Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA76: Yapi yatatamalaki na mambo yatakuwaje?

Wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wanazingatia umbali kati ya mtu na mtu wakati mikutano inayoendelea katika Umoja wa Mataifa
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wajumbe katika ukumbi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wanazingatia umbali kati ya mtu na mtu wakati mikutano inayoendelea katika Umoja wa Mataifa

UNGA76: Yapi yatatamalaki na mambo yatakuwaje?

Masuala ya UM

Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeanza tarehe 14 Septemba, na uko tofauti sana na mkutano wa mwaka jana 2020 ambao wote ulikuwa ni kwa njia ya mtandao.  

UNGA 76 bado inaghubikwa na janga la corona au COVID-19, lakini hiyo haitawazuia viongozi wa dunia ambao wengine watakuwa ana kwa ana katika Ukumbi wa Baraza Kuu kushughulikia changamoto za haraka za ulimwengu. Na haya ndio mambo matano makubwa unayopaswa kuyajua kuhusu mjadala huo "mseto" wa ngazi ya juu mwaka huu wa 2021. 

1)Kuhudhuria ana kwa ana ama la 

Muundo wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu ni(UNGA 76) ni mseto na ni kielelezo cha hali halisi ya ulimwengu wa sasa kuanza kurejea polepole kwenye mikutano ya ana kwa ana, na wajumbe wengine wakisalia kujumuika mtandaoni, lakini pia hamu ya kurudi kwenye maisha ya kawaida  iliyotiwa chachu na kutambua kwamba janga la COVID-19 halijakwisha. 

Kufuatia UNGA ya mwaka jana 2020 iliyofanyika kwa njia ya mtandao, mwaka huu baadhi ya wakuu wa nchi watakuja makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani kutoa hotuba zao kwenye jukwaa la mjadala mkuu, wakati wengi watasalia makwao na kutoa ujumbe wao kupitia njia ya video. 

Moja ya mambo muhimu zaidi ya UNGA kwa wakuu wa Nchi na maafisa wengine wakuu wa serikali, ni fursa ya kushiriki mikutano isiyo rasmi, ya moja kwa moja na wenzao, mbali na kupepesa macho kwenye kioo.  

Fursa hii ilikosekana mwaka jana 2020, lakini mwaka huu 2021 itakuwepo na "vibanda maalum vya faragha vimewekwa

Ingawa bado haijulikani ni viongozi gani wa nchi na serikali watakaojitokeza ana kwa ana katika mkutano wa mwaka huu, ukweli ni kwamba unaweza kufuatilia mjadala huo moja kwa moja kwenye wavuti kuu ya UN News, na kutazama moja kwa moja, kwenye Televisheni ya wavuti ya Umoja wa Mataifa  UN Web TV.

Mgao wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unapaswa kuimarishwa.
© UNICEF/Zoe Mangwinda
Mgao wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unapaswa kuimarishwa.

 2)Chanjo inapewa kipaumbele 

Kuhusu mada ya chanjo ya corona au COVID-19, kaulimbiu ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani (WHO) imekuwa "Hakuna mtu aliye salama hadi pale kila mtu atakapokuwa salamasalama ": kwa maneno mengine, kwa nchi tajiri, ambazo zinafanya maendeleo makubwa katika kuchanja raia wao wengi , zinapaswa kuhakikisha kuwa watu katika nchi maskini pia wanalindwa. 
Lakini, ni wazi kwamba hili halifanyiki, kulingana na Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkuu wa WHO.  

Tarehe 20 Septemba, kama sehemu ya "Wakati wa SDG" kwa ajili ya muongo wa utekelezaji ambao ni msukumo wa Umoja wa Mataifa wa kutoa suluhisho endelevu kwa changamoto kubwa zinazoukabili ulimwengu, Dkt. Tedros atazungumzia hali ya sasa ya kutolewa kwa chanjo, sanjari na Achim Steiner , mkuu wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), na Vera Songwe, ambaye anaongoza tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA). 

Je! BTS watavunja rekodi mtandaoni tena? 

Mkutano huo wa siku nzima utaambatana na tamasha la muziki kutoka kwa kundi maarufu la  Korea ambalo ni Rafiki mkubwa wa Umoja wa Mataifa lijulikanalo kama BTS

Kundi la muziki wa Pop toka Korea  lenye wanamuziki 7 limekuwa likishirikiana na Shirika la  Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF tangu mwaka 2017 kwenye kampeni ya “Kujipenda” ili  kukomesha uonevu, na kukuza kujithamini. 

Timu ya Umoja wa Mataifa bila shaka itakuwa makini wakati tarehe 20 Septemba inakaribia, ikikumbukwa idadi kubwa ya wafuasi wa mtandao wa BTS iliyovutiwa wakati wa ziara yao ya awali kwenye mkutano wa Baraza Kuu mwaka 2018, na wakati ujumbe wao wa video ulipotolewa kwenye mkutano wa Baraza Kuu mwaka jana na matukio yote mawili yakiuacha mtandao umelewa na idadi ya watu.

Mifumo ya chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.
© FAO/Petterik Wiggers
Mifumo ya chakula barani Afrika imevurugwa kwa kiasi kikubwa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hivi karibuni zaidi janga la Corona.

