Kulikoni baadhi ya chanjo zitumike kama kizuizi cha kuingia nchi nyingine?

22 Septemba 2021

Rais wa Ghana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo amehutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 na kusema kuwa kitendo cha matumizi ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kama kigezo cha uhamiaji kitarudisha nyuma harakati za kupambana na janga hilo.
 

Ametoa kauli hiyo akizingatia ripoti ya kwamba baadhi ya nchi zinazuia  watu waliochomwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 aina ya AstraZeneca iliyotengenezwa India kuingia kwenye nchi hizo akisema, “jambo hili linashangaza sana.”

“Na kinachoshangaza ni kwamba chanjo hizi zilisambazwa barani Afrika kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa COVAX wa kusaka na kusambaza chanjo za COVID-19,” amesema Rais Akufo-Addo akitaka kitendo cha kuzuia watu waliochanjwa AstraZeneca ya India kikome.

Mafunzo kutokana na COVID-19: Ushirikiano mpya wa kimataifa

Rais huyo wa Ghana akamulika ushirikiano wa kimataifa na janga la COVID-19 akisema kuwa, “ Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Fedha duniani, IMF vyote vilianzishwa ili kusaidia kujenga amani na usalama duniani, kujenga uchumi baada ya vita na kusongesha ushirikiano duniani. dunia bora, endelevu, yenye amani na maendeleo. Lakini hata kabla ya COVID-19 watu wengi walithibitisha kuwa mfumo wa ushirikiano duniani ulioanzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita haukuwa na uwezo wa kutosha kufadhili miundombinu na maendeleo katika nchi zinazoendelea,” amesema Rais Akufo- Addo.

Mwanamke akipata chanjo ya COVID-19 hospitalini katika mji wa Kumasi, Ghana
© UNICEF/Apagnawen Annankra
Mwanamke akipata chanjo ya COVID-19 hospitalini katika mji wa Kumasi, Ghana

Ni kwa mantiki hiyo amesema kutokana na udhaifu wa mfumo wa ufadhili duniani kutoa fedha za kutosha katika kufadhili malengo ya maendeleo endelevu, SDGs tunhitaji tathmini yenye manufaa ya mfumo wa ushirikiaon duniani. 

“Janga la COVID-19 linatoa fursa mpya ya kufikiria ushirikiano wa kimataifa kwa kuzingatia misingi ya urafiki, ustawi wa Pamoja, usawa kama ilivyowekwa bayan ana SDGs,” amefafanua Rais huyo wa Ghana.

Ametanabaisha kuwa iwapo mkutano uliofanyika San Franscico mwaka 1946 kuanzisha Umoja wa Mataifa ungalifanyika leo, basi kungalikuwepo na Katiba tofauti kabisa ya Umoja wa Mataifa ambayo ingaliandikwa. Halikadhalika Benki ya Dunia ,IMF na WHO za vilivyoundwa wakati huo baada ya Vita Kuu ya Pili ya dunia vingalikuwa tofauti kabisa iwapo vingaliundwa leo kwa kuwa nchi za Afrika na Karibea hazikuweko kwenye mkutano huo wakati huo.

Sayansi na Teknolojia bado zina safari ndefu kumuelewa binadamu

Rais huyo wa Ghana akatumia pia hotuba yake kusema kuwa ingawa kuna maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani, bado kuna safari ndefu ya maendeleo hayo kutambua vyema mwili wa binadamu na maisha.

“Janga la COVID-19 lilipoanza, ilielezwa kuwa maiti za waliokufa kwa ugonjwa huo wa Corona zitatapakaa barabarani, lakini ingawa hatukuwa na chanjo nyingi kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine na licha ya vifo na wagonjwa bado hilo lililotabiriwa halikutokea.”

Hata hivyo amependekeza kuwepo kwa ufadhili wa kutosha kwa WHO ili kuweza kufadhili sekta ya afya ya umma duniani, halikadhalika kuweka vyanzo endelevu vya fedha ili kukwamuka kutoka COVID-19 kuwe endelevu na bora.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter