Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa UNGA76 afunga pazia la mjadala mkuu; asema ushirikiano wa kimataifa ungali hai

Rais wa UNGA76 Abdullah Shahid akifunga mjadala mkuu wa UNGA76 jijini New York, Marekani 27 Septemba 2021
UN/Cia Pak
Rais wa UNGA76 Abdullah Shahid akifunga mjadala mkuu wa UNGA76 jijini New York, Marekani 27 Septemba 2021

Rais wa UNGA76 afunga pazia la mjadala mkuu; asema ushirikiano wa kimataifa ungali hai

Masuala ya UM

Hatimaye mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 umefunga pazia leo Jumatatu katika makao makuu ya Umoja huo jijini New York, Marekani huku Rais wa Baraza hilo Abdullah Shahid akisema mkutano huo umefanyika kwa mafaniko makubwa katikati ya janga la Corona au COVID-19 huku akitaja sababu za mafanikio hayo kuwa ni hatua bora za kupunguza maambukizi na viwango vya juu vya chanjo.
 

Akitoa hotuba ya kufunga mkutano huo ulioanza tarehe 20 na kufikia ukingoni leo kwa njia ya mtandao na ukumbini, Bwana Shahid amesema Umoja wa Mataifa umechukua hatua za kijasiri zaidi za kuibuka kwenye janga la Corona na tunapaswa kutumia mafanikio haya kuendeleza kasi ya sasa.

“Hata hivyo, kipimo sahihi cha mafanikio yetu kinasalia kuwa utayari wet una uwezo wetu wa kushirikiana kwa njia ya mazungumoz na kuweka imani yetu katima ushirikiano wa kimataifa,” amesema Bwana Shahid.

Wanawake 18 tu kati ya wahutubiaji 194

Akichambua mjadala mkuu uliotoa fursa kwa viongozi w anchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhutubia, Bwana Shahid amesema katika kipindi cha wiki nzima kulikuwepo na wazungumzaji 194 waliohutubia wakiwemo marais 100, wakuu wa serikali 52, makamu marais 3 na mawaziri 34.Miongoni mwa viongozi hao wanawake waliohutubia mjadala mkuu wa UNGA76 ni Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

“Naamini mmehamasishwa kama ilivyokuwa kwangu mimi kwa kurejea kwa diplomasia hii,” amesema Rais huyo wa Baraza Kuu akifurahishwa na jinsi ambavyo kumbi za Umoja wa Mataifa na migahawa yake ilijawa na mazungumzo, mijadala, vicheko na maridhiano.

Hata hivyo akitanabaisha kuwa kati ya wahutubiaji 194 wa mwaka huu, wanawake walikuwa ni 18 tu, Bwana Shahid amesisitiza kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa zaidi ili kuweka mizania katika uongozi.
“Nimekuwa na mazungumzo na viongozi wanawake wa nchi na serikali pamoja na Muungano wa Ulaya kuhusu jinsi ya kusongesha usawa wa kijinsia,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani 23 09 2021
UN/Cia Pak
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani 23 09 2021

Hofu zinazojitokeza mara kwa mara

Ingawa masuala mengi yalijadiliwa wiki iliyopita, bado kuna masuala yanayoibuka mara kwa mara kama vile COVID-19, mabadiliko ya tabianchi, amani, usalama na hatari ya kutokuwepo kwa utulivu.

“Suala kwamba kila moja ya mambo hayo yalipatiwa kipaumbele, kuna jambo kubwa kuhusu kile ambacho dunia inataka,” amesema Rais huyo wa Baraza Kuu akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kupatia suluhu shaka na shuku hizo kwa njia ambayo itabadili kila changamoto kuwa fursa, fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuleta matunda bora kwenye jamii .

Amesisitiza kuwa hakuna muda wa kuzubaa kwa kuwa dunia hivi sasa inahitaji hatua zaidi na si pungufu.
Huku vikao vya ngazi ya juu vya COVID-19, tabianchi na mazingira pamoja na uwezeshaji wanawake, wasichana na vijana  vikiwa vimeshapangwa, Bwana Shahid amesema anatarajia ushiriki wa dhati na ujumuishi.

Ukweli na utata katika changamoto na suluhu

Akitamatisha hotuba yake, Bwana Shahid amesema katika mjadala wote kuna mambo mawili yamejitokeza. Mosi kila mtu anakubali juu ya shaka na shuku zinazokumba dunia na ari ya kuondokana na changamoto hivyo.

Hata hivyo kuna tofauti kubwa juu ya njia au mbinu za kuchukua kukabili changamoto hizo.
Pili ni kwamba ushirikiano wa kimataifa bado uko hai na katika hali bora, hali iliyodhihirishwa na kwamba watu wengi wamezungumza na kutoa maazimio akisema ni dalili ya dunia kuendelea kuamini katika mazungumzo na diplomasia, na hiyo ni kuonesha imani kwa Umoja wa Mataifa wenye uwezo na ulio tayari.

Ni kwa mantiki hiyo amesema, “hebu na tupate matumaini kutokana na kweli hizi na tufanye kazi kwa kuwajibika na ari kwa kipindi chote cha UNGA76 kilichobakia.”

UNGA76 itafunga pazia  mwezi Septemba mwaka kesho wa 2022.