Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kimataifa yataka mabaharia na wahudumu wa ndege kupewe kipaumbele cha chanjo ya COVID-19

UN inataka mabaharia na wahudumu wa ndege kuchukuliwa kama wahudumu wa msitari wa mbele na hivyo kupewa kipaumbele katika chanjo ya COVID-19
IMO/Hedi Marzougui
UN inataka mabaharia na wahudumu wa ndege kuchukuliwa kama wahudumu wa msitari wa mbele na hivyo kupewa kipaumbele katika chanjo ya COVID-19

Mashirika ya kimataifa yataka mabaharia na wahudumu wa ndege kupewe kipaumbele cha chanjo ya COVID-19

Afya

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na mashirika ya kimataifa imetoa wito kwa mabahatria na wahudumu wa ndege kuchukuliwa kama ni watoa huduma walio msitari wa mbele na hivyo kupewa kipaumbele katika chanjo dhidi ya corona au COVID-19.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya pamoja ya shirika la usafiri wa anga ICAO, shirika la Umoja wa Mataifa afya duniani WHO, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, shirika la kimataifa la usafiri wa majini IMO na shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO janga la COVID-19 limesababisha athari mbaya kwa maisha ya binadamu na uchumi wa dunis na usafiri wa baharini na angani ni njyanja mbili muhimu ambazo zinategemewa na biashara ya kimataifa na uhamaji na ni kitovu cha ujikwamuaji endelevu wa kijamii na kiuchumi.

Taarifa imeongeza kuwa zaidi ya asillimia 80% ya biashara ya ulimwengu kwa kiasi huhamishwa na usafirishaji wa baharini. 
Uchumi wa ulimwengu unategemea mabaharia milioni 2 wadunia ambao wanaendesha meli za kibiashara duniani. 

Mabaharia wameathiriwa sana na vizuizi vya kusafiri vilivyowekwa wakati wa janga la COVID-19 na tangu Januari 2021, inakadiriwa kuwa mabaharia wengine 400,000 wamekwama kwenye meli za kibiashara, kwa muda mrefu wakati mikataba yao imeshamalizika na hawawezi kusafirishwa huku idadfi kama hiyo ya mabaharia wanahitaji haraka kujiunga na meli hilo ili kuzibadilishana.

Umuhimu wa safari za anga

Kwa upande wa safari za anga , taarifa ya pamoja ya mashirika hayo ya kimataifa imesema usafiri wa anga wa abiria ulibeba abiria wapatao bilioni 5.7 mwaka 2019 wakati ambapo usafirishaji wa ndege unawakilisha 35% ya thamani ya bidhaa zilizosafirishwa kwa njia zote pamoja. 
Idadi ya wataalam wote wa usafiri wa anga walio na leseni, wakiwemo marubani, wadhibiti trafiki wa anga na mafundi wataalamweny leseni ya utunzaji, walikuwa 887,000 mwaka 2019, kulingana na takwimu za wafanyikazi wa ICAO

Lakini utekelezaji wa sheria kali za afya ya umma kwa wafanyikazi wa anga, pamoja na amri ya kusalia majumbani kujikinga na janga la COVID-19, vimesababisha athari kubwa katika utendaji na pia gharama kubwa. Imeongeza taarifa yao.

Usafiri wa ndege za abiria umeshuka kwa asilimia 60 sababu ya janga la COVID-19
Unsplash/Ismail Mohamed - SoviLe
Usafiri wa ndege za abiria umeshuka kwa asilimia 60 sababu ya janga la COVID-19


Umuhimu wa mabaharia na wahudumu wa ndege

Kwa mujibu wa taarifa ya mashirika hayo “usafiri wa baharini na anga hutegemea mabaharia na wafanyikazi wa ndege na kwamba ni wafanyikazi muhimu wanaohitajika kusafiri kuvuka mipaka kila wakati, hali ambayo inaweza kusababisha kuhitaji kuwasilisha uthibitisho wa chanjo ya COVID-19 kama sharti la kuingiua nchi zingine.” 
Hii ni licha ya pendekezo la WHO kwamba, kwa wakati huu, nchi hazipaswi kuanzisha mahitaji ya uthibitisho wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa kusafiri kimataifa kama hali ya kuingia, kwani bado kuna mambo muhimu ambayo hayajulikani kuhusu ufanisi wa chanjo katika kupunguza maambukizi na upatikanaji mdogo wa chanjo hiyo. 
Ili usafirishaji wa njia ya bahari na usafirishaji wa angani uendelee kufanya kazi kwa usalama, harakati salama za mpakani za mabaharia na wafanyakazi wa usafiri wa anga lazima ziwezeshwe. 
“Tunarudia wito wetu kwa nchi ambazo hazijafanya hivyo kuhakikisha inawachukulia mabaharia na wahudumu wa usafiri wa ndege kuwa ni wafanyikazi muhimu na wanastahili kupewa kipaumbele katika kupata chanjo dhidi ya COVID-19.”