Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabaharia watambuliwe kuwa wafanyakazi walio mstari wa mbele- UN

Nahodha akiendesha meli ya Wakala wa Rasilimali za Uvuvi ya Korea iliyo na miundombinu chini ya bahari ambayo inakusudia kurejesha rasilimali za uvuvi na kuunda mazingira endelevu.
International Maritime Organization
Nahodha akiendesha meli ya Wakala wa Rasilimali za Uvuvi ya Korea iliyo na miundombinu chini ya bahari ambayo inakusudia kurejesha rasilimali za uvuvi na kuunda mazingira endelevu.

Mabaharia watambuliwe kuwa wafanyakazi walio mstari wa mbele- UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya sekta ya bahari , janga la corona au COVID-19 limethibitisha umuhimu wa bahari na kujitolea kwa mamilioni ya mabaharia wanaofanyakazi katika sekta hiyo amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Guterres amesema “Usafiri wa bahari umeendelea kusafirisha zaidi ya asilimia 80 ya biashara duniani ikiwemo bidhaa muhimu za kitabibu, chakula na bidhaa nyingine za msingi kwa ajili ya kukabiliana na kujikwamua na janga la corona au COVID-19, lakini maelfu kwa maelfu ya mabaharia wanakabiliwa na mgogoro wa kibinadamu baada ya kukwama baharini, wakishindwa kutoka kwenye meli zao huku mikataba yao ikiongezewa muda zaidi wa kusalia melini.”  

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba hali hiyo inapaswa kushughulikiwa haraka kwa serikali kuwatenga mabaharia kama wahudumu muhimu na kuhakikisha waliokwama baharini wanabadilishwa kwa njia salama akiongeza kwamba  
“Ninasisitiza ombi langu kwa serikali kushughulikia shida yao kwa kuwachagua rasmi mabaharia na wafanyikazi wengine wa baharini kama wafanyikazi muhimu, kuhakikisha mabadiliko ya wafanyikazi kwa njia salama, kutekeleza itifaki zilizowekwa, na kuruhusu mabaharia waliokwama kurudishwa nyumbani na wengine kujiunga melini. " 

Maudhui ya siku ya mwaka huu ni “Mabaharia katika kitovu cha usafirishaji siku zijazo” na lengo lake ni kuelimisha kuhusu jukumu muhimu la mabaharia katika biashara duniani na kuongeza ufahamu wa kazi zao.”

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la masuala ya bahari IMO janga la COVID-19 mwaka jana 2020 limedhihirisha mchango wa mabaharia kama wahudumu muhimu walio msitari wa mbele katika kuhakikisha bidhaa muhimu zinafika kwa wakati wakati wa janga hili na wakati mwingine wote. 

Limeongeza kuwa usafiri wa kimataifa wa njia ya bahari husafirisha zaidi ya asilimia 80 ya biashara duniani kwa watu na jamii kote duniani.