Afrika imejipanga kujinasua na COVID-19 lakini uhisani uongezeke- Tshisekedi

21 Septemba 2021

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, ni miongoni mwa viongozi waliohutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 siku ya Jumanne ambapo amesema bara la Afrika tayari lina mkakati dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 lakini kinachohitajika sasa ni ufadhili wa fedha ili uchumi wao uweze kukwamuka.
 

“Ushindi dhidi ya COVID-19 unawezekana pale tu vita dhidi yake itakuwa ni ya kila mtu na iwapo tutafanikiwa kujenga kinga dhidi ya virusi hivyo kwa kila mkazi wa dunia,” ameonya Rais Tshisekedi ambaye nchi yake imekuwa mwenyeiti wa Muungano wa Afrika AU tangu mwanzo wa mwaka huu.

Hata hivyo amesema Afrika kwa upande wake haijabweteka na haina mpango wa kusalia nyuma na  badala yake imeweka mkakati wa pamoja wa bara dhidi ya COVID-19 akitaja mfano wa kuundwa kwa jukwaa la AVAT ambalo linawajibika kusaka chanjo na kuzisambaza kwa nchi zote pamoja na vifaa na teknolojia zinazotakiwa.

Ameongeza kuwa suala kwamba tarehe 28 mwezi Machi mwaka huu wa 2021 bara la Afrika kupitia AVAT iliingia makubaliano ya kununua dozi milioni 220 za chanjo ya COVID-19 ambapo baadhi ya nchi tayari zilianzisha mradi wa kuwa na Wakala wa Dawa Afrika huku nyingine tayari zimeanza kuzalisha chanjo baada ya kupatiwa leseni.

“Ifikapo Januari mwaka 2022, idadi ya chanjo zitakazokuwa zimesambazwa Afrika zitazidi milioni 25  kwa mwezi,” amesema Rais huyo wa DRC.

Mgao wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unapaswa kuimarishwa.
© UNICEF/Zoe Mangwinda
Mgao wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unapaswa kuimarishwa.

Nchi maskini ziko katika mazingira magumu

Rais Tshisekedi pamoja na kuelezea mipango hiyo ya Afrika amerejelea suala ya kwamba janga la Corona siyo tu limeua watu bali pia ni virusi ambavyo vimesababisha uchumi wa dunia kutumbikia katika mdororo hasa kwa nchi maskini na tegemezi, nyingi zao zikiwa ni za Afrika.

“Katika mazingira ya sasa ya janga la kiafya kutokana na janga la COVID-19, uchumi wa nchi za Afrika ziko katika mahitaij makubwa ya fedha ili ziweze kujikwamua, hasa kwa kuzingatia kuwa mbinu za kitaifa za kujijengea mnepo zimekuwa za shida ikilinganishwa na katika nchi tajiri. Kwa hiyo hali na mikakati ya kujikwamua bila shaka itaendelea kuongeza pengo la ukosefu wa usawa kati ya nchi za Afrika na nyinginezo duniani.”

Tunakaribisha mipango ya ufadhili ya kunasua Afrika

Ni kwa mantiki hiyo amesema bara la Afrika linakaribisha mipango yote inayohusiana na kuzipatia ufadhili wa fedha nchi za Afrika zilizoathirika kiuchumi kutokana na janga la COVID-19, hususan mikakati ya kundi la nchi 20 zenye uchumi wa juu, G20 za kusamehe ulipaji madeni na mfumo mpana wa kupanga upya ulipaji wa madeni na zaidi ya yote kutenga dola bilioni 650 katika mfumo wa haki ya ukopaji, SDR kutoka shirika la fedha duniani, IMF kuwezesha nchi zilizoathirika na janga ziweze kujinasua.

“Hata hivyo dola bilioni 33 zilizotengwa kwa bara la Afrika kupitia SDR hazitoshelezi kulingana na kiwango cha fedha za kuchechemua uchumi zinazohitajika,” amesema Rais huyo wa DRC.

Hivyo amesema ndio maana “ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa na wanachama wake kuunga mkono lengo la mkutano wa Paris la kufikia uchangiaji wad ola bilioni 100 za SDR kwa Afrika, ambapo asilimia 25 zinaelekezwa nchi maskini.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter