Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa GAVI kuwezesha chanjo ya Malaria kupatikana zaidi Afrika- WHO

Clara Magalasi kutoka maeneo ya kijijini ya mji mkuu wa Malawi, Lilongwe alitembea kilometa 4 kuhakikisha mtoto wake Grace mwenye umri wa miezi 22 anapata dozi yake ya nne na ya mwisho ya chanjo ya Malaria.
WHO Malawi
Clara Magalasi kutoka maeneo ya kijijini ya mji mkuu wa Malawi, Lilongwe alitembea kilometa 4 kuhakikisha mtoto wake Grace mwenye umri wa miezi 22 anapata dozi yake ya nne na ya mwisho ya chanjo ya Malaria.

Mpango wa GAVI kuwezesha chanjo ya Malaria kupatikana zaidi Afrika- WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika, limekaribisha uzinduzi uliofanywa na ubia wa chanjo duniani, GAVI wa fursa kwa nchi kuwasilisha maombi ya fedha ili kuanza kusambaza chanjo dhidi ya Malaria, hatua ambao WHO imesema itawezesha chanjo hiyo kufikia watoto walio hatarini zaidi kwa kuanzia na Ghana, Kenya na Malawi, ambazo tayari zilianza majaribio ya chanjo hiyo mwaka 2019 na hatimaye kusambazwa nchi zingine ambako Malaria imeota mizizi.

Taarifa ya WHO Kanda ya Afrika iliyotolewa leo mjini Brazaville, Congo imesema Malaria unasalia sababu kuu ya magonjwa na vifo miongoni mwa watoto katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Mwaka 2020 takribani watoto laki 5 barani Afrika walikufa kwa Malaria. Mtoto mmoja hufariki dunia kila dakika moja kwenye eneo la Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara.

Usaidizi huo wa kimataifa utatenga dola milioni 160 kati ya mwaka huu wa 2022 hadi 2025 ili kuwezesha ongezeko la upatikanaji wa chanjo ya Malaria kwenye maeneo hatarishi zaidi Afrika.

Hatua ya GAVI inatusogeza kufikia watoto wengi zaidi

Mkurugenzi wa WHO  kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema, “fungu jipya la fedha kutoka GAVI linatusogeza hatua mbele zaidi kukaribia mamilioni ya watoto barani Afrika na chanjo  hiyo ya Malaria , RTS, S. Wakati wote wa janga la COVID-19, pindi vituo vya huduma za afya vilipokumbwa na changamoto, wazazi na walezi waliendelea kwa umakini kupeleka watoto wao ili wapate chanjo dhidi ya Malaria. Wanafahamu fika kwamba watoto wanakufa kila siku kwa Malaria na wako makini kulinda watoto wao dhidi ya ugonjwa huo hatari.”

Kufuatia pendekezo la WHO la mwezi Oktoba mwaka 2021 juu ya kusambaza matumizi ya chanjo ya Malaria, miongoni mwa watoto katika maeneo ambako maambukizi yameshamiri, mataifa mengi ambako Malaria imejikita, yaliwasilisha ombi la kupata chanjo hiyo na WHO inasema ni matumaini yake kuwa yatawasilisha rasmi maombi huko GAVI ili kunufaika na taarifa ya leo.

Chanjo hii ya Malaria aina ya RTS, S inazuia vimelea vya Malaria aina ya Plasmodium Falciparum, kimelea ambacho ni hatari zaidi na kinapatikana zaidi barani Afrika.

Watoto nchini Kenya ambao ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya malaria.
GAVI
Watoto nchini Kenya ambao ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya malaria.

Chanjo imeonesha ufanisi kule ambako tayari inatumika

Kule ambako chanjo hiyo imeanza kutolewa kwa watoto, kumekuweko na kupungua kwa kiwango kikubwa cha idadi ya watoto wanaokwenda hospitali na kulazwa kwa kuugua Malaria, sambamba na vifo vya Malaria.

GAVI imedokeza kuwa muda wa mwisho wa maombi ya awali ya kupatiwa msaada huo ambao ni mwezi Septemba mwaka huu wa 2022 ni kwa nchi ambazo tayari zinatumia chanjo hiyo. 

Dirisha la pili la maombi lililo wazi kwa mataifa mengine yanayokidhi vigezo litafungwa mwezi Januari mwaka 2023.