Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Programu ya UNICEF nchini kenya yawasaidia watoto wa kike kurejea shuleni

Binti akiwa ameshikilia vitabu msaada wa Umoja wa Ulaya kwa watoto wakimbizi katika kambi ya Dadaab nchini Kenya
© UNHCR/Mohamed Aden Maalim
Binti akiwa ameshikilia vitabu msaada wa Umoja wa Ulaya kwa watoto wakimbizi katika kambi ya Dadaab nchini Kenya

Programu ya UNICEF nchini kenya yawasaidia watoto wa kike kurejea shuleni

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF kwa kushirikiana na serikali ya Kenya wanaendesha program maalum ya “Elimisha mtoto” inayowachagiza wazazi na watoto wa kike walioacha shule wakati wa janga la corona au COVID-19, kwa sababu ya mimba za utotoni, na sababu nyingine kurejea shuleni.

Binti Christine Aleper mwenye umri wa miaka 16 ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Namoruputh kaunti yaTurkana. Ni miongoni mwa wasichana wengi ambao waliacha shule kwa sababu ya mimba za utotoni, ndoa za mapema, na kazi za majumbani. 

Kwa Christine sababu kubwa ilikuwa kufanyishwa kazi za majumbani na baba yake kutaka kumuoza mapema, lakini alikataa na sasa amerejea shuleni kupitia programu ya “Elimisha mtoto”  

“Siku moja chifu alikuwa anazungumza kwenye mkutano wa jamii, alisema hakikisheni mnapeleka watoto wenu shuleni. Nikamuuliza baba yangu endapo ninaweza kwenda shule lakini alikataa, baba yangu anataka kunioza kwa mzee, mimi nikaamua acha niende shule peke yangu , nilivua ushanga wangu wa kimila nikaondoka. Na sasa najihisi vizuri kwa sababu nimejifunza kusoma na ninaelewa na kuzungumza Kiswahili” 

Kwa mujibu wa naibu chifu wa Namoruth Matthew Koringang Lemuya wazazi wengi wanawaona watoto wa kike kama kitega uchumi. “Kimila jamii imezoea kufikiri kwamba wasichana ni bidhaa kwa ajili ya kupata mahari, na pia kuna hukla katika jamii yetu ya kumuona mwanamke ni mtu wa chini”. 

Programu ya elimisha mtoto inayofadhiliwa na UNICEF imemsaidia Christine ambaye alikuwa binti mwenye haya, amebadilika na sasa anafurahia elimu na utoto wake na waalimu wake wanatumai siku moja atakuwa mfano wa kuigwa na wasichana wengine katika jamii yake.  

Andrew Brown ni mkuu wa mawasiliano, utetezi na ushirikiano wa UNICEF nchini Kenya anasema “Wakati wa janga la COVID-19 tumeshuhudia watoto wengi wakiacha shule na sio wote waliorejea , UNICEF kupitia program yetu ya kuwasaidia watoto walioacha shule tunashirikiana na serikali na machifu wa kimila kujaribu kupinga hulka na mila zilizokita mizizi na kujaribu kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kupeleka mtoto shule awe msichana, mvulana au mwenye ulemavu”.

UNICEF inasema mradi huu sio tu unampa mtoto fursa ya kusoma bali pia unamfungulia mlango wa mustakabali bora.