Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuwezi kusubiri miaka mingine 40, nishati safi na mbadala kwa wote ianze sasa:Guterres

Mwanafunzi akipita mbele ya shamba la upepo lenye megawati 150 nchini Ufilipino.
ADB/Al Benavente
Mwanafunzi akipita mbele ya shamba la upepo lenye megawati 150 nchini Ufilipino.

Hatuwezi kusubiri miaka mingine 40, nishati safi na mbadala kwa wote ianze sasa:Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni miaka 40 sasa tangu suala la nishati lilipojadiliwa katika mkutano wa ngazi ya juu, na leo hii dunia inakabiliwa na ukweli kwamba karibu watu milioni 760 bado wanakosa fursa ya nishati ya umeme huku wengine bilioni 2.6 bado hawana fursa ya kupata nishati safi ya kupikia. 

Guterres amekumbusha hayo wakati akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu nishati unaofanyika kandoni mwa mjada mkuu wa wazi wa Baraza Kuu ambao leo umeingia katika siku ya 4 na kuongeza kwamba “Jinsi tunavyozalisha na kutumia nishati ni chanzo kikuu cha mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi. Hewa chafuzi itokanayo na nishati ni takribani asilimia 75 ya gesi yote chafuzi ya viwandani.” 

Kwa hivyo, amesema “Tuna umuhimu mara mbili wa kumaliza umaskini wa nishati na kupunguza mabadiliko ya tabianchi. Na tuna jibu ambalo litatimiza maagizo yote mawili. Nishati nafuu, mbadala na endelevu kwa wote. Hili ndilo lengo na ni lengo la maendeleo endelevu  namba 7.” 

Guterres amesisitiza kuwa kuwekeza katika nishati safi, ya bei rahisi kwa wote kutaboresha ustawi wa mabilioni ya watu na kunaweza kuunda ajira zinazojali mazingira ambazo tunahitaji haraka ili kujikwamua na janga la COVID-19 na pia kutasongesha malengo yote ya maendeleo endelevu na ni suluhisho moja muhimu zaidi la kuepusha janga la mabadiliko ya tabianchi. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ( Kulia) akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu nishati
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ( Kulia) akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu nishati

Rasilimali zinazohitajika tunazo  

Katibu Mkuu amesema  karibu nyenzo zote zinazohitajika zipo katika nchi nyingi  “Tuna nishati ya jua ambayo sasa ndio chanzo cha bei rahisi cha nishati. Sekta ya nishati mbadala inazalisha kazi mara tatu zaidi kuliko sekta ya mafuta. Nguvu ya jua na upepo ni nyota zinazoinuka za mfumo wetu wa nishati. Wakati wa janga la COVID-19, vyanzo hivi vya nishati ndio pekee viliweza kuendelea. Lakini kasi iko polepole mno kwani bado tuko mbali kuweza kutoka kwenye nishati chafuzi na kuhamia kwenye nishati safi na ya bei rahisi kwa wote.” 

Akitolea mfano barani Afrika amesema katika nchi 11 za Kusini mwa Jangwa la Sahara, robo ya vituo vya afya haviwezi kupata umeme. 

Karibu watu 9 kati ya 10 ulimwenguni wanapumua hewa iliyochafuliwa, ambayo ndio sababu ya vifo vya mapema vya watu milioni 8 kila mwaka. 

Ameongeza kuwa majanga ya asili, yanayokuzwa na mabadiliko ya tabianchi, yanaongezeka, upataji wa vyanzo bora vya nishati safi ni suala la maisha na kifo. 

“Wanawake na wanaume,wapendwa, tunahitaji kutatua shida hizi katika miaka kumi ijayo na lazima tuanze leo. Ikiwa hatutaondoa haraka na kwa kasi mifumo yetu ya nishati kwa miaka kumi ijayo, hatutaweza kupunguza kiwango cha joto hadi kufikia nyuzi joto 1.5 za Celsius, kulingana na lengo lililowekwa katika mkataba wa Paris nah ii itakuwa pigo mbaya kwa malengo ya maendeleo endelevu kwa sisi wote na sayari.” 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema katika hotuba yake kwamba mabilioni ya watu wataanguka katika umaskini na magonjwa, wakati mifumo ya ikolojia tunayotegemea itafutwa. 

“Huu ni udhalimu mkubwa kwa vizazi vya leo na kesho. Lakini hatujahukumiwa kwa hatima hii ya giza. Sayansi inatuonyesha haswa jinsi ya kuikwepa. Ili kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5 Celsius, uzalishaji wa hewa chafuzi lazima upunguzwe kwa asilimia 45% kutoka viwango vya 2010 ifikapo mwaka 2030 na kutokomeza kabisa uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo 2050. Kila nchi ina jukumu la kutekeleza hili.m Lazima tutimize ahadi iliyotolewa kwa nchi zinazoendelea kuchangisha dola bilioni 100 kwa mwaka kwa ajili ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.” 

Umeme wa jua unatumika sana nchini Indonesia kuwapatia wanajamii nishati endelevu
ADB/Sean Crowley
Umeme wa jua unatumika sana nchini Indonesia kuwapatia wanajamii nishati endelevu

Fedha za ufadhili zitumike ipasavyo 

Bwana Guterres amehimiza kuwa  asilimia 50 ya fedha za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji kutumiwa katika hatua za kukabiliana na hali na kujenga mbepo dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa siku zijazo. 

Mkutano wa leo unawakilisha tukio la kihistoria. Ninategemea nchi zote na haswa watoaji wakubwa wa hewa chafuzi kuongeza jukumu hilo, pamoja na wadau wakuu katika ulimwengu wa biashara na fedha. 

‘’Nimefurahi kuona kuwa watoaji wakuu kadhaa wa hewa chafuzi nchi zote na viwanda wanaonyesha uongozi katika Mazungumzo haya ya ngazi ya juu, na kuonyesha ahadi za ujasiri za kuchukua hatua.’’ 

Katibu mkuu ametanabaisha vipaumbele vikubwa vinne kwa ajili ya mustakbali wa nishati endelevu kwa wote ambavyo ni   

  1. Mosi: lazima kuziba pengo la ufikiaji wa nishati ifikapo mwaka 2030. Hiyo inamaanisha kupunguza nusu ya idadi ya watu wasio na huduma ya umeme ifikapo 2025. Na inamaanisha kuwapa zaidi ya watu bilioni 1 fursa ya ufikiaji wa suluhisho safi za nishati ya kupikia ifikapo 2025. Ameongeza kuwa gharama ya kuziba pengo la ufikiaji wa nishati ni ya kawaida: karibu dola bilioni 35 kwa mwaka kwa upatikanaji wa umeme na dola bilioni 25 kwa mwaka kwa nishati safi ya kupikia. 
  2. Pili: lazima tuhamie haraka katika mifumo ya nishati mbadala. Kufikia 2030, uwezo wa jua na upepo unapaswa kuongezeka mara nne kwa mtiririko huo kuwa gigawati 630 na 390 zitakazoongeza uwezo wa uzalishaji nishati kila mwaka. Na lazima tuongeze juhudi zetu za kuboresha ufanisi wa nishati. Haipaswi kuwa na mitambo mipya ya makaa ya mawe iliyojengwa baada ya 2021. Nchi za OECD lazima zijitolee kutokomeza matumizi ya makaa ya mawe yaliyopo ifikapo mwaka 2030, na nchi zingine zote zifuate nyayo ifikapo mwaka 20. Hakuna sababu ya nchi au wawekezaji kufadhili utafutaji mpya wa mafuta, leseni au miundombinu ya uzalishaji wake. Ufumbuzi safi wa nishati mbadala hutoa fursa bora za biashara. Amesisitiza kwamba ushirikiano wa kimataifa lazima uongezwe kwa kasi ili kuchochea fedha na uwekezaji unaohitajika kuharakisha mabadiliko kama haya ya nishati, haswa katika nchi zinazoendelea na nchi za visiwa vidogo zinazoendelea. 
  3. Tatu: Ili kufikia lengo la nishati kwa wote ifikapo mwaka 2030 na kutimiza utokomezaji kabisa wa hewa ukaa katikati ya karne hii, lazima tuhamasishe fedha zinazohitajika na kukuza uhamishaji wa teknolojia kwa nchi zinazoendelea. “Tunahitaji uwekezaji mara tatu katika nishati mbadala na ufanisi wa nishati hadi dola trilioni 5 kwa mwaka. Na benki zote za maendeleo na pande nyingi, kikanda, na kitaifa zinahitaji kusaidia nchi zinapobadilisha uchumi wao. Fedha za umma na za kibinafsi lazima zihamasishwe haraka na kupelekwa kwa kiwango kinachohitajika ili kuharakisha utokomezaji wa uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe.” 
  4. Nne: lazima tuhakikishe hakuna mtu aliyeachwa nyuma kwenye mbio hizi kwa siku zijazo. Hatyua za kuhamia nishati safi duniani lazima ziwe za haki, ujumuishe, na za usawa. Kuwekeza katika nishati mbadala badala ya kutumia mabilioni kutzalisha mafuta kisukuku kunaweza kuunda makumi ya mamilioni yaajira nzuri na kuwapa uwezo walio hatarini zaidi. 

Kila nchi, mjini, taasisi za kifedha, makampuni na jumuia za kiraiya zina jukumu katika kujenga mustakabali endelevu na wenye usawa wa nishati. 

“Leo, natoa wito kwa serikali zote kujenga ushirikiano wa kimataifa na kutoa msaada wa fedha zinazohitajika kwa ajili ya kuwa na uhamaji wenye usawa, jumuishi na endelevu ambao unahakikisha upatikanaji wa nishati mbadala kwa wote. Hatuwezi kusubiri miaka mingine 40 zaidi. Wakati wa upatikanaji wa nishati mbadala, ya bei rahisi kwa wote lazima uanze leo.” 


TAGS: Nishati, SDGs, nishati mbadala, UNGA76