka zote za kuwapa kibali cha kuishi katika nchi hizo.