Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia ina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 55: Ripoti yao yawasilishwa UN

Kambi ya Al- Hol iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Syria inawakimbizi zaidi ya 60,000 wengi wao wakiwana ni wanawake na watoto wanaoishi katika hali duni
© UNICEF/Delil Souleiman
Kambi ya Al- Hol iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Syria inawakimbizi zaidi ya 60,000 wengi wao wakiwana ni wanawake na watoto wanaoishi katika hali duni

Dunia ina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 55: Ripoti yao yawasilishwa UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Suluhu za kitaifa lazima zipatikane kwa watu zaidi ya milioni 55 waliotawanywa kwenye nchi zao kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na jopo la ngazi ya juu linalojikita na wakimbizi wa ndani. 

Akipokea ripoti hiyo “Kutanabaisha hali ya wakimbizi wa ndani , maono ya mustakbali wao” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Kwa miongo mingi idadi ya wakimbizi wa ndani kote duniani imekuwa ikiongezeka na kufikia kiwango cha juu mwaka baada ya mwaka. Msaada wa kibinadamu ni muhimu kuwasaidia kuweza kuishi. Lakini juhudi zaidi zinahitajika kurejesha hali ya kawaida na kuwapa suluhu ya kudumu.” 

Piga simu ili kuchagiza hatua 

Ili kusaidia mamilioni ya watu waliokwama katika mgogoro wa kutawanywa, ripoti inahimiza mataifa kuchukua "mtazamo unaolenga maendeleo" kwa raia na wakaazi wanaolazimishwa kukimbia majumbani mwao kwa sababu ya vurugu, mizozo, majanga na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Katika kuwasilisha ripoti yake, jopo hilo limezitaka serikali, asasi za kiraia, jamii ya kimataifa na sekta binafsi, kuongeza hatua za pamoja kuelekea mabadiliko ya kimfumo ili kumaliza changamoto ya muda mrefu ya watu kutawanywa. 

Kusaka suluhisho  

Ripoti hiyo ya maono ya siku za usoni inakiri kwamba "kushindwa kwa juhudi za pamoja kuzuia, kushughulikia na kusuluhisha tatizo la wakimbizi wa ndani, lakini pia inabainisha fursa za kubadilisha mbinu na mazoea ambayo yanaweza kumaliza mateso yasiyo ya lazima kwa watu hao.” 

Ripoti imeongeza kuwa, wakimbizi wa ndani au IDPs lazima waweze kutumia haki zao za msingi na wasionekane au kuchukuliwa tu kama wanufaika wa msaada wa muda mfupi. 

Hivi sasa, hawaajajumuishwa kimfumo katika sera za Serikali, fedha za maendeleo, michakato ya amani au mikakati ya Umoja wa Mataifa. 

"Ni kwa faida ya serikali kumiliki suala hili, kwa sababu hawawezi kufikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) bila kuboresha maisha ya wakimbizi wote wa ndani kuanzia wanawake na watoto waliohamishwa hadi wazee," amesema mwenyekiti mwenza wa jopo, Donald Kaberuka. 
Kusaidia mataifa 

Ili kusaidia serikali, jopo hilo limetoa witoo wa kuwepo na uongozi wenye nguvu wa Umoja wa Mataifa kupitia hatua thabiti zaidi za kushughulikia masuala ya kibinadamu, maendeleo, amani, maafa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, yanayochochea watu kukimbia makazi yao. 

Na kuzisaidia serikali kushinda vizuizi hivyo, waandishi wa ripoti pia wamependekeza kwamba kuanzishwe mfuko wa kimataifa wa suluhisho za wakimbizi wa ndani ili kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa mipango na mikakati ya kitaifa. 

"Kwa kuzingatia hali ya sasa ya mizozo na mwenendo wa ukuaji wa miji na mabadiliko ya tabianchi, wakati wa kuchukua hatua ni sasa. Kuendelea na hali ilivyo sasa sio chaguo ", amesema mwenyekiti mwenza wa jopo Federica Mogherini.

Mataifa ya Kusini na Mashariki mwa Afrika yanaendelea kukabiliwa na mafuriko, ukame na matukio mengine ya mabadiliko ya hali ya hewa katika miaka ya karibuni
UNDP/Arjen van de Merwe
Mataifa ya Kusini na Mashariki mwa Afrika yanaendelea kukabiliwa na mafuriko, ukame na matukio mengine ya mabadiliko ya hali ya hewa katika miaka ya karibuni


Masuala mengine muhimu  
 

Ukijulikana kwa mateso makubwa unayowapa binadamu ukimbizi wa ndani ni, moja ya mgogoro unaopuuzwa zaidi ulimwenguni, athari zake za kijamii na kiuchumi zinaweza kusukuma nje zaidi utekelezaji wa malengo ya SDGs. 

Jopo hilo limeguswa na ukosefu wa dhamira ya kisiasa kushughulikia tatizo la wakimbizi wa ndani na kwamba mataifa mengi yameshindwa kukubali au kuwajibika kwa raia wao na wakaazi wao. 

Kwa kuongezea, Umoja wa Mataifa, nchi wahisani na taasisi za kifedha za kimataifa, zimepuuza kutimiza kiwango cha kujitolea kinachohitajika kumaliza shida hii ya kimataifa. 
Suluhisho huanza na maendeleo 
 
Jopo limetoa wito wa mtazamo unaolenga maendeleo ambao unatoa kipaumbele  kwa suluhu kuanzia ngazi ya mitaa na kitaifa na ambayo ni zaidi ya usaidizi wa kibinadamu. 

Wametaka pia kuwe na uteuzi wa mwakilishi mpya wa Umoja wa Mataifa ambaye atakuwa maalum kwa ajili ya kuendeleza suluhu za changamoto za wakimbizi wa ndani kwa sababu tatizo la wakimbizi wa ndani kimataifa linazidi kuwa baya. 

Na wamemtaka Katibu Mkuu aanzishe bodi ya ushauri ya sekta binafsi, kusaidia kusaka suluhisho kwa tatizo la wakimbizi wa ndani. 

Bwana Guterres sasa atazingatia matokeo ya ripotoi hiyo , na atafakari ripoti hiyo. 

Wakati ari ya kisiasa ya serikali inaweza kutatua au kuathiri mabadiliko, waandishi wa ripoti wanasema kwamba hatua ya pamoja ni muhimu katika miaka ijayo.