3) Njaa ya mabadiliko: Mapishi ya mifumo mipya ya chakula 

Mwaka uliopita kumekuwa na msukumo mpya kwa Umoja wa Mataifa juu ya hitaji la kubadilisha mifumo ya chakula, inayoelezewa kama kila kitu kinachohusika katika kupata chakula bora na chenye lishe, kuanzia kwenye mazao hadi nyama, na mpaka kwenye sahani zetu. 

Msukumo huu mpya unachagizwa na uamuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuandaa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa wa mifumo ya chakula wa ambao utafanyika tarehe  23 Septemba. 

Wataalam kadhaa wameonya kuwa mfumo wa sasa wa chakula ulimwenguni unaiathiri sayari na idadi ya watu ulimwenguni.  

Akitangaza mkutano huo, Bwana Guterres amesema kuwa mifumo ya chakula ni "moja ya sababu kuu inayotufanya kushindwa kukaa ndani ya mipaka ya ikolojia ya sayari yetu". 

Mifumo ya chakula hutoa karibu theluthi moja ya gesi chafuzi duniani, husababisha ukataji miti na kusababisha karibu asilimia 80 ya upotezaji wa bioanuwai. 

Mbali ya uharibifu wa mazingira, la kushangaza, ni kwamba karibu theluthi moja ya chakula kinachozalishwa kila mwaka hupotea au kutupwa. 

Lengo la mkutano huo ni kuendeleza mikakati ya kupambana na changamoto za ulimwengu kama vile njaa, mabadiliko ya tabianchi, umaskini na ukosefu wa usawa na kuunda mifumo mipya ya chakula ambayo inawanufaisha watu wote na kuilinda sayari dunia. 

Mmomonyoko wa pwani unaonekana karibu na Grenville, Grenada, katika kisiwa cha Karibea.
NOOR/Kadir van Lohuizen
Mmomonyoko wa pwani unaonekana karibu na Grenville, Grenada, katika kisiwa cha Karibea.

4)Kutabiri dhoruba ya tishio la hali ya hewa na usalama 

Katika kisiwa cha Ushelisheli, juhudi zinafanywa kuboresha ulinzi wa maeneo ya  pwani kutokana na mafuriko yanayosababishwa na dhoruba na kuongezeka kuongezeka kwa kIna cha bahari kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi sasa unatambuliwa kama suala ambalo sio tu ni janga la kimazingira, lakini pia ni zahma inayotuathiri sote. 

Umoja wa Mataifa umeyaelezea mabadiliko tabianchi kama "suala linaloongeza shinikizo katika uchumi, kijamii, na mifumo ya kisiasa ya kila nchi. 

Kwa mfano, ukame katika eneo la Sahel Kaskazini mwa Afrika ni jambo linalochangia mizozo, ukiondoa idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa na matarajio duni ya maisha. 

Kuna baadhi ya tafiti zimeunganisha mabadiliko ya tabianchi na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, na vile vile matukio ya hivi karibuni kama vile vita huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, na onghezeko la machafuko katika bonde la Ziwa Chad, chanzo cha maji kinachotumiwa na nchi kadhaa, ambacho kimeshuka kwa asilimia 90 tangu 1960. 

Habari za UN zitaripoti mjadala maalum wa Baraza la Usalama juu ya hali ya mabadiliko ya tabianchi na usalama, unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 Septemba. 

Saruji ya ujenzi wa majengo nayo inachangia katika uchafuzi wa hewa ya ukaa kutokana na jinsi ambavyo inazalishwa.
© UN-Habitat /Julius Mwelu
Saruji ya ujenzi wa majengo nayo inachangia katika uchafuzi wa hewa ya ukaa kutokana na jinsi ambavyo inazalishwa.

 
5) Kutozalisha hewa ukaa: kugeukia nishati safi na ya kuaminika 

Maswali yanayozunguka nishati ni kiini cha juhudi za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, kwa hivyo inaweza kushangaza kuwa mkutano wa mwisho wa kimataifa juu ya nishati uliofanyika chini ya usimamizi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , ulifanyika miaka 40 iliyopita. 

Kwa hivyo, ni wakati muafaka kwa ajili ya mkutano mpya, na mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu nishati utafanyika tarehe 24 Septemba.  

Unafanyika katika ulimwengu ambao unaangalia matumizi ya mafuta na nishati mbadala, tofauti san na ilivyokuwa miaka ya 1980. 
Ufikiaji wa nishati ya bei rahisi, ya kuaminika, endelevu na ya kisasa kwa wote, ni moja ya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) ambayo yanaunda Ajenda ya 2030 ya maendeleo ambayo ni, mwongozo wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mustakbali bora. 

Changamoto nyingine ambayo itajadiliwa katika mjadala huo itakuwa jinsi gani ya kutokomeza kabisa uzalishaji wa gesi chafuzi inayochangia pakubwa katika mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2050. 

Ni kazi kubwa, inayohitaji vitendo kabambe kuanzia sasa hivi. Hii ndio sababu mataifa, maeneo, biashara, mashirika yasiyo ya kiserikali na wengine watatakiwa kuwasilisha "mkataba wa nishati", wakiweka ahadi za hiari na mipango thabiti inayoelezea jinsi watakavyofanya kutimiza lengo hilo.