Mtazamo wa matumaini ndio umetukwamua Madagascar – Rajoelina

Rais Andry Rajoelina wa Madagascar akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York Marekani
UN/Cia Pak
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York Marekani

Mtazamo wa matumaini ndio umetukwamua Madagascar – Rajoelina

Afya

Viongozi na wakuu wa nchi na serikali wanaoshiriki mjadala wa mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 hii leo wamejulishwa kuwa mtazamo wa matumani ndio muarobaini wa Madagascar baada ya kukumbwa na ugonja wa Corona au COVID-19.
 

Akihutubia mkutano huo, Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amesema “nchi yangu imeweza kuhimili athari za COVID-19 kwa kuwa badala ya kusalia na mshtuko tumeamua kupitisha mtazamo wa matumaini ili tuweze kufikia dira yetu. COVID-19 haikutuzuia kuendeleza mipango yetu ya maendeleo.”

Ametaja hatua ambazo wamejifunza kutokana na janga la Corona na hivyo kuchukua hatua thabiti ili kujenga mnepo kwa majanga ya afya ya usoni ni miundombinu ya afya akisema,  “lengo letu ni kuanzisha afya kwa wote. Kwa kujenga hospitali na vituo vya afya katika mikoa yote na wilaya zote za Madagascar.”

Mama nchini Madagascar akisubiri mgao wa chakula huku akiwa amembeba mwanae katika taifa hilo linalokumbwa na ukame kwenye maeneo ya kusini.
© WFP/Fenoarisoa Ralaiharinony
Mama nchini Madagascar akisubiri mgao wa chakula huku akiwa amembeba mwanae katika taifa hilo linalokumbwa na ukame kwenye maeneo ya kusini.

Athari za Mabadiliko ya Tabianchi

Wakati dunia inakabiliana na COVID-19, janga la mabadiliko ya tabianchi nalo limekuwa sambamba. Mfululizo wa matukio ya mafuriko na vimbunga vikali Ulaya, Afrika, Amerika na Kusini-Mashariki mwa Asia halikadhalika mioto ya nyika Australia na Marekani vimesalia ni tishio huku Madagascar nayo ikiwa miongoni mwa muathirika wa mabadiliko ya tabianchi.

Wimbi la ukame kusini mwa nchi limekausha vyanzo vya maji na kukwmaisha shughuli za kujipatia kipato ikiwemo kilimo.

“Nchi za kusini kama sisi zinabeba mzigo wa janga la tabianchi ambalo hazikusababisha.”

Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, Madagascar imetangaza hatua kunusuru wananchi ikiwemo kujenga bomba kubwa la maji kusambaza maji katika ukanda wa kusini “ili kufanikisha umwagiliaji na kuwezesha wakazi wa eneo hilo kulima na kujipatia kipato. Mradi huu mkubwa wa maji ni ahadi ya kipekee kutoka kwa serikali kwenda kwa wananchi.”

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na wa serikali ya Madagascar wakipokea shehena ya chanjo za Covid-19 katika Uwanja wa ndege wa Antananarivo.
© UNICEF/Rina Andrianandra
Maafisa wa Umoja wa Mataifa na wa serikali ya Madagascar wakipokea shehena ya chanjo za Covid-19 katika Uwanja wa ndege wa Antananarivo.

Tusioneshe taswira ya umaskini tu

Katika hotuba yake Rais huyo wa Madagascar amezungumzia suala la nchi kama za Afrika kuoneshwa kama nchi maskini zisizo na maendeleo yoyote.

“Unajua ambacho huniacha na fikra nyingi ni kwamba unapozungumzia nchi iliyoko kwenye mchakato wa maendeleo kama Madagascar, mara nyingi upande unaozungumziwa au taswira inayooneshwa kimataifa ni ule hasi, kimaskini. Tunapozungumzia Afrika, mara nyingi tunaweka kiza kwenye uhalisia wake.” amesema.
Rais Rajoelina amesema “ni wakati sasa kubadili mtazamo huo, na tuache kusambaza fikra hizi potofu. Ni kama vile mchakato wa COVID-19 uliochapishwa ukitabiri kuwa hali ya kutisha ya kiafya Afrika kutokana na janga hilo. Lakini hatimaye Afrika na nchi zilizotabiriwa kuwa hatarini zimethibitisha vinginevyo.”