Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itikadi za misimamo mikali tusambaratishe bila uoga- Kagame

Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia kwa njia ya video mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani tarehe 22 Septemba 2021
UN/Cia Pak
Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia kwa njia ya video mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani tarehe 22 Septemba 2021

Itikadi za misimamo mikali tusambaratishe bila uoga- Kagame

Amani na Usalama

Rais Paul Kagame wa Rwanda amehutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 na kusisitiza umuhimu wa kuwa na uongozi jumuishi wa wananchi na uwajibikaji.
 

Katika hotuba yake ya kurasa 7, ambayo Rais Kagame ametoa kwa njia ya video kutoka Kigali, Rwanda, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha siyo tu ustawi na maendeleo bali pia usalama, utulivu na imani kwa mustakabali wa dunia na taifa.

Hata hivyo amesema sambamba na hilo “ni lazima kubaini mapema na kusambatarisha bila kuchelea na bila utata itikadi za misimamo mikali inayochochea ugaidi na mauaji ya kimbari. Hatuwezi kucheza mchezo wa kisiasa.”

Katika nchi zinazoendelea kama Rwanda, watu walio katika hatari kubwa ya kuathirika na janga la COVID-19 ndio wanaopewa kipaumbele
WHO
Katika nchi zinazoendelea kama Rwanda, watu walio katika hatari kubwa ya kuathirika na janga la COVID-19 ndio wanaopewa kipaumbele

COVAX imetunusuru

Rais Kagame pia amezungumzia suala la mgao wa chanjo akisema licha ya mifano ya kusikitisha katika mshikamano wa chanjo duniani wakati wa COVID-19 bado mfumo Umoja wa Mataifa wa mgao wa chanjo, COVAX licha ya changamoto zake umekuwa mfano wa maadili bora ya Umoja wa Mataifa.

Ni lazima kubaini mapema na kusambatarisha bila kuchelea na bila utata itikadi za misimamo mikali inayochochea ugaidi na mauaji ya kimbari- Paul Kagame, Rais wa Rwanda

“Bila mfumo huu, pengo la chanjo Afrika lingalikuwa kubwa zaidi. Lakini tunaweza na tunapaswa kuchukua hatua zaidi na kuongeza kasi ya mgao wa chanjo Afrika. Kwa kufanya hivyo kunakuwa ni manufaa kwa dunia nzima. Hatua chanya kutoka kwa baadhi ya wadau na kampuni za kujenga uwezo wa kuzalisha chanjo Afrika nazo zinaungwa mkono,” amesema Rais Kagame ambaye nchi yake ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kupokea chanjo za COVID-19 kupitia COVAX.

Ajenda yetu ya Pamoja

Rais huyo wa Rwanda ametumia pia hotuba yake kuunga mkono ripoti ya Ajenda Yetu ya Pamoja iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hivi karibuni.

“Katibu Mkuu ana haki ya kuonya juu ya uwezekano wa kusambaratika kwa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, kuongezeka kwa mizozo, dharura ya tabianchi na ufukara,” amesema Rais Kagame.

Amesema hilo litakuwa na madhara makubwa na hivyo “ni lazima zote tuwe makini. Mpango wa Katibu Mkuu unapaswa kuungwa mkono nasi sote hususan umuhimu wa kuwa na mpango wa chanjo duniani, kurejesha imani baina ya serikali na wananchi wao, kujikita zaidi kwa vijana na kuchagiza zaidi matumizi ya sayansi.”

Rais Kagame amesisitiza kuwa iwapo “tunaweza kukutana sote ukumbini wakati wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu mwaka 2022 au mkutano wa viongozi kuhusu mustakabali wa baadaye ambao Katibu Mkuu amependekeza, yote hii itategemea hatua tutakazochukua siku za usoni. Tukiazimia na kuwa makini tunaweza kufanikiwa.”