Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imelaani vikali mauaji ya wakimbizi wa ndani 25 Burkina Faso 

Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.

UNHCR imelaani vikali mauaji ya wakimbizi wa ndani 25 Burkina Faso 

Amani na Usalama

 Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limelaani vikali shambulio ambalo limekatili maisha ya wakimbizi wa ndani 25 nchini Burkina Faso. 

Manusura wa shambulio hilo lililofanyika usiku wa Oktoba 4 wamesema watu 25 ambao wote ni wanaume waliuawa na mmoja kujeruhiwa vibaya wakati msafara wao uliokuwa umebeba watu 46 uliposhambuliwa na kundi la watu wenye silaha karibu na Kijiji cha Ouintokoulga katika jimbo la Sanmatenga nchini humo. 

Wanaume hao walitenganishwa kutoka kwenye kundi zima ambalo pia lilikuwa na wanawake na watoto na wakauawa na mmoja wao aliyejeruhiwa vibaya akaachwa. 

Baada ya muda watu hao wenye silaha waliwaachilia wanawake na watoto na kisha watu hao wenye silaha wakakimbia. 

 Loli Kimyaci mwakilishi wa UNHCR nchini Burkina Faso amesema “Tumehudhunishwa sana na kitendo hiki cha kikatili. Raia wasio na hatia wnasaka usalama lakini badala yake wanalipa gharama ya Maisha yao katika kiwango cha kutisha.” 

 Manusura wa shambulio hilo walifanikiwa Pissila mji uliopo kilometa tisa kutoka sehemu la tukio. 

Mshirika wa UNHCR ambaye ni shirika la ICAHD limekuwa likiwapatia manusura hao msaada wa kisaikolojia. 

Shambulio hilo limetokea wakati wakimbizi hao wa ndani walikuwa safarini kurejea majumbani kwao kutoka Pissila wakitumai kuwa hali ya usalama imeimarika. 

Mamia ya watu wameuawa Burkina Faso mwaka huu katika mashambulizi zaidi ya kumi dhidi ya raia. 

Hivi sasa nchi hiyo ya afrika Magharibi ina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 1 kwa sababu ya machafuko yanayoendelea ambayo yamewafanya maelfu ya watu kufungasha virago zaidi ya mara moja hasa katika maeneo ya Kaskazini na Mashariki mwa nchi hiyo.