Ghana yawa nchi ya kwanza duniani kupokea chanjo za COVID-19 kupitia COVAX

24 Februari 2021

Baada ya mwaka mzima wa mvurugano wa maisha uliosababishwa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, huku waghana zaidi ya 80,700 wakiambukizwa ugonjwa huo na zaidi ya 580 kufariki dunia, hatimaye mwelekeo wa kuondokana na janga hilo umeonekana.

Hiyo ni kauli ya mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Ghana, Dkt. Francis Kasolo aliyoitoa hii leo punde tu baada ya shehena ya kwanza ya chanjo aina ya AstraZeneca / Oxford zilizotolewa kupitia mfumo wa COVAX kuwasili nchini humo.

"Chanjo hizo 600,000 ni sehemu ya mpango wa awali ya kusambaza chanjo kupitia mfumo wa COVAX na zimetokana na leseni kwa taasisi ya Serum ya India na inawakilisha awamu ya kwanza ya chanjo za COVID-19 zinazoelekezwa nchi za kipato cha chini na kati," amesema Dkt. Kasolo.

Ghana inakuwa nchi ya kwanza duniani na barani Afrika kupokea chanjo hizo kupitia mfumo wa COVAX ambao unajumuisha Umoja wa Mataifa na wadau katika kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa kila mtu na kwa gharama nafuu.

Dkt. Kasolo amesema leo ni wakati wa kihistoria kwa kuwa inaashiria kumalizika kwa janga hilo katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Njia pekee ya kuondokana na janga hili ni kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa kila mtu popote aliko. Tunashukuru wadau wote wanaounga mkono COVAX katika kusambaza chanjo salama dhidi ya COVID-19 kwa haraka na kwa haki."

Kuwasili kwa shehena hiyo pia ni mwanzo wa kile kinachopaswa kuwa operesheni kubwa zaidi ya kusambaza chanjo duniani. Mfumo wa COVAX unapanga kusambaza takribani chanjo bilioni 2 za chanjo dhidi ya COVID-19 mwaka huu pekee na ni hatua ya kipekee duniani katika harakati za kuahkikisha kila mkazi wa dunia anapata chanjo.

Mwakilishi huyo wa UNICEF amesema kuwa wanashukuru kuwa Ghana imekuwa nchi ya kwanza duniani kupata chanjo kupitia mfumo wa COVAX, "tunapongeza serikali ya Ghana hususan wizara ya Afya na wizara ya Habari kwa juhudi zao za kulinda raia."

Halikadhalika amesisitiza kuwa timu ya Umoja wa Mataifa nchini Ghana pamoja na UNICEF na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO wataendelea kuunga mkono kampeni za chanjo na kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona, kwa kushirikiana na wadau kama vile fuko la chanjo duniani, GAVI na ubia wa ubunifu wa kujiandaa dhidi ya milipuko, CEPI.

Ametamatasha taarifa yake akisema kuwa chanjo zinaokoa maisha. "Wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine wa mstari wa mbele wanapopatiwa chanjo, sote taratibu tutaanza kurejea katika maisha ya kawaida ikiwemo kupata huduma bora za afya, elimu na ulinzi kwa wote. Na kwa kuzingatia azma yetu ya Huduma ya Afya kwa Wote na hivyo tusimwache yeyote nyuma."

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter