Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dereva wa teksi asaidia kuzuia kusambaa kwa COVID-19 nchini Ghana

Daniel Jordan, dereva wa Uber huko Ashanti nchini Ghana anahakikisha anajilinda yeye na abiria wake dhidi ya janga la COVID-19
WHO/Africa
Daniel Jordan, dereva wa Uber huko Ashanti nchini Ghana anahakikisha anajilinda yeye na abiria wake dhidi ya janga la COVID-19

Dereva wa teksi asaidia kuzuia kusambaa kwa COVID-19 nchini Ghana

Afya

Ni Jumatatu asubuhi, mvua inanyesha mjini Kumasi, mji mkuu wa eneo la Ashanti nchini Ghana. Madereva wengine wametumia fursa hiyo ya mvua ya asubuhi kufanya kazi kutokana na watu wengi kutaka huduma ya teksi.

Daniel Jordan, dereva wa teksi kupitia kampuni ya Uber amemfikisha abiria wake kituo anachotaka na papo hapo anapokea simu nyingine ya ombi la kumbeba abiria mwingine aliye karibu.

Wakiwa wanaelewa vyema kuhusu janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, na madhara yake, Daniel anajihami kwa barakoa na ana nyingine za ziada, chupa ya kitakasa mikono na vitambaa vya kutakasa kwa abiria.

Kitu kingine kilicho ndani ya gari la Daniel aina ya Toyota Vitz, ni kadi ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO yenye maelekezo jinsi ya kutumia usafiri wa umma  wakati wa janga la COVID-19, kadi inayoning’inia kwenye kioo cha dereva ili abiria wote wapate kusoma na kijifunza kuhusu usalama wao.

Mwandishi wa makala hii kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika anaeleza kuwa amegundua madereva wengi wanaotoa huduma kwa umma hawafuati kanuni za usalama za kujikinga na COVID-19 na ndipo akamuuliza Daniel maswali yafuatayo:

Mbona umeamua kuwa tofauti?

Kila siku, tunasikia watu wanakufa kutoka na COVID-19 kwa hiyo niliamua kusikiliza ushauri kutoka kwa wataalamu kupitia vyombo vya habari  na kuhakikisha kuwa hakuna mtu ataambukizwa COVID-19 anapotumia gari langu. Kwa hiyo ninahakikisha kuwa abiria wangu wote wamevaa barakoa zao na wametakasa mikono kabla ya kuingia.

Mwanaume mwenye umri wa miaka 76 mkazi wa Kasoa nchini Ghana akionesha kadi yake ya chanjo dhidi ya COVID-19
© UNICEF/Francis Kokoroko
Mwanaume mwenye umri wa miaka 76 mkazi wa Kasoa nchini Ghana akionesha kadi yake ya chanjo dhidi ya COVID-19

Umepata chanjo?

Naam. Nimepata chanjo zote mbili. Ninahakikisha pia kuwa ninawashauri abiria wanaotumia gari langu kuchanjwa.

Umeshawahi kuambukizwa COVID-19 au una jamaa wa karibu ambaye ameambukizwa ugonjwa huo?
Sijaambukizwa lakini rafiki yangu aliambukizwa na ingawa alipona alipitia machungu mengi kwa sababu alikuwa mgonjwa sana. Ndipo nikagundua kuwa COVID-19 ipo.

Licha kuwa kampuni za teksi ambazo abiria wanaweza kutumia pamoja usafiri mmoja zinafanya juhudi ya kutekeleza kanunii za afya za COVID-19, hata wakati wa kuomba teksi, madereva wengi hawafanyi jitihada za kufuata kanuni hizo baada ya kuwabeba abiria. Katika mtandao wake kampuni ya Uber inasema kampuni inawashauri abiria kujilinda.

Una ujumbe gani kwa madereva wenzako?

Nashindwa kuelewa pale baadhi ya marafiki zangu  wanasema kuwa tunapiga kelele sana kuhusu COVID-19  au tunawasumbua. Kwangu,wao ndio wanajisumbua, kwa sababu kama madereva pia tuko katika hatari na ikiwa tutaendelea kupuuza ushauri tutajipata kwenye hatari kubwa.

Ujumbe wako kwa umma ni upi?

COVID-19 ipo. Sitaki kufa, wala sitaki yeyote afe au aonyeshe dalili kwa hivyo ninawashauri wananchi wenzangu wa Ghana wote wachukue chanjo wakati watapa fursa na pia waendelee kufuata kanunua za afya. Nitafanya wajibu wangu hivyo kila mmoja naye afanye wake.

Katika eneo ambapo ufuatiliaji wa kanuni za COVID-19 umelegea, maafisa wa afya ya umma na washika dau wengine warudi mezani kupanga mikakati kuhusu njia muafaka ya kukabiliana na hali ya kuchoka katika utekelezaji wa kanuni za afya.