Chakula ni uhai, lakini mamilioni ya watu kila siku hulala njaa:Guterres

23 Septemba 2021

Watu bilioni 3 duniani hawawezi kumudu lishe bora, wengine bilioni 2 wana utipwatiwa huku milioni 462 wana uzito mdogo usio stahili, na yote hay ani sababu ya chakula amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Akuzungumza katika mjadala wa wazi wa ngazi ya juu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York Marekani leo ukijadili mifumo ya chakula amekumbusha kwamba “Chakula ni uhai, lakini nchi , jamii na kaya nyingi katika kila kona ya dunia hitaji hili la msingi ambalo ni haki ya binadamu halitimizwi.” 

Ameongeza kuwa kila uchao mamilioni ya watu hulala njaa wakiwemo watoto wakati karibu theluthi moja ya chakula chjote kinachozalishwa hupotea au kutupwa. 

Kwa ,mantiki hiyo amesisitiza “Ni lazima tujenge dunia ambayo lishe bora na yenye virutubisho vyote inapatikana na kwa gharama nafuu kwa kila mt una kila mahali” 

Changamoto zilizopo 

Katibu Mkuu amesema anatambua changamoto inayoikabili dunia na si mpya, lakini janga la corona au COVID-19 limeongeza changamoto hiyo, kupanua pengo la usawa, kusambaratisha uchumi, kuwasukuma mamilioni ya watu zaidi katika umasikini uliokithiri na kuongeza tishio la baa la njaa katika baadhi ya nchi. 

Wakati huohuo amesema dunia iko katika vita na mazingira asilia na kuvuna makapi, kwani mazao yameharibiwa, uchumi umeporomoka na kuna mifumo ya chakula isiyo na ufanisi. 

“Mifumo ya chakula inazalisha theluthi moja ya hewa chafuzi ya viwandani na inahusika na kupotea kwa bayoanuwai kwa hadi asilimia 80” Ameongeza Bwana Guterres. 

Na kwa kulitambua hilo amesisitiza kwamba “Mifumo ya chakula inaweza na ni lazima ibebe jukumu kubwa katika kushughulikia changamoto zote hizi ili kuweza kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030.” 

Amehimiza kwamba nchi wanachama na ushirikiano wa kimataifa ndio vinashika usukani ya kuongoza njia ya kuwa na mifumo ya chakula ambayo inaweza kuikwamua dunia katika njia muhimu tatu, kwa ajili ya watu, kwa ajili ya sayari na kwa ajili ya mafanikio. 

Mkimbizi wa zamani na sasa mshiriki mkulima wa Jumuiya ya Jamii ya Bantu ya Somali huko Lewiston, Maine, huwa na mifugo.
Hazel Plunkett
Mkimbizi wa zamani na sasa mshiriki mkulima wa Jumuiya ya Jamii ya Bantu ya Somali huko Lewiston, Maine, huwa na mifugo.

Njia kuu tatu za kuzingatia 

Amezitaja njia hizo kuu tatu kuwa ni

  1. Mosi:tunahitaji mifumo ya chakula ambayo inasaidia afya na ustawi wa watu wote. Utapiamlo, njaa na baa la njaa sio majanga ya asili ni matokeo ya kuchukua hatua au kutochukua hatua kwetu sote. Natoa wito kwa serikali na wafanyabiashara kushirikiana kuongeza fursa za upatikanaji wa lishe bora ikiwemo kuchagiza hulka mpya mfano kuchagiza chakula bora mashuleni.” 
  2. Pili: Tunahitaji mifumo ya chakula ambayo italinda sayari yetu, kwani inawezekana kulisha idadi ya watu inayoongezeka duniani huku pia tukilinda mazingira yetu. Inahitaji mbinu na suluhu asilia za uzalishaji na ulaji, udhibiti mzuri wa rasilimali kuanzia mashamba hadi sekta ya uvuvi. 
  3. Tatu na mwisho: Tunahitaji mifumo ambayo inaungamkono mafanikio, na si mafanikio ya biashara na wadau tu, bali mafanikio ya wakulimana wafanyakazi wa sekta ya chakula na bila shaka ya mabnilioni ya watu duniani kote ambao wanategemea sekta hii kuweza kuishi, iwe kwa kufanyakazi mashambani, kusafirisha chakula hadi sokoni na katika nyumba zetu. 

Amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa asasi za kiraia kuendelea kupaza sauti ya mabadiliko na pia kujumuisha watu walio kitovu katika mnyororo wa mfumo wa chakula ambao ni familia za wakulima, wafugaji, wafanyakazi, watu wa asili, wanawake na vijana kwani amesema “Chakula ni uhai na chakula ni matumaini, kubadili mifumo ya chakula sio tu kwamba inawezekana, bali ni lazima kwa ajili ya watu, sayari na mafanikio, na huu ndio wakati wetu hebu tufanye kazi kutimiza hilo.” 
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter