Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziara yangu ya kwanza Somalia ni somo - Robert Piper

Msaidizi wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Suluhisho la Wakimbizi wa Ndani Robert Piper akizungumza na mkazi wa makazi ya Barwaqo IDP huko Baidoa, Somalia tarehe 13 Februari 2023.
UN Photo / Ali Bakka
Msaidizi wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Suluhisho la Wakimbizi wa Ndani Robert Piper akizungumza na mkazi wa makazi ya Barwaqo IDP huko Baidoa, Somalia tarehe 13 Februari 2023.

Ziara yangu ya kwanza Somalia ni somo - Robert Piper

Wahamiaji na Wakimbizi

Robert Piper akiwaeleza kwa ufupi wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kimataifa kuhusu nia ya ziara yake anasema, “nimekuja kuwasikiliza Wakimbizi wa Ndani na kuelewa hali zao na kujifunza kutoka kwa familia ya Umoja wa Mataifa na wadau wetu kuhusu jinsi tunavyokuungeni mkono katika changamoto hii.”  

 

Ziara ya Bwana Piper iliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita Jumamosi tarehe 11 hadi juzi tarehe 15 Februari ililenga kuyaelewa masuala yanayoendelea Somalia, pamoja na kuhamasisha kuhusu Ajenda ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimbizi wa ndani. Somalia ni mojawapo ya Nchi 16 Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizochaguliwa kufanya majaribio ya ajenda ya hatua kuhusu ukimbizi wa ndani. 

Soundcloud

Alipotembelea Baidoa, jiji kubwa zaidi katika Jimbo la Kusini Magharibi mwa Somalia, Bwana Piper alikutana na maafisa wa serikali, akiwemo meya wa Baidoa, na kutembelea makazi ya Goorisane 2 na Yarabi kuona jinsi Umoja wa Mataifa na wadau wengine wasio wa kiserikali wanaunga mkono juhudi za serikali kushughulikia mahitaji ya haraka na ya muda mrefu ya jamii zilizofurushwa. Na hapo ndipo alipopata wasaa wa kuzungumza na baadhi ya wakimbizi hao wa ndani wakamweleza hali ilivyo na kwa hakika kwa macho yake akajionea kuwa hali ni mbaya japokuwa kuna hatua ambazo tayari zimepigwa, 

“Tumekaa na wakimbizi wa ndani na kusikiliza simulizi zao.Tumesikia kuhusu baadhi ya maendeleo ambayo yamefanywa. Zaidi ya yote wengi wao wamesema sasa wanajisikia salama. Wale tuliozungumza nao sasa wana hatimiliki ya ardhi wanapoishi ambayo ni maendeleo ya kubadilisha maisha. Ni jambo moja kuwa na nyumba, ni jambo jingine kuhakikisha watu wanapata mahitaji. Ni jambo moja kuwa na kituo cha afya, lakini kinahitaji kuwa kizuri cha kutosha kukidhi mahitaji ya kila mtu saa 24 siku 7 sio tu wakati wa mchana kwa huduma nyepesi za matibabu. Inafedhehesha kutambua ni kiasi gani kuna mengi ya kufanya lakini tunahitaji kuchukua mafunzo kutoka Somalia na kuyatumia kote ulimwenguni." 

Ujumbe unaoongozwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu  Umoja wa Mataifa wa Suluhisho la Wakimbizi wa Ndani Robert Piper ukiwasili katika Kituo cha Rasilimali za Jamii cha Yarabi huko Baidoa, Somalia tarehe 13 Februari 2023.
UN Photo / Ali Bakka
Ujumbe unaoongozwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa wa Suluhisho la Wakimbizi wa Ndani Robert Piper ukiwasili katika Kituo cha Rasilimali za Jamii cha Yarabi huko Baidoa, Somalia tarehe 13 Februari 2023.

Ajenda ya hatua kuhusu wakimbizi wa ndani ambayo ilitolewa mwezi Juni mwaka jana 2022 ina malengo makuu matatu ambayo ni kusaidia wakimbizi wa ndani kupata suluhisho la kudumu la uhamaji wao, uzuiaji bora wa kuibuka kwa majanga mapya, na kuhakikisha kuwa wale wanaokabiliwa na ufurushwaji wanapata ulinzi na usaidizi unaofaa. 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kwa Somalia, miongo kadhaa ya migogoro na ghasia pamoja na ukame wa mara kwa mara ni vichochezi vikuu vya wakimbizi wa ndani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambayo kwa sasa ina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni tatu